NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli, sasa ameanza kufanya vituko kwa kuwazuia waandishi wa habari kuingia na vitendea kazi vya aina yoyote ofisini kwake wanapokwenda kufanya naye mahojiano.
Kigurumjuli ameweka mlinzi katika mlango wa ofisi yake anayechagua watu wa kuingia na pia anachagua nani na yupi asiingie ambapo leo asubuhi, mlinzi huyo ameizuia Tanzania PANORAMA Blog kuonana na bosi wake kwa ajili ya kufanya mahojiano ikiwa na ‘notebook’ na kalamu mpaka itii sharti la kuingia mikono mitupu.
Katika hatua ya kushangaza, Kigurumjuli pia, wiki iliyopita alitoa maneno ya kashfa na kejeli kwa viongozi waandamizi wa serikali pamoja na aidha; leo hakupokea simu wala kujibu meseji kwa watu aliopanga miadi ya kukutana nao ofisini kwake.
Vituko hivi vya Kigurumjuli vimekuja siku chache baada ya yeye mwenyewe kuieleza Tanzania PANORAKA Blog kuwa amepata presha hivyo hawezi kwenda kazini baada ya kuripotiwa kwa taarifa za kukwama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale huku taarifa nyingine zikieleza kuwa ana hasira kwa sababu ya kuripotiwa kwa mkwamo wa ujenzi wa soko la Tandale na amejiapiza kuwashughulikia wanaofuatilia habari hiyo.
Katika tukio la leo asubuhi, Kigurumjuli alikuwa ametoa miadi ya kukutana ili azungumzie matatizo yaliyokwamisha ujenzi wa soko la Tandale. Miadi hiyo haikufanikiwa baada ya mlinzi aliyemuweka mlangoni kutaka aachiwe vitendea kazi vyote vya Tanzania PANORAMA Blog ikiwa ni pamoja na begi alilotaka apewe alishike.
“Toa vitu vyako vyote kwenye kibegi chako weka hapo kwenye kiti, hilo begi nipe hapa nilishike ukitoka utachukua vitu vyako nitakupa na begi lako,” alieleza mlinzi ambaye jina lake halikufahamika.
Alipoelezwa kuwa ndani ya begi kuna kalamu, ‘notebook’ na nyaraka kadhaa na kufunguliwa akague na mwandishi alieleza yupo tayari kupekuliwa, alisisitiza kuwa bosi wake ameagiza waandishi wasiingie na kitu chochote isipokuwa wao tu.
“Hii ni amri, kalamu na karatasi zako toa weka kwenye kiti, begi nipe hapa nitakushikia hatuna sababu ya kubishana,” alisema kwa msisitizo.
Tanzania PANORAMA Blog haikumpatia begi mlinzi huyo kama alivyokuwa akisisitiza kwa sababu lilikuwa na taarifa za kuwepo kwa mipango miovu ya kupandikiziwa vitu visivyofaa kisha wangeitwa wana usalama kupekua begi hilo na kukuta vitu hivyo kabla ya kuwatia matatani kwa lengo la kuwazuia wasiripoti taarifa za soko la Tandale.
Kabla ya kuondoka eneo hilo, lilimpigia simu Mkurugenzi huyo kumjulisha hali halisi ilivyo hapo nje ya mlango wa ofisi yake, simu yake ilisikika ndani ikiita lakini hakuipokea na pia alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno mara tatu ambao aliusoma lakini hakujibu.
Katika mahojiano ya wiki iliyopita kuhusu kukwama kwa ujenzi wa soko la Tandale na kuweka zuio kwa waandishi wa habari kiripoti habari za soko hilo bila ruhusa yake, Kigurumjuli alisema yeye binafsi ndiye aliyekwenda kutafuta fedha za ujenzi wa soko la Tandale, Wizara ya Fedha na Mipango na alipewa za kutosha ila tatizo lililopo sasa ni kukosekana kwa saruji.
Alipoulizwa sababu iliyomfanya yeye binafsi kwenda wizarani kushawishi kutolewa kwa fedha huku tayari aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jaffo akiwa amekwishatoa tamko kuhusu ujenzi wa masoko yaliyokuwa kwenye mpango wa kujengwa….. haraka alilikatisha swali hilo na kuanza kung’aka.
“Ni kinini hicho, Selemani Jafo ndiyo kitu gani hicho. Hapa unaongea na Mkurugenzi, upo ofisini kwa mkurugenzi usinitajie majina ya ajabu ajabu wewe. Huyo Jafo wakati nahangaika hazina alikuwepo?
Kigurumjuli
“Fedha nimetafuta mimi na nimepewa mimi na nimekujibu hivyo au ulisikia kuna Jafo au huyo mkuu wenu wa mkoa? Wao kazi si kutembea tu na ….. (anasema maneno yasiyofaa) kwenye miradi tunayotafuta sisi. Hivi sasa tuna tatizo la saruji usiniletee mambo ya wanasiasa hapa. Uliza swali jingine,” alisema kwa sauti ya juu Kigurumjuli.
Aidha Kigurumjuli alikana kutoa maagizo kwa mkarandasi yanayowataka waandishi wa habari kuwa na vibali vya maandishi kutoka kwake wanapotaka kuripoti habari za ujenzi wa soko la Tandale.
Taarifa ya kuwepo kwa zuio hilo kwa waandishi wa habari lilitolewa na meneja miradi wa Kampuni Namis, James Msumali ambaye baada ya kufikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuombwa kuzungumzia mkwamo huo alisema mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutolewa kwa taarifa yoyote ya ujenzi wa soko mpaka kiwepo kibali cha maandishi kutoka Kigurumjuli.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Namis Thomas Uiso ambaye awali alikuwa ameitaka Tanzania PANORAMA Blog kumpelekea maswali kwa maandishi ili naye apate wasaa mzuri wa kuyajibu, ombi ambalo lilitekelezwa, alipotafutwa wiki iliyopita aliandika ujumbe wenye maneno machafu badala ya kujibu na muda mfupi baadaye aliufuta kisha alipiga simu na kueleza kuwa soko la Tandale linasimamiwa na Mkurugenzi ambaye ameagiza mwandishi yoyote anayetaka taarifa aelekezwe kwake.
“Maswali gani, wewe……(anaandika maneno ambayo hatuwezi kuyaandika). Nimepata taarifa zako mkurugenzi kanambia, hovyo sana wewe kumbe unachimba maisha ya watu. Ukimtaja Jafo au Kunenge ndiyo watu tutaogopa? Hao ni …….. (Anaandika maneno yasiyoandikika) huu ni utawala mwingine utapotea wewe na hutamuona Jafo wala Kunenge.
“Kuwa gentleman bhana, hapa ni mjini, haya ni maisha. Kwani unadhani hata nikiharibikiwa wewe ndiyo utapewa hiyo tenda? Ondoa huo uchafu ulioandika kwenye blog yako halafu kamuone mkurugenzi maisha yaendelee…., »alisema Uiso.
WIKI ILIYOPITA Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa, WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo zimeanza kuonyesha dalili ya kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.
Katikati ya hilo, msimamo wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo bila ukiritimba, zinazofanywa na serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua miradi inayotekelezwa kwa kodi zao, nao unaonekana kuingia doa baada ya mkandarasi anajenga soko la Tandale kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.
Haya yamebainika baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema wiki iliyopita kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa na baadhi ya wafanyakazi kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Tanzania PANORAMA baada ya kufika katika eneo la mradi lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku ujenzi ukiwa hauendelei na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri kulipwa fedha zao waondoke kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.
“Bora umekuja na sijui umeingiaje huku maana hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona watakugawana. Hapa hakuna kazi kama unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha. Tunasikia bosi hajalipwa huko serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini sisi tumeambiwa tukiulizwa tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la kitaifa kwa sasa.
” Kama unaweza twende tukupeleke kwa msimamizi wetu ukamuhoji ila uwe unajiamini. Ila sisi tunasubiri akipata pesa kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu nyingine maana hata wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa tunajiuliza hiyo serikali inatoa hela kwa wiki?” alisema mmoja wa mafundi hao.
Msimamizi wa mradi ambaye alipofikiwa na Tanzania PANORAMA na kuulizwa kwanza alielekeza afuatwe ofisini ambako alichukua simu na kuwasiliana na makao makuu ya kampuni yake kisha alisema;
“Unasema kuna wenzako kwenye gari wanakusubiri …. umesema hujapiga picha…. hili ni eneo la site, mtu yoyote haruhusiwi kuingia humu bila kibali cha makao makuu, awe mkuu wa mkoa, awe waziri anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza kuangukiwa na kitu kizito kama nondo au ubao ukaaumia.
“Sasa nimeongea na makao makuu, nadhani umeona naongea na simu, kama una maswali nenda huko watakujibu na kama unataka kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka makao makuu.
“Tena tumekuheshimu sana kwa sababu umeingia eneo ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje njoo nikipitishe njia salama usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo, ” alisema.
Tanzania PANORAMA lilifika Makao Makuu ya Kampuni ya Namis, iliyopo Mbezi Africana ambayo ndiyo iliyopewa kandarasi ya kujenga soko la Tandale kwa ajili ya kupata maelezo ya kasimama kwa ujenzi wa soko hilo na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Akizungumza kuhusu katazo hilo lililo kwenye mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la James Msumali alisema changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza kuzizungumzia iwapo atapata idhini ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.
“Mimi ndiyo meneja mradi na ndiye ninayeweza kuzungumza, boss unayetaka kuonana naye hayupo. Utaratibu upo hivi, mkataba wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa yoyote ya mradi haiwezi kutolewa mpaka kwa Kibali cha Mkurugenzi.
“Tena Kibali cha maandishi au anipigie simu yeye mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda Manispaa kamtafute Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje nikueleze hicho unachotafuta,” alisema Msumali.
Alipofikiwa na kuelezwa hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli alihoji ni kwanini Tanzania PANORAMA linafuatilia mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye kelele nyingi badala ya kuandika maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa la ofisi ya Mkurugenzi au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
“Kwanini Ujenzi wa Soko la Tandale ambalo lina kelele nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa, kwanini huandiki kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dad es Salaam?
” Lakini nimeitwa mahali sasa siwezi kuwasiliza kwa sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni kesho,” alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa siku iliyofuata alisema kusimama kwa mradi huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa kuhusu zuio la kuandika habari za soko hilo alisema halitambui isipokuwa mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia katika miradi ya aina hiyo.
“Hilo zuio silijui na nitoe barua kwa mwandishi kwenda kuandika habari kutok lini hiyo. Hao watakuwa na yao lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa kufuata utaratibu maalumu ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi,” alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Namis Corporate Ltd, Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza aulizwe meneja mradi, Msumali.
Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hilo.