NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI mbili za ujenzi za China, China Road and Breadge Corporation (CRBC) na SCG Overseas Tanzania Company Limited zinadaiwa kufanya biashara inayoziingia mabiilioni ya shilingi ambayo hayatozwi kodi.
Sambamba na biashara hiyo unaofubaza fuko la fedha zikusanywazwo na Mamlaka ya Mapato (TRA) kama kodi, Kampuni ya CRBC imekusanya na kutia kibindoni mamilioni ya fedha ilizokuwa ikiwakata wafanyakazi wake kama malipo ya pensheni.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedai kuwa SCG Overseas Tanzania Company Limited, ambayo iliingia nchini kwa ajili ya kujishughulisha na ujenzi wa barabara na madaraja ilipewa msamaha wa kodi wa vifaa vyake vya ujenzi.
Inadaiwa kampuni hiyo ambayo sasa imemaliza shughuli zake hapa nchini, imekuwa ikikodisha vifaa ilivyokuwa ikitumia kwa shughuli zake za ujenzi vikiwa na msamaha wa kodi kwa Kampuni ya CRBC ambayo huilipa mamilioni ya fedha.
Taarifa zaidi zilizokusanywa na Tanzania PANORAMA Blog zimeonyesha kuwa biashara kati ya kampuni hizo mbili, licha ya kuwa yenye thamani kubwa, risiti zinazotolewa kuthibitisha kufanyika kwa malipo hazitambuliki kwenye mfumo rasmi wa kikodi wa hapa nchini.
“Hawa wachina wa hizo kampuni mbili wanafanya biashara ya mabilioni kwa kukodishiana vifaa na mitambo ya ujenzi. Kiukweli wanaoga fedha hapa Dar es Salaam,” alisema mmoja wa watoa taarifa.
Wakati huo huo, CRBC inadaiwa kuweka katika fuko lake ya fedha mamilioni ya shilingi waliyokuwa wakikatwa wafanyakazi wake kama malipo ya pensheni.
Katika mahojiano kati ya baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na Tanzania PANORAMA Blog huku wakiwa na nyaraka zao za malipo ya mshahara mkononi (salary slip) wamedai kwa zaidi ya mwaka mmoja walikuwa wakikatwa pesa katika mishahara yao kwa ajili ya pensheni lakini baada ya mikataba yao ya kazi kuisha wamebaini kuwa fedha hizo zilikuwa haziwasilishwi kwenye mifuko ya jamii.
Alipoulizwa Meneja Rasilimali Watu wa CRBC, Alice Charles kuhusu madai hayo alikubali kuzungumzia suala ya malipo ya pensheni huku dai la kuwepo biashara baina ya CRBC na SCG alisema hilo kwake ni zito na anayeweza kulisemea ni bosi wake aliyemtaja kwa jina moja la Zhang.
Alice alisema madai ya wafanyakazi kukatwa sehemu ya mishahara yao kwa ajili ya pensheni ni ya kweli.
Aidha, Alice alieza zaidi kuwa fedha hizo badala ya kuwasilishwa kwenye mifuko ya kijamii zilikuwa zikiingizwa kwenye fuko kuu la kampuni hiyo kwa sababu wafanyakazi hao walikuwa siyo wanachama wa mifuko hiyo.
Alice aliahidi kuwasiliana na bosi wake Zhang ili azungumzie madai ya kuwepo biashara baina ya CRBC na SCG na kwamba taarifa rasmi angeitoa kwa Tanzania PANORAMA Blog lakini kwa zaidi ya wiki mbili sasa ameshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.
Meneja wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alipotafutwa kuzungumzia iwapo taratibu za mamlaka hiyo zinaruhusu vifaa vilivyoingizwa nchini vikiwa na msamaha wa kodi kutumiwa kibiashara, simu yake iliita zaidi ya mara tano bila kupokelewa na hata alipotumiwa maswali kwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani, aliyasoma lakini hakujibu chochote.
Jitihada za kumpata balozi wa China kuzungumzia suala hilo hazikiweza kuzaa matunda baada ya simu kuwa inaita bila kupokelewa