NA CHARLES MULLINDA
KUNA mijadala mingi inayoendelea kuhusu kushambuliwa na Serikali na Bunge kumtelekeza kwa kutomlipia gharama za matibabu, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Liss aliyeshambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017, alipokuwa akitoka kwenye kikao cha Bunge kurejea nyumbani kwake eneo la area D, jijini Dodoma kwa mapumziko ya mchana.
Mijadala ni mikali hasa kwenye mitandao ya kijamii ambako baadhi ya wachangiaji, kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu uamuzi wa familia ya Lissu na Chadema kuiweka pembeni Serikali na Bunge kujihusisha kwa namna yoyote ile na matibabu ya Lissu.
Lissu mwenyewe ndiye anayeiibua mijadala hiyo na kuikoleza baada ya kurejea nchini hivi karibuni akitokea Ubelgiji alikokuwa akiishi. Hivi sasa anagombea urais na katika hotuba zake anazozitoa kwenye majukwaa ya kisiasa anapozunguza nchi nzima kusaka kura zitakazomuwezesha kuwa rais amekuwa akihubiri shambulio hilo dhidi yake tofauti ya uhalisia wake.
Mwandishi CHARLES MULLINDA alifanya uchunguzi wa kina kuhusu sakata hilo na kuandika ripoti maalumu ambayo haijawahi kukosolewa au kupingwa na Chadema, Lissu mwenyewe, Serikali, Bunge au chombo chochote cha kiuchunguzi ndani na nje ya nchi.
Ripoti hiyo ilichapishwa kwanza katika vyombo vya habari na hapa mwandishi anairejea ili kuweka kumbukumbu sahihi kuhusu tukio hilo.
Ripoti hii maalumu inaelezea mtiririko wa matukio baada ya shambulizi hilo la kusikitisha; utata wa Chadema kutaka kumchukua Lissu akiwa mahututi, matibabu ya awali aliyopatiwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma, ambayo yalimsaidia kusafiri salama hadi Nairobi Kenya, majadiliano baina ya Serikali, Bunge, familia ya Lissu, Chadema, NHIF na wadau wengine kuhusu wajibu na dhamana ya kumtibu, pamoja na taratibu za matibabu ya wabunge kwa ujumla.
Taratibu za matibabu kwa wabunge zimeonyesha kuwa wabunge wote, mawaziri na maspika wastaafu, wanastahili kupewa matibabu bure ndani na nje ya nchi; na Bunge linapaswa kugharamia matibabu hayo.
Hivyo, wabunge wote ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ikijumuisha wenza wao na watoto wanne wa umri usiozidi miaka 18. Na hii ni kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji Bunge, Sura Na.115 ya Mwaka 2008.
Taratibu hizo zimeonyesha kuwa mfuko husimamia matibabu ya wabunge ndani ya nchi kwa mujibu wa mkataba wa utoaji huduma hiyo uliopo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Konga Bernard alipohojiwa, alieleza kuwa taasisi yake haina dhamana yoyote kwa mtu ambaye ni mwanachama anapoamua kwenda kujitibu kwa gharama zake mwenyewe.
Kwa yake maneno yake aeleza; “Mwanachama anayeamua kwenda kujitibu mwenyewe sisi hatuna dhamana naye. Wanachama wetu huwa tunawaambia vituo au hospitali ambazo wanapaswa kwenda kutibiwa ambazo tuna mkataba nazo.
“Hospitali au vituo vya afya ambavyo tuna mkataba huwa vinatuletea madai baada ya kuwatibu wateja wetu wakiwamo wabunge na sisi tunalipa.
“Bima ya Afya ni kama bima ya magari, gari lisipogongwa haliendi kutengenezwa lakini likigongwa gharama ya kulitengeneza ni kubwa na pengine mtu anaweza kupewa gari jipya kabisa. Hivyo hivyo na Bima ya Afya ukiugua unaweza kutumia gharama kubwa sana kutibiwa.
“Lakini mtu anayeamua kujitibu mwenyewe ndani au nje ya nchi, huo ni uamuzi wake na sisi hatuna dhamana hapo kwa sababa kwanza ugonjwa ni siri ya mtu.”
Kauli hii ya Konga inatoa picha kuwa mbunge anapoamua kwenda kujitibu mwenyewe ndani au nje ya nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa na NHFI, gharama za matibabu yake anazibeba yeye mwenyewe.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga |
Utaratibu wa matibabu kwa wabunge na mawaziri unaonyesha kuwa matibabu ya wabunge nje ya nchi yanasimamiwa moja kwa moja na Bunge lenyewe.
Kunapokuwa na mahitaji ya mbunge kutibiwa nje ya nchi, jopo la madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) au Moi ndiyo hushauri na ndizo taasisii pekee zenye mamlaka ya kupendekeza kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Kwa mujibu wa taratibu hizo ili matibabu ya nje yafanyike ni sharti mbunge atibiwe katika hospitali za ndani zilizosajiliwa na NHIF na inaposhindikana ndipo rufaa ya kwenda Muhimibili au Moi hutolewa.
Endapo mbunge atapata rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hulitaarifu Bunge, ikiweka bayana hospitali anayokwenda kutibiwa, muda wa awali wa matibabu na endapo kuna hitaji la kusindikizwa na mwana familia, daktari au muuguzi, rufaa hiyo huweka bayana.
Wajibu wa Bunge baada ya kupokea rufaa, hufanya maandalizi ya safari ya nje, ikijumuisha gharama za matibabu ya mwanzo, kununua tiketi ya ndege, posho ya kujikimu kwa mbunge na msindikizaji au wasindikizaji na kibali cha kusafiri nje ya nchi kwa mujibu wa Amri ya Rais wa Awamu ya Kwanza “State House Clearance” kwa safari zote za nje bila kujali kama ni matibabu au shughuli nyingine yoyote kwa yeyote anayelipwa fedha za umma kusafiri nje ya nchi.
Mwalimu Julius Nyerere |
Rekodi zilizoko serikalini zinaonyesha kuwa haijapata kutokea kwa mbunge aliyepata rufaa kukosa kibali cha Ikulu cha kusafiri nje ya nchi kwa matibabu.
Sheria ya uendeshaji Bunge inaeleza kuwa mbunge ana haki ya kupata posho ya jimbo kila mwezi, mshahara wake pamoja na fedha za mfuko wa jimbo hata pale anapokuwa mgonjwa. Na katika uchunguzi wa sakata hili ilibainika pasipo shaka kuwa Lissu alikuwa akipatiwa stahiki zake hizo.
Uchunguzi ulionyesha kuwa Lissu alikuwa halipwi posho ya vikao na posho ya ushiriki na hilo limethibitishwa na mmoja wa maafisa wa Bunge wa Idara ya Uhasibu aliyetoa ushirikiano mkubwa wakati wa uchunguzi huu lakini jina lake limehifadhiwa kwa sababu siyo msemaji wa Bunge.
“Haki zake anapata kama ulivyo utaratibu, tunamlipa mshahara wake, tunampa posho ya jimbo na fedha ya mfuko wa jimbo lakini hapewi ‘sitting allowance’ na ‘per diem’ kwa sababu hizo ni lazima aingie kwenye vikao.
“Na fahamu kuwa mbunge akifanya safari binafsi nje ya nchi, Bunge haliwajibiki kumlipa yeye wala msaidizi wake ‘per diem’, hata akiwa mgonjwa halipwi kama kaenda binafsi kwa sababu anakuwa hana rufaa inayotambulika, utaratibu huo uko wazi,” alisema afisa huyo.
Taarifa zaidi zilizokusanywa kutoka ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, zilionyesha kuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo, matibabu endelezo ya wabunge na familia zao hufanyika nchini India katika Hospitali ya Apollo isipokuwa kama inapendekezwa tofauti kulingana na aina ya matibabu yanayotakiwa kutokuwepo India na katika Hospitali ya Apollo, ndiyo uamuzi wa matibabu mbali na India hufanyika.
Kwamba kama ilivyo kwa wabunge wote, Lissu alistahili kutibiwa katika hospitali na vituo vyote vilivyosajiliwa na NHIF kwa kuzingatia ‘medical scheme’ ya matibabu ya wabunge ambayo inampatia mbunge nafuu ya kulipiwa gharama zote, kusafirishwa kwa ndege au helikopta kokote atakapopata dharura ya matibabu na kuhitaji kupelekwa ambako kuna hospitali yenye utaalamu zaidi popote ndani ya nchi na huduma za gari la wagonjwa.
Hivyo, uchunguzi ulithibitisha kuwa Lissu aliposhambuliwa kikatili kwa risasi, gharama za matibabu yake zilipaswa kubebwa na NHIF kwa jinsi ile ile utaratibu unavyoelekeza na tayari jukumu hilo lilikuwa limekwishaanza kutekelezwa chini ya usimamizi wa Bunge
Lakini NHIF haikuweza kuendelea kutimiza wajibu wake huo baada ya familia ya Lissu na Chadema kumtwaa kwa kile walichoeleza kuwa hawakuwa na imani na Serikali wala Bunge kusimamia matibabu hayo.
Uchunguzi kuhusu sakata la Serikali na Bunge kutolipia gharama za matibabu ya Lissu ulionyesha kuwa baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma akiwa na majereha mengi ya risasi na akiwa amepoteza damu nyingi, wabunge wa Chadema wakiongozwa na mwenyeketi wao, Freeman Mbowe, dereva wa Lissu na wafuasi wao walizingira eneo la chumba cha upasuaji alikokuwa amelazwa wakitaka kumchukua ili wakamtibu mahali wanapopajua wao.
Ilielezwa na mashuhuda kuwa purukushani hiyo ilidumu kwa muda huku walinzi wa hospitali wakipambana na kundi hilo lenye hasira na jazba. Uongozi wa hospitali uliomba msaada wa askari polisi kutuliza jazba, lakini hawakufanya lolote zaidi ya kuangalia tu.
Matibabu waliohojiwa wanaeleza kuwa Lissu alifikishwa hospitalini na wana familia ya Naibu Spika, Tulia Ackson anayoishi nayo jirani eneo la Area D na gari lililotumika kumfikisha hospitalini hapo ni la Khadija Akukweti.
Naibu Spika, Dk Tulia Ackson |
Msimamo wa Mbowe, wabunge wa Chadema na wafuasi wao kutaka kumtwaa Lissu kutoka hospitalini waliujenga katika msingi wa kutokuwa na imani na hospitali za Serikali hivyo walitaka wapewe wakamtibu wenyewe mahali wanakokujua.
Wafanyakazi hao wanaeleza kuwa Lissu alifikishwa hospitalini akiwa na hali mbaya sana. Alikuwa na majereha mengi ya risasi na alikuwa amepoteza damu nyingi hivyo alihitaji matibabu ya haraka na hasa kuongezewa damu.
Kwamba kwa namna yoyote ile, kumuondoa hospitalini kama ilivyokuwa ikishinikizwa na Mbowe na wenzake lilikuwa jambo la hatari kwa sababu lingeweza kugharimu maisha yake.
Katika mahojiano hayo, matabibu nao walihoji busara ya kutaka kumchukua ilitoka wapi ikizingatiwa muda ule ilikuwa mchana, akiwa amepoteza damu nyingi na hajiwezi! Walitaka kumpeleka wapi ambako walikuwa na imani nako?
Mmoja wa manesi (jina tunalihifadhi) ameeleza kuwa kwa anayeijua Dodoma vizuri, zaidi ya hospitali za Serikali hakuna hospitali kubwa ambayo ingeweza kufanya walichokifanya madaktari wa Hospitali Rufaa ya Dodoma. Anasema hajui kama Lissu analijua hilo na dhamira ya wenzake ya kutompatia tiba mbadala.
Uchunguzi ulionyesha kuwa madaktari wa Hospitali ya Rufaa Dodoma pamoja na uongozi wa Bunge, kwa kutambua hatari ambayo ingeweza kutokea kwa Lissu iwapo asingepatiwa matibabu ya haraka na ya dharura, busara iliwaongoza kumuita Mbowe na Mchungaji Msigwa ofisini kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Dodoma kufanya naye kikao ili waruhusu Lissu atibiwe haraka kuokoa maisha yake.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Katibu wa Bunge.
Katibu wa Bunge Mstaafu, Dk. Thomas Kashillilah |
Katika kikao hicho yalifikiwa makubaliano kuwa ni lazima jitihada za kuokoa maisha yake zichukuliwe haraka hivyo Mbowe alitakiwa aruhusu mara moja aongezewe damu na afanyiwe upasuaji.
Makubaliano mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho ni uongozi wa Chadema kuwaondoa wafuasi wao wote waliokuwa wamejazana hospitalini hapo, polisi wote waliokuwa hospitalini waondolewe na Mkuu wa Mkoa (RC) na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) watoe taarifa rasmi juu ya tukio hilo, mambo ambayo yalitekelezwa
Ilielezwa na baadhi ya wanafamilia na jamaa wa karibu wa Lissu waliofikiwa wakati wa uchunguzi na kuzungumza huko Singida kuwa haina shaka hata kidogo kuwa Lissu hajapata kuambiwa hospitali ambayo wenzake walisena hawana imani nayo ndiyo ilimtibu kwanza kwa kumuongezea damu na kuziba majeraha ya risasi ili damu isiendelee kuvuja pamoja na kumfanyia upasuaji wa kwanza.
Kazi ya kuokoa maisha ya Lissu iliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya.
Dk. Mpoki Ulisubisya |
NHIF ilitafuta ndege kwa ajili ya kumpeleka Lissu Muhimbili kwa matibabu zaidi ambayo iliwasili Dodona majira ya Saa 10 jioni na kusubiri matibabu ya awali yakamilike ili asafirishwe kwenda Muhimbili au Moi.
Spika Job Ndugai |
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati tukio la Lissu kushambuliwa linatokea, Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa Dar es Salaam akiongoza ujumbe wa Bunge Ikulu ya Magogoni, ambako Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa akiwasilisha kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli taarifa za Kamati za Almasi na Tanzanite alizokuwa amepokea toka kwa spika jana yake mjini Dodoma.
Spika alirejea Dodoma baada ya kumalizika kwa tukio hilo na kwenda hospitalini kumjulia hali Lissu, lakini hakuweza kumuona kwa sababu alikuwa bado yupo katika chumba cha upasuaji.
Hata hivyo, Spika aliyepokelewa na Waziri wa Afya, alipokea taarifa ya mganga mkuu kwa Spika kuhusu hali ya Lissu ambaye madaktari walikuwa katika jitahida za kuokoa maisha yake.
Spika alielezwa kuwa Lissu angehitaji matibabu zaidi Muhimbili au Moi na endapo itakuwa haitoshi basi apelekwe nje ya nchi.
Baada ya Spika kupokea taarifa hiyo, aliongoza kikao kilichofanyika jengo la NHIF na kuhudhuriwa na Waziri wa Afya, ndugu wa karibu wa Lissu, Mbowe, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye pia ni Kamishna wa Bunge, na makamishna wengine wakiwemo Salim Turki, Idd Azzan Zungu, Katibu wa Bunge pamoja na mwakilishi wa NHIF ili kujadili matibabu yake zaidi.
Katika kikao hicho, Spika alipewa maelezo ya tukio zima lilivyotokea na hatua zilizochukuliwa na yeye alieleza wazi kuwa Bunge litatekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha Lissu anapata matibabu ndani na nje ya nchi endapo itahitajika kufanya hivyo.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu |
Lakini pia Waziri wa Afya, naye alisema jopo la madaktari litashauri kama ulivyo utaratibu iwapo Lissu atalazimika kwenda kutibiwa nje, Serikali itaridhia atapelekwa India au sehemu nyingine ambako itashauriwa lakini katika hatua ya kushangaza ndugu wa familia alishukuru kisha akasema hawahitaji msaada wa Serikali wala Bunge kumtibu Lissu.
Anakaririwa katika taarifa rasmi ya Bunge akieleza kwa maneno yake mwenyewe kuwa “familia ya Lissu na Chadema wanashukuru sana kwa ukarimu wa Serikali na Bunge lakini tunachokitaka ni ruhusa ya kumchukua tukamtibu sehemu nyingine ambako tuna imani nako kwa sababu hatuiamini Serikali wala Bunge na hatuko tayari kuona anapelekwa Muhimbili au Moi ambako Serikali itakwenda kummaliza kabisa.”
Huo pia ndiyo ulikuwa msimamo wa Chadema uliotolewa na Mbowe mbele ya kikao na kurekodiwa katika kumbukumbu rasmi za kikao hicho na kwamba waliitaka Serikali na Bunge visijihusishe kwa namna yoyote ile na Lissu kwa sababu hawakuwa na imani na mamlaka hizo.
Taarifa ya kikao hicho inakwenda mbali zaidi kwa kuonyesha kuwa Spika hakuwa na jinsi kwa sababu familia ya Lissu na Chadema hawakuwa na imani na taasisi anayoiongoza hivyo kwa mikono miwili alikubali matakwa ya familia na Chadema mbele ya makamishna wa Tume ya Bunge na Waziri wa Afya.
Lakini kumbukumbu zaidi za kikao hicho zinaonyesha kuwa Waziri wa Afya alitoa rai kwa familia na Chadema kuwa pamoja na uamuzi wao huo watoe muda kwa jopo la madaktari waliokuwa wakimfanyia upasuaji wamalize ndipo wamuandae kwa safari.
Inaeleza kuwa wakati kikao hicho kikiendelea, tayari Rais Dk. John Pombe Magufuli alikuwa amekwishamuagiza Waziri wa Afya kusimamia na kuratibu mipango yote ya matibabu ya Lissu na maagizo mengine alikwishatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia tukio hilo.
Rais John Pombe Magufuli |
Sehemu moja ya kumbukumbu ya kibunge ambayo inathibitishwa na mmoja wa maafisa wa Ikulu aliyezungumzia sakata hilo inonyesha kuwa Rais Dk. Magufuli alikuwa amemuagiza Waziri wa Afya kuharakisha mchakato wa rufaa ya Lissu kwenda Hospitali ya Apollo nchini India au kwingineko ambako ingeshauriwa na madaktari wa Muhimbili au Moi kwa jinsi hali yake ilivyokuwa na kwamba alikuwa akisuburi ushauri wa madaktari ili kutoa ridhaa tu.
Afisa huyo wa Ikulu alielzai kuwa baada ya uamuzi wa familia na Chadema wa kulazimisha kumchùkua Lissu huku wakiionyooshea kidole Serikali na Bunge kutaka kwenda kumuua iwapo angelazwa katika hosiptali za hapa nchini, Rais alipopewa taarifa hiyo aliinamisha kichwa chini kwa masikito na kwamba hakuzungumza chochote tena.
Chadema na familia ya Lissu baada ya kuitosa Serikali na Bunge na jukumu hilo kubaki mikononi mwao, walianza maandalizi ya kumpeleka Nairobi Kenya kimya kimya bila kulitaarifu Bunge wala Serikali. Waliwasiliana na rubani wa ndege ndogo iliyokuwa imeletwa na NHIF ili imsafirishe kwenda Nairobi na gharama za safari hiyo zingelipwa na Chadema wenyewe.
Hata hivyo, rubani huyo aliwaambia ndege yake haiwezi kwenda Kenya wakati huo kwa sababu haina chombo cha kuongozea ndege wakati wa kutua usiku.
Baada ya hapo, Chadema waliwasiliana na mmoja wa makamishna wa Bunge, Salim Turky ili awadhamini wakodishe ndege ndogo imsafirishe kisha watalipa jambo ambalo lilifanyika na Lissu alisafirishwa majira ya saa sita usiku kwenda Nairobi akiwa ameambatana na viongozi wa Chadema pamoja na mkewe.
Mahojiano ya pande zote zilizofikiwa yalionyesha kwamba Bunge na Serikali vilikuwa tayari kutimiza wajibu wa kumtibu Lissu lakini Chadema na familia yake walikataa.
Hili lilithibitishwa pia na taarifa ya uongozi wa Chadema na familia ya Lissu walioweka wazi kuwa ni nia ya Serikali kumuua huku wakijiapiza kutokuwa tayari kuona akipelekwa Muhimbili au Moi.
Nyaraka zote za kumbukumbu ya tukio hilo na watu wote waliohojiwa havionyeshi msimamo huu kubatilishwa na hilo linajenga taswira kuwa malalamiko kwamba Lissu alitelekezwa hayana msingi.
Katika uchunguzi wa nani anapaswa kubeba gharama za matibabu ya Lissu kwa kurejea baadhi ya matukio ya wabunge waliopata kutibiwa nje ambao mwenendo wa matibabu yao umekuwa ukitolewa kama mfano wa kwanini Serikali na Bunge visitende hivyo hivyo kwa Lissu, imebainika kuwa;.
Kwa mujibu wa taratibu, rufaa ya mbunge kwenda kutibiwa nje ya nchi inatolewa baada ya jopo la Madaktari wa Muhimbili au Moi kutoa mapendekezo kwa Wizara ya Afya kuwa mgonjwa husika anahitaji rufaa ya kwenda nje ya nchi.
Na kwamba kiongozi wa ngazi ya mbunge, rufaa yake kwenda kutibiwa nje ya nchi ni lazima mamlaka ya rais itoe ridhaa kama ilivyo kwa majaji na mawaziri.
Vyanzo mbalimbali kutoka serikalini vilieleza kuwa utaratibu wa mamlaka ya Rais kutoa ridhaa ya safari za nje kwa viongozi haukuwekwa na Rais Dk. John Magufuli bali umekuwapo tangu wakati wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.
Inaelezwa kwamba Mwalimu Nyerere aliweka utaratibu huo wakati nchi ikiwa kwenye matatizo ya fedha za kigeni mwaka 1978, lengo lilikuwa kusimamia safari za viongozi nje ya nchi.
Hivyo kilichofanywa na Serikali ya Awali ya Tano ni kukumbushia tu takwa hilo ambalo lipo tangu awamu ya kwanza na kama kulikuwa na kulegalega kwa usimamizi wa kanuni na taratibu hapo katikati hilo ni jambo jingine.
Marehemu Samuel Sitta |
Aidha, rekodi zaidi za kibunge zilionyesha kuwa aliyekuwa Spika wa Bunge, marehemu Samuel Sitta, yeye baada ya ubunge wake kukoma, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alitoa amri ya rais kuwa maspika wastaafu wote wapewe matibabu kama ya wabunge.
Kwa sababu hiyo, maspika wastaafu wana kadi za NHIF lakini nao ili wakatibiwe nje ya nchi huwa wanafuata taratibu zote za rufaa.
Imeelezwa kuwa marehemu Sitta alikwenda Uingereza kwa mambo yake binafsi na kuangalia afya yake, akiwa huko aliugua na alipozidiwa huku uwezo wa kifedha ukawa mdogo aliwasiliana na uongozi wa Bunge, ambao ulimkasimu Balozi wa Tanzania nchini Uingereza jukumu la kutoa taarifa ya hali yake na kuiwasilisha Wizara ya Afya kwa taratatibu nyingine za rufaa, na baadae akapewa rufaa husika, na ndipo Bunge lilipochukua jukumu lake.
Marehemu Philemon Ndasamburo |
Kumbukumbu hizo zinaonyesha pia kuwa marehemu Philemon Ndesamburo, naye alipougua ghafla akiwa nchini Uingereza alikokwenda kwa shughuli zake binafsi, kama mbunge alifuata utaratibu kama ilivyokuwa kwa marehemu Sitta.
Pia dada yake Lissu, marehemu Christina Mugwai alipougua na kutakiwa kwenda nje kwa matibabu zaidi kwa ushauri wa Hospitali ya Aghakhan, ilibidi utaratibu ufuatwe ambapo alihamishiwa Muhimbili na baada ya jopo la madakari kupendekeza ndio wizara ilitoa rufaa yake ya kwenda india.
Marehemu Dk. Eli Macha |
Mwingine katika orodha hiyo ni Dk Eli Macha, aliyekuwa Mbunge wa viti maalumu Chadema, yeye alipougua alianza kujitibia binafsi katika Hospitali ya Siliani Arusha, kisha akaenda Nairobi na baadaye Uingereza.
Alipozidiwa na hali ya kifedha ikawa haimruhusu kuendelea kujigharamia mwenyewe, akiwa kitandani, aliomba uongozi wa Bunge umsaidie umgharimie. Taratibu hizo hizo zilifuatwa, lakini haikuwezekana kwa kuwa alifariki mapema kabla ya kupelekwa India.
Kamishna mmoja wa Bunge alieleza kuwa; “Lakini kwa namna ya kipekee wabunge wanapopewa rufaa kwenda India na kuamua kwenda kwingineko kwa gharama zao, hilo haliwezi kuwa kosa kwao sababu ni matakwa yao binafsi na haijawahi tokea mbunge wa aina hiyo arudi tena kulalamika huku akiwa amekataa haki yake ya msingi kama alivyofanya Lissu.
“Mbona wapo wabunge wengi tu ambao walipewa rufaa ya kwenda nje lakini walikataa na kwenda kwingineko na haijawahi kuwa jambo la kuilalamikia Serikali na Bunge.
“Sambamba na hilo matibabu ya mbunge huwa hayana chama, lakini hili la Lissu mbona Chadema inakuwa ndio msemaji wake. Wabunge wa vyama vyote wamekuwa wakipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi na familia zao na haijawahi tokea chama fulani ndio kikawa msemaji, nadhani hapo kuna shida.
“Suala la Lissu lisifanywe kuwa la kisiasa na nadhani hapo ndipo kwenye tatizo, wabunge wa kila kambi ndani ya Bunge wanapata matibabu kila mmoja kwa binafsi yake na haijawahi semekana kuwa wanakosa matibabu sababu ya itikadi zao. Hapa tunampongeza sana Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kusimamia haki ya msingi ya kila mbunge na familia yake.
“Familia yake iwe ndio msemaji, tena ile ya karibu inayotambuliwa na Bunge na hasa mwenza wake. Na pengine kama Chadema na familia walifanya kosa kutoa lugha ya kejeli na majigambo na kukataa haki ya msingi iliyowekwa kisheria, wanaona shida gani kwa utaratibu ule ule walioutumia kukataa haki ya kumtibu ndani na nje, kurejea tena na kusema tumekosea tunaomba radhi?”
Mwenendo mzima wa uchunguzi ulionyesha kuwa Chadema haikuwa na dhamira ya kweli ya kutaka kumtibu Lissu ilipoonyesha nia ya kumchukua akiwa dhaifu, amepoteza damu nyingi na hajitambui.
Tafasiri ya kitendo hicho ni kuwa Chadema walitaka kuchelewesha matibabu yake kwa makusudi ili baadaye kipate sababu ya kuilamu Serikali na Bunge.
Kama siyo jitihada za Serikali na Bunge, leo hii historia ya Lissu ingekuwa inasomeka kuwa aliyewahi kuwa mbunge wa Singida Mjini.
Lakini pia Lissu mwenye alipata kukiri mchango na weredi wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa Dodoma.
Kwa wafuatiliaji wa mambo wanapaswa kujiuliza kuwa ni kwanini Chadema walitaka kumchukua Lissu huku wakijua kuwa hawana hata senti kwa ajili ya matibabu yake.
Kwa sababu hata walipopewa akiwa tayari amekwishafanyiwa matibabu ya awali hawakuwa na fedha ya kulipia ndege na walikuwa hawakopesheki. Iliwalazimu wasaidiwe kudhaminiwa ndege ambayo malipo yake ilichukua zaidi ya mwezi mzima baada ya kupitisha bakuli wachangiwe.
Na walilipa baada ya mdhamini wao kutishia kuwashtaki. Lakini pia Chadema walikataa kutoa namba ya akaunti ili wabunge wamchangie Lissu kama ilivyokuwa imeombwa na Spika.
Serikali na Bunge kwa kutambua mchango wake, licha ya Chadema kung’ang’ania kumchukua, ililipia gharama za daktari aliyemsindikiza hadi Nairobi Kenya.
Hitimisho la uchunguzi linaonyesha kuwa Chadema walitupa jongoo na mti wake kwa sababu walimzuia hata Spika kwenda kumjulia hali kwani kila alipoomba kwenda kumuona alipingwa chenga wakati watu wengine walipageuza Nairobi kuwa sebule na kituo cha kumshambulia Rais Magufuli na Bunge.