Monday, June 23, 2025
spot_img

DC MURO 'AJIPIGAPIGA' KIFUA UJENZI WA MADARASA, MAFANIKIO YA ELIMU ARUMERU

 

NA MWANDISHI WETU, ARUMERU

MKUU wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha (DC) Jerry Murro amesimama mbele ya wananchi wa Wilaya ya Arumeru na kujipigapiga kifua akijivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa na wilaya yake katika sekta ya elimu.

Mbele ya wazazi wa wanafunzi, wadau wa elimu na wafadhili, DC Murro amesema Wilaya ya Arumeru kwa kipindi cha miaka miwili imeendesha kwa mafanikio makubwa kampeni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari na msingi na kwamba Mkoa wa Arusha unajivunia kushika nafasi ya pili kwa ufaulu wa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule za sekondari na msingi wilayani Arumeru, DC Murro amesema yeye mwenyewe pamoja na wananchi wa Arumeru hawana rekodi ya kushindwa kutekeleza maagizo ya viongozi wakuu wa serikali na historia ya wana Arumeru inasomeka vizuri katika utoaji elimu bora na ujenzi wa miundombinu yake.

“Mkoa wetu wa Arusha umekuwa wa pili kitaifa kwa ufaulu wa wanafunzi na sisi kama Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arumeru tumekuwa na ajenda endelevu ya kuhakikisha tunawapokea wanafunzi wote ambao juzi wametangazwa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo.

” Ndugu zangu wazazi nipo hapa kwanza kiwashukuru kwa kuitikia kampeni yetu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule za msingi na sekondari… Sisi kama Wilaya ya Arumeru tulifanya kazi hiyo kwa miaka miwili mfululizo hivyo hatukuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa.

” Tumeanza kampeni ya awamu nyingine ya pili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari. Sisi Wilaya ya Arumeru mpango wa kujenga vyumba vingine vya madarasa uwe umekamilika kabla ya Februari 22, 2021,” alisema DC Murro.

Mkuu huyo wa wilaya anaendelea na kampeni ya kuhamasisha ujenzi wa madarasa kwa wilaya za Meru na Arumeru ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa linalowataka viongozi wenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu kuhahakisha wanafunzi wote wanaoanza elimu ya msingi na waliochaghuliwa kujiunga kidato cha kwanza hawakosi madarasa na madawati.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya