NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Multvet Farm Ltd ya jijini Dar es Salaam inadaiwa kuingiza nchini dawa za mifugo na kuzisambaza kwa matumizi kwa kutumia vibali vyenye shaka vya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedai kuwa sehemu kubwa ya vifaa hivyo inaagizwa kutoka Afrika Kusini na muagiza amekuwa akilipa kodi zote za serikali lakini katika hatua ya kushangaza amekuwa akitumia vibali vyenye shaka vya TMDA.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Kampuni ya Multvet vimeeleza kuwa mwenendo huo wa kutumia vibali vyenye shaka ni wa muda mrefu tangu TMDA ilipokuwa ikijulikana kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Tanzania PANORAMA Blog limeiona orodha ya baadhi ya vibali na dawa za mifugo zinazoingiwa nchini kwa kutumia vibali vyenye kutiliwa shaka vinaonyesha kutolewa na TFDA
Moja ya kibali kinachodaiwa kuwa na shaka kilicchoonwa na Tanzania PANORAMA Blog kinaonyesha kilitolewa Juni 17, 2018 kikiwa na namba TFDA – WEB0518/D/IPER/1032 na kilitumika kuingiza dawa za mifugo kutoka nchini Afrika Kusini.
Alipoulizwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo (jina tunalihifadhi) kwa sababu si msemaji rasmi, kwanza alikanusha kufahamu lolote kuhusu madai hayo lakini alipoelezwa kuwa Tanzania PANORAMA Blog limeona baadhi ya vibali vinavyodaiwa kutiliwa shaka na dawa ambazo zimekuwa zikiingizwa nchini kwa kutumia vibali vya aina hiyo alisema hayo ni mambo ya zamani na hivi sasa kampuni hiyo ilishaachana nayo.
Alisema hivi sasa yeye na washirika wake wanamiliki kiwanda cha kutengeneza dawa za mifugo lakini alipobanwa kuwa vibali vinavyodaiwa kutumiwa kuingia dawa hizo ni vya kampuni yake alisema ni kweli jambo hilo liliwahi kutokea na alilipeleka Dodoma kwa wakubwa bila kufafanua alilipeleka kwa wakubwa gani na likichukukiwa maamuzi gani.
Msemaji wa TMDA, Gaudencia Simwaza akizungumzia suala hilo baada ya Tanzania PANORAMA Blog kumfikishia alisema taasisi yake imelipokea na inaendelea na uchunguzi kabla ya kutoa tamko