Monday, June 23, 2025
spot_img

JWTZ, TISS KUOMBWA KUMSAKA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY’S

Mkuu wa Majeshi, Venance Mabeyo

 

NA MWANDISHI WETU

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wataombwa kumsaka mwanafunzi aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde, Labna Said Salim ambaye ametoweka tangu Oktoba 4, 2020.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere kwa Tanzania PANORAMA Blog leo, imeeleza kuwa taasisi hizo zitaombwa kusaidia kumsaka mwanafunzi huyo popote alipo baada ya jitihada za Jeshi la Polisi kumsaka kushindwa kuzaa matunda.

Kapere ambaye alikuwa akizungumzia mwenendo wa uchunguzi wa timu ya maafisa wanne wa serikali iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kuchunguza mazingira ya kutoweka kwa mwanafunzi huyo na kumsaka mahali alipo, ameeleza kuwa tume hiyo imekwishamkamata kijana anayedaiwa kuishi na mwanafunzi huyo baada ya kutoroka shuleni na sasa inasubiri wanafunzi wa kidato cha nne wamalize mitihani ya taifa ili iweze kuchukua hatua zaidi.

Timu hiyo inayomsaka mwanafunzi huyo inaundwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Usdalama wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni na Mdhibiti Ubora wa Elimu Kanda.

“Uchunguzi wetu unaendelea lakini hatufanikiwa kumpata huyo mtoto. Tiumekwishamkamata na kumuhoji kijana ambaye inadaiwa kuwa yule mtoto alitorokea kwake, anakiri kwamba ni kweli alikwenda chumbani kwake lakini huwa anakwenda mara kwa mara na marafiki zake na kwamba aliondoka akamuacha hapo chumbani akiwa na marafiki zake.

“Lakini wale marafiki zake saba tuliowakuta nyumbani kwa baba yake mahali ambako anaishi huyo kijana wakiwa wanavuta bangi wameeleza kuwa ni kweli huyo mtoto alipotoroka shule ule usiku alikwenda kwa huyo kijana wakawa wote kabla ya kutoweka kusikojulikana,

“Na wale waliomsindikiza kwenda kwenye hiyo nyumba ambao ni wanafunzi wenzake nao tuimewahoji na wanakiri kuwa mtoto Labna alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na huyo kijana na kwamba siku hiyo walimsindikiza akaenda kwake.

“Sasa unajua wanafunzi wengi wa kidato cha nne wako kwenye mitahani, tunasubiri jumatano wamalize ili tuiwakutanishe pamoja wote tuliowahoji watueleze kwa pamoja ndipo tuchukua hatua zaidi,” alisema Kapere.

Alipoulizwa hatua zitakazochikuliwa na timu hiyo baada ya kukamilisha uchunguzi wake alisema itaandika taarifa itakayoipeleka kwa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi lakini itaomba Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) vialikwe kusaidia kumsaka mwanafunzi huyo kutokana na jeshi la polisi kutopata mafanikio.

“Sisi tutaandika taarifa yetu na tumeishaanza kuandika, tutaeleza upungufu wote tulioubaini kwenye hiyo shule na tutatoa mapendekezo tutapeleka kwa mkuu wa wilaya ambaye ndiye aliyeunda timu hii. Lakini niseme tu moja kwa moja katika mapendekezo yetu tutashauri TISS na JWTZ waalikwe kumsaka huyu mtoto kwasababu nadhani polisi wanahitaji msaada maana mpaka sasa hawajafanikiwa,” alisema Kapere.

Labna


Mwanafunzi Labna alitoweka shuleni Oktoba 4, 2020 na taarifa za awali zilieleza kuwa alitoroka akiwa na wafunzi wanzake kwenda kwenye maeneo ya starehe na kutokomea moja kwa moja.

Zephania Maduhu ambaye ni mjomba wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akimlipia ada ya shule aliieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa ana wasiwasi mtoto wake ameuawa kwani tangu Oktoba 4, 2020 alipopotea akiwa chini ya uangalizi wa shule, taarifa za kupotea kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa mwanafunzi huyo akiulizia kama ameishafika nyumbani jambo ambalo limekuwa liibua hisia zinazotia shaka kuhusu usalama wa mtoto huyo.

“Huyo mtoto ninamlea mimi, ninamlipia ada ya shule mimi, ni mtoto wa dada yangu, anasoma St. Mary’s, Mbezi Makonde. Oktoba 8, mwaka huu, matron wake anaitwa Sarah Murra, alimpigia simu mama yake, yaani dada yangu akimuuliza kama Labna kafika nyumbani.

 “Dada yangu ambaye wakati huo alikuwa mkoani Shinyanga akashangaa akamuuliza amefikaje nyumbani wakati yupo shule au shule zimefungwa ghafla tena? Yule matron akamjibu ametoroka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 hivyo alikuwa anataka kujua kama yupo nyumbani, dada akamwambia yeye yupo mkoani Shinyanga na anajua mtoto wake yupo shule.

 “Aliporudi kutoka safari Shinyanga akakuta mtoto hajapatikana na shule haijatoa taarifa polisi yaani hata wasiwasi hawana. Ikabidi yeye aende kutoa ripoti Kituo cha Polisi cha Stakishari, waliponipa taarifa mimi nikafunga safari mpaka shuleni.

 “Pale shuleni nikamkuta mkuu wa shule anaitwa Reca Ntipoo, akanijibu mtoto alitoroka shule usiku hajarudi na hawajui alipokwenda. Nikauliza kama wamefanya jitihada zozote za kumtafuta na kama wameisha ripoti polisi akasema hilo ni jukumu letu wazazi.

 “Sasa hapo nikakasirika nikamuuliza mtoto tumemkabidhi shule na ada tumelipa kumbe katoroka zaidi ya mwezi hata taarifa polisi hawajatoa, hapo akajibu labda tukamtafute kwenye vijiwe vyao vya usiku wakitoroka huwa wanakwenda huko ambako wanafunzi wenzake wanavijua, akamuita mwanafunzi mmoja kweli akatuelekeza huko wanakokwenda usiku.

 “Nilikuwa na rafiki yangu alinisindikiza tukaenda kumtafuta huko hatukumpata, hatukuwa na jinsi ikatubidi sisi tukatoe taarifa nyingine kituo cha Polisi Goba na polisi tulipowaelezea nao walishangaa  kweli kweli.

 “Sasa RB tunayo ni STK/RB/10714/2020 na mpelelezi wa shauri hilo ni Afande Gwake Mwakapande. Sidhani kama yupo hai sisi tunaamini ameishakufa lakini uongozi wa shule hii ndiyo umetuulia mtoto wetu. Polisi wanajua sasa sijui kama wameishawauliza au bado,” alisema Maduhu.

 Kapere amekwishaieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa Mkuu wa Shule ya St. Mary’s, Ntipoo alikiri kufanya uzembe kutotoa taarifa polisi na kwa wazazi kuhusu kupotea kwa mwanafunzi Labna na kwamba kutoroka kwa wanafunzi usiku na kwenda kwenye maeneo ya starehe ni jambo alilolikuta shuleni hapo hivyo hata baada ya kutoonekana kwa Labna aliamini kuwa alitoroka usiku kwenda kwenye mambo yake lakini angerudi.

 Aidha Kapere amwishaeleza kuwa timu imebaini kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s ni chafu, haina ulinzi wa kutosha na ukuta wake haufai.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya