![]() |
Ujenzi wa soko jipya la Tandale ulipofikia umefikia Agosti mwaka jana |
NA MWANDISHI WETU
WAKATI serikali ya awamu ya tano ikiwa imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu, shule, hospitali na masoko, jitihada hizo zimeanza kuingia doa baada ya kusimama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale.
Katikati ya hilo, msimamo wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli za maendeleo bila ukiritimba, zinazofanywa na serikali ili kutoa fursa kwa wananchi kujua miradi inayotekelezwa kwa kodi zao, nao unaonekana kuingia doa baada ya mkandarasi anajenga soko la Tandale, Namis Corporate Ltd kuweka zuio la upatikanaji wa taarifa hizo.
Haya yamebainika baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika eneo la ujenzi wa soko jipya la Tandale mapema wiki iliyopita kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo baada ya kudokezwa na baadhi ya wafanyakazi kuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Tanzania PANORAMA Blog baada ya kufika katika eneo la mradi, lilishuhudia mafundi wakiwa wamekaa kivulini huku ujenzi ukiwa umesimama na baada ya kuwahoji baadhi yao walisema wanasubiri kulipwa fedha zao waondoke kwa sababu mahali hapo hakuna kazi tena.
“Bora umekuja na sijui umeingiaje huku maana hamruhusiwi nyie kuingia humu na wakikuona watakugawana. Hapa hakuna kazi kama unavyoona ujenzi umesimama hakuna fedha. Tunasikia bosi hajalipwa huko serikalini ndiyo bado anafuatilia malipo lakini sisi tumeambiwa tukiulizwa tuseme tuna tatizo la simenti ambalo ni tatizo la kitaifa kwa sasa.
” Kama unaweza twende tukupeleke kwa msimamizi wetu ukamuhoji ila uwe unajiamini labda watatulipa. Sisi tunasubiri akipata pesa kutoka serikalini akitulipa ndiyo basi tunatafuta kazi sehemu nyingine maana hapa, wiki hii mnafanya kazi wiki ijayo hakuna kazi sasa tunajiuliza hiyo serikali inatoa hela kwa wiki?” alisema mmoja wa mafundi hao.
Msimamizi wa mradi alipofikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuulizwa, kwanza alielekeza afuatwe ofisini ambako alichukua simu na kuwasiliana na Makao Makuu ya kampuni yake kisha alisema;
“Unasema kuna wenzako kwenye gari wanakusubiri …. Umesema hujapiga picha…. Hili ni eneo la ‘site,’ mtu yoyote haruhusiwi kuingia humu bila kibali cha makao Makuu, awe Mkuu wa Mkoa, awe Waziri anapotaka kuja hapa ni lazima awe na kibali kwa sababu anaweza kuangukiwa na kitu kizito kama nondo au ubao ukaumia.
” Sasa nimeongea na Makao Makuu nadhani umeona naongea na simu, kama una maswali nenda huko watakujibu na kama unataka kutembelea hapa uje na kibali cha maandishi kutoka makao makuu.
“Tena tumekuheshimu sana kwa sababu umeingia eneo ambalo haliruhusiwi ila kwa vile una wenzako nje njoo nikupitishe njia salama usije ukajikwaa halafu mkaanza kutunga uongo, ” alisema.
Tanzania PANORAMA Blog lilifika Makao Makuu ya Kampuni ya Namis Corporate Ltd yaliyopo Mbezi Africana kwa ajili ya kupata maelezo ya kasimama kwa ujenzi wa soko la Tandale na kuelezwa kuwa mkataba wa ujenzi una kipengele kinachozuia kutoa taarifa yoyote ya mwenendo wa ujenzi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Akizungumza kuhusu katazo hilo alilodai lipo kwenye mkataba huo, Meneja Mradi aliyejitambulisha kwa jina la James Msumali alisema changamoto zinazowakabili katika ujenzi huo anaweza kuzizungumzia iwapo atapata kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.
“Mimi ndiyo meneja mradi na ndiye ninayeweza kuzungumza, bosi unayetaka kuonana naye hayupo. Utaratibu upo hivi, mkataba wetu una kipengele kinachoelekeza kuwa taarifa yoyote ya mradi haiwezi kutolewa mpaka kwa kibali cha Mkurugenzi.
“Tena kibali cha maandishi au anipigie simu yeye mwenyewe aseme nitoe taarifa kwako. Kwa hiyo nenda Manispaa kamtafute Mkurugenzi muombe kibali au mwambie anipigie simu ndiyo uje nikueleze hicho unachotafuta,” alisema Msumali.
![]() |
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli |
Alipofikiwa na kuelezwa hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alihoji ni kwanini Tanzania PANORAMA Blog linafuatilia mradi wa ujenzi wa soko la Tandale wenye kelele nyingi badala ya kuandika maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ghorofa la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni au ujenzi wa bwawa na kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
“Kwanini Ujenzi wa Soko la Tandale ambalo lina kelele nyingi saaana. Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa ghorofa hiyo hapo sasa umefikia ghorofa ya nne, kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere? Kwanini huandiki kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa, kwanini huandiki kuhusu stendi Mpya ya mabasi ya Dar es Salaam?
” Lakini nimeitwa mahali sasa siwezi kuwasikiliza kwa sababu nimeitwa na wakubwa. Njooni kesho,” alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa siku iliyofuata alisema kusimama kwa mradi huo kunachangiwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa saruji. Alipoulizwa kuhusu zuio la kuandika habari za soko hilo alisema halitambui isipokuwa mwananchi anapaswa kufuata utaratibu kuingia katika miradi ya aina hiyo.
“Hilo zuio silijui na nitoe barua kwa mwandishi kwenda kuandika habari kutoka lini hiyo. Hao watakuwa na yao lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia kwenye miradi ya aina hiyo kwa kufuata utaratibu maalumu ulioandaliwa na (project manager) Meneja mradi,” alisema Kagurumjuli.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Namis Corporate Ltd, Thomas Uiso alikataa kuzungumza lolote na kueleza aulizwe meneja mradi, Msumali.
Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hilo.