Friday, December 27, 2024
spot_img

WENGI WANAGHUSHI NYARAKA ZA SERIKALI – TMDA

 

NA MWANDISHI WETU

IMEELEZWA kuwa vitendo vya kughushi nyaraka za serikali vinafanywa na watanzania wengi hapa nchini.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba( TMDA), Akida Khea, alisema siyo jambo jipya wala la kushtusha kwa nyaraka za serikali kughushiwa na kazi ya serikali ni kupambana na uhalifu huo.

Khea alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwenendo wa uchunguzi wa tuhuma kuhusu Kampuni ya Multvet Farm Ltd ya jijini Dar es Salaam kuingiza nchini dawa za mifugo na kuzisambaza kwa matumizi kwa kutumia vibali vyenye shaka vya TMDA.

Msemaji wa TMDA, Gaudensia Simwaza ambaye awali alilieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa taasisi yake inaendelea na uchunguzi wa nyaraka za kampuni hiyo hivyo ipewe muda wa kutosha, jana alipoulizwa alisema mkurugenzi wake mkuu  alitaka kwanza kuzungumza na Tanzania PANORAMA Blog.

Katika mazungumzo yake na Tanzania PANORAMA Blog, Khea aliomba mkutano wa ana kwa ana kwa kuialika ofisini kwake Jumatatu, Oktoba 5, 2020 huku akisisitiza kuwa anahitaji kupata msaada utakaosadia uchunguzi unaofanywa taasisi yake.

Alisema, vitendo vya kughushi nyaraka za serikali siyo vipya kwani vimekuwa vikifanywa na watu wengi hivyo vipo kila mara na kwamba serikali imekuwa ikipambana navyo.

“Njoo ofisini tuzungumze, njoo utusaidie. Huyu mtu siyo wa kwanza. Wapo wengi tu. Hivi vitendo vya watu kughushi nyaraka za serikali vinafanywa na watu kila mara na serikali inapambana navyo kikamalifu,” alisema Khea.

Inadaiwa kuwa Kampuni ya Multvet Farm Ltd inayoagiza dawa za mifugo kutoka nje ya nchi imekuwa ikitumia vibali vyenye shaka vya TMDA huku akilipa kodi zote za serikali.

Kwamba kampuni hiyo imekuwa ikitumia vibali vyenye shaka vya TMDA kwa zaidi ya miaka minne sasa na baadhi ya wataalamu wa afya ya mifugo wameeleza kuwa dawa ambazo hazijathibitishwa na TMDA kutumika katika mifugo zinaweza kuwa na athari mbaya katika ustawi wa mifugo na kuongeza kuwa hilo linaweza kuwa moja ya mipango ovu ya kuangamiza mifugo hapa nchini.

Mmiliki wa Kampuni ya Multvet Farm Ltd, Dk. Henry Ruhinguka alipoulizwa kuhusu kampuni yake kuelekezewa madai hayo kwanza alikanusha kuwa yeye siyo msemaji wa kampuni hiyo na pia alikanusha kufahamu lolote kuhusu madai hayo.

Hata hivyo uchunguzi wa Tanzania PANORAMA Blog umebaini kuwa Dk. Henry ndiye mmiliki wa kampuni hiyo na amekuwa mzungumzaji wake mkuu.

Katika mahojiano hayo Dk. Henry baada ya kuelezwa kuwa baadhi ya nyaraka zenye shaka za kampuni yake zilizotumika kuingiza dawa hizo Tanzania PANORAMA Blog limeziona alisema, hayo ni mambo ya zamani na hivi sasa kampuni hiyo iliishaachana nayo.

Alisema ni kweli jambo hilo liliwahi kutokea na alilipeleka Dodoma kwa wakubwa  lakini hakufafanua alilipeleka kwa wakubwa gani na maamuzi yaliyochukuliwa.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya