NA CHARLES MULLINDA
HISTORIA, licha ya kuwa mwalimu mzuri ina tabia ya kujirudia. Matukio mengi, mazuri na mabaya yaliyopata kutokea na yanayotokea sasa yamo katika vitabu vya historia.
Kwa tabia hiyo hiyo ya historia, mwenendo wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 28, 2020 kwa ujumla; na ule wa wagombea binafsi hususan wale wa kiti cha urais, maneno na matendo yao, bila kujali kama ni mazuri au mabaya yamo katika vitabu vya historia.
Na historia hiyo hiyo ina tabia moja mbaya ya kuadhibu wale wote wasioizingatia. Kwa tabia yake hiyo, pengine kwa kutambua ghadhabu zake na wepesi wake wa kuadhibu bila huruma wale wote wasiopenda kijifunza kutoka kwayo, imetoa mwanya kwa matendo yake makuu na yenye kuogofya kutunzwa vitabuni na pia kuwa simulizi.
Kwa Watanzania ambao wamo katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa kuchagua rais, wabunge na madiwani, historia kwa tabia yake ilivyo, kwanza imewafunulia ‘chapta’ inayoelezea kwa kina vita vya mawakala wa mabeberu nchini Libya na imewapa sauti thabiti wasimulizi wa tabia za mabeberu na uchu wao dhidi ya rasilimali ambazo mwenyezi Mungu ameyajalia mataifa ya Afrika na hasa Tanzania ili kupitia historia hiyo, Watanzania wasifanye kosa kama walilofanya Walibya.
Si nia yangu MCHOKONOZI kurejea historia hizo kwa kina lakini hofu yangu dhidi ya ghadhabu ya historia imenisukuma kuwakumbusha Watanzania kuwa kinachoendelea sasa hapa nchini kimo katika vitabu vya historia na tusipoizingatia historia kama itakavyo, haina shaka itatutendea kwa mujibu wa taratibu zake.
Historia inatufundisha kuwa utajiri wa nishati iliyonayo Libya na aina ya kiongozi aliyekuwa akiliongoza taifa hilo kuliifanya imezewe mate sana na mabeberu.
Mabeberu hawakuitamani Libya kwa mema bali waliitamani kwa mabaya, walitamani utajiri wake wa nishati uwe wao na walitamani kiongozi wa taifa hilo, Hayati Muammar Ghadafi awe mzungu lakini kwa sababu hakuwa wao walitamani asiwepo kabisa duniani. Walitamani afe. Waliweka nia ya kumuua. Na walimuua kwa kutumia mikono ya Walibya wenyewe. Hii ni historia.
Wazungu mabeberu walitamani mafuta ya Libya yawe ya kwao, wayauze duniani kote kwa kadri watakavyo ili wawe na pesa za kutosha mifukoni mwao za kunywea kikombe cha kahawa chapa ya Africafe na kutafuna korosho tamu za Mtwara na Lindi kwa kadri ya tamaa zao.
Walitamani watoto na wajukuu zao wakipevuka na kuoana, wapewe nyumba na pesa lukuki za kuanzia maisha tofauti na kwao ambako liwe jua au mvua utu wa mtu hauna thamani bali mtu huthaminiwa kwa mali. Hivyo wako tayari kufanya lolote ili wapate mali isiyokuwa yao.
Mabeberu weupe lakini waovu walitamani Ghadafi awe Rais wao ili ayaongoze mataifa yao kwa mafanikio na kuwapa raha raia wa kizungu kama alivyokuwa akifanya kwa Waafrika wa Libya lakini hilo lilikuwa haliwezekani kwa sababa Ghadafi mwenyewe alikuwa Mwafrika anayejitambua. Alitambua kuwa Mungu hakumuumba kimakosa kuwa mlibya. Alitambua kuwa yeye aliumbwa kwa ajili ya Walibya na Afrika.
Kwa sababu ya uovu wao, watu hao mabeberu weupe waliamini Walibya hawakustahili kuwa na kiongozi bora kama Ghadafi na kwa sababu alikuwa jiwe kweli kweli kwao waliazimia asiwepo duniani. Haya ni kwa mujibu wa historia.
Historia hiyo hiyo inaonyesha kuwa zilipoanza kuzuka vurugu katika mataifa ya kiarabu, mabeberu walijipenyeza kwa nguvu Libya, wakawatumia vibaraka wao na nguvu zao za kijeshi kuuangusha utawala wa Hayati Ghadafi.
Wazungu mabeberu kwa kuwatumia vibaraka wao walipenyeza sumu yao ya uchonganishi, baadhi ya Walibya, kwa ujinga wao wakashawishika na ghilba walizopenyezewa, wakayakataa maisha bora na kuyakaribisha maisha ya kulala mitaani, maisha ya kuwa wakimbizi, maisha ya kukosa huduma za afya, elimu bure, maji, umeme na kila neema waliyokuwa nayo.
Walibya kwa kushawishiwa na vibaraka wa mabeberu wakaikumbatia vita, wakamuua kwanza kiongozi wao Ghadafi aliyewatoa kwenye nchi iliyokuwa jangwa na kuwapeleka kwenye Libya iliyokuwa bora kuliko mataifa ya mabeberu na baada ya hapo wakaanza kuuana wenyewe kwa wenyewe.
Leo, Walibya wanapoendelea kuuana, vibaraka wa mabeberu waliowamwangia upupu vichwani mwao kuvuruga akili zao kiasi cha kuzitoa kwenye mawazo ya kijitegemea na kuwa tegemezi, wakimbizi na watumwa. Wao na familia zao wanaishi maisha ya anasa ughaibuni.
Na kwa vibaraka wa mabeberu walioko Libya, kama wapo. Watakuwa wapo kwa ajili ya kutawala kwa niaba ya mabwana zao, mabeberu. Wake na watoto wao hawapo Libya, wanaishi kwa mabeberu. Ni watawala wa dhambi.
Â
Katikati ya mateso hayo ya Walibya, mabeberu wa kizungu wananyonya utajili wa Libya watakavyo. Wanaibomoabomoa Libya kwa silaha nzito nzito kwa kuwatumia Walibya wenyewe.
Walibya na ndugu zao wa Bara la Afrika wanauana katika ardhi ya Libya na viungo vyao; maini, figo pengine hata makanyagio yao vikinyofolewa kwenye miili yao na kuuzwa kwa mafungu kama ziuzwavyo pilipili hoho sokoni. Hii ndiyo ghadhabu ya historia.
‘Chapta’ katika kitabu cha historia hii ambayo wino wake haujakauka, sasa ipo wazi kwa kila Mtanzania. Ni ama tuisome na kuizingatia ili historia isomeke kuwa Taifa la Tanzania ndilo taifa pekee Barani Afrika lililoepuka ghilba za mabeberu likasonga mbele kuelekea nchi ya maziwa na asali au tuisome na kuipuuza kisha ivimbe kwa hasira na kutuadhibu kwa namna ile ile inavyowaadhibu Walibya.
‘Chapta’ hii ya historia ya hovyo ya Walibya iliyofunuliwa sasa ili kila Mtanzania aisome na kuamua mwenyewe kuishi kama mtumwa katika nchi yake au kubaki na heshima ya utu wake, bila kuwa ombaomba, maandishi yake yanaumba kivuli cha kiumbe anayefanana na Tundu Lissu, aliyetoka kwa wazungu mabeberu akiwa amevaa pete ya uraia wao, ambaye sasa yupo Tanzania akiwa amefumbata fuko la dhambi tayari kwa kuiangamiza Tanzania na Watanzania.
Kwa wachokonozi, Lissu kama walivyo binadamu wengine, kwa muonekano wa jinsi alivyofinyangwa na muumba wetu, hana muonekano mbaya ndiyo maana kote anako pita kuwaomba Watanzania wamchague kuwa kiongozi wao mkuu, wanajitokeza kumsikiliza.
Kote anakopita sasa baada ya kutokuwepo nchini kwa muda mrefu nyumbani, wapo wanaokwenda kushangaa muonekane wake, wapo wanaokwenda kuangalia miondoko yake na wapo wanaokwenda kumshangaa anachokisema dhidi ya Taifa la Tanzania na Watanzania wenzake. Haina shaka wapo wanaovutiwa naye na kuamua kuipa kisogo historia.
Nyuma ya historia ya kuangamia kwa Libya kinaonekana kivuli cha Lissu. Maneno na matendo yaliyo ndani ya kivuli hicho vinachora umbo la rais mwovu akiwa amesimama nyuma ya tamaa ya urais wa damu.
Ni kivuli kibaya kukitazama kwa sababu kinaogofya. Kivuli kinachotoa taswira ya rais atakayeligawa Taifa la Tanzania katika makabila – ukanda, kivuli chenye umbo jeusi linalotishia kuzigawa rasilimali za Watanzania kwa mabeberu na katika kivuli hicho hicho, kwa mbali linaonekana umbo la mwanaume shoga akiwa ameachama mdomo wake na kutoa ulimi nje, ishara kwamba ana kiu kali hivyo anasubiri tone la maji baridi kutoka Ziwa Victoria lidondoke kinywani mwake na kumtia nguvu ya kuchomoka kwa kasi nyuma ya kivuli alichopo kuingia mitaani.
Kivuli hiki kilichomtanguliza Lissu katika harakati za kuusaka ukuu wa dola kinamuonyesha katika sura ya mtu mwenye dharau. Sura ya mgombea urais anayewadharau wapiga kura na kuheshimu mabeberu ambao sifa yao kuu ni kuvuruga amani ya wenyeji, kuwachonganisha na kuwapa silaha ili wauane wenyewe kwa wenyewe wakati wao wakipora mali zao.
Lissu anaonekana mbele ya kivuli cha urais kilichofifia kinachotoa maneno ya dharau na kejeli kwa kiongozi mkuu wa Tanzania anayeheshimika zaidi duniani kwa sasa baada ya kuliwezesha taifa lake kumuangukia Mungu naye akaliinua kwa mkono wake wa kiume dhidi ya gonjwa baya la Corona linalowateketeza walimwengu bila huruma.
Kivuli kilicho nyuma ya Lissu, kinamuonyesha akijaribu kunyanyua mguu apige hatua kuwaelekea Watanzania akiwa amefumbata furushi la dhambi ya kuwahamasisha ndugu zake Watanzania waingie barabarani kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu ili wamwage damu kabla ya kuchukua mkondo ule ule machafuko ya Libya.
Dunia bado haiamini kuwa mabeberu na kibaraka wao watafanikiwa kuwatumbukiza Watanzania katika vurugu zitakazo liangamiza taifa lao na historia ipo inasubiri kusikia kanusho la kuwakana mabeberu na kibaraka wao kutoka kwenye midomo ya Watanzania wenyewe ifikapo oktoba 28, 2020.