Friday, December 27, 2024
spot_img

WATANZANIA WAASWA KUCHAGUA KIONGOZI ATAKAYEKUZA UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA

 


NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewaasa watanzania kuchagua kiongozi ambaye atakuza uhusiano wa kidiplomasia na nchi jirani.

“Tanzania inazungukwa na nchi tisa ambazo baadhi yake ziko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyingine hazimo. Tunahitaji kiongozi ambaye ataweza kuhakikisha nchi hii inakuwa na uhusiano mwema na nchi jirani na nchi nyingine duniani kote lakini pia anayeweza kuilinda heshima ya nchi yetu,” amesema.

Majaliwa ameyasema hayo Alhamisi, Oktoba Mosi, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kata za Nyakahura na Nyakanazi, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera akiwa njiani kuelekea Wilaya za Bukombe na Mbogwe mkoani Geita.

Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake mkoani Kagera ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, Injinia Ezra Chiwelesa na wagombea udiwani wa CCM wa kata hizo, Apolinary Mgalula na Amos Madegwa.

Akielezea suala la vitambulisho vya uraia, amesema kote alikopita mkoani humo wananchi wanauliza kuhusu kuchelewa kutolewa kwa vitambulisho hivyo.

“Ucheleweshaji huu hauko hapa mkoani Kagera tu bali hata kwenye mikoa ya pembezoni ya Kigoma, Songwe, Katavi, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani, Arusha na Mara.

“Hii ni kwa sababu tunataka tujiridhishe na uraia wa waombaji kwani hili suala ni kwa usalama wa nchi yetu. Wale walioko jirani umbali wa km. 10 wanaruhusiwa kuja kutembea au kufanya biashara na kurudi kwao. Hawaruhusiwi kupata vitambulisho, hivi ni kwa Watanzania tu,” amesema Majaliwa.

Kiongozi huyo amewahakikishia wakazi hao kwamba kila Mtanzania mwenye sifa atapata kitambulisho cha Taifa kwa kuwa ndiyo mkakati wa Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Magufuli.

Majaliwa amesema Idara ya Uhamiaji inatakiwa kuwa makini kusimamia mchakato huo kwa sababu wapo baadhi ya raia wa nchi jirani wanatamani kupata kitambulisho cha Taifa kutokana na amani iliyopo nchini.

“Uhamiaji iwe makini haitapendeza kuona Mtanzania anakosa kitambulisho cha Taifa halafu mgeni kutoka nchi jirani anapata,” amesema.

Hata hivyo, amewataka wakazi hao wasikubali kutoa rushwa kwa sababu hiyo ni haki yao na kwamba endapo itatokea wameombwa rushwa watoe taarifa.

“Mtu wa uhamiaji akidai rushwa ili akupatie kitambulisho toa taarifa mara moja ili tumshughulikie,” amesisitiza.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya