Saturday, December 28, 2024
spot_img

UJENZI UBUNGO INTERCHANGE KUKAMILIKA DISEMBA 30, 2020


UJENZI wa barabara za juu eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, maarufu kama Ubungo Interchange unaozikutanisha barabara tatu za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro unatarajiwa kukamilika Disemba 30, mwaka huu.

Ujenzi huo unaotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), sasa umefikia asilimia 81.

Akizungumza katika mahojiano maalumu  meneja wa mradi huo, Mhandisi Barakaeli Mmari amesema ujenzi huo ulioanza Mei, 2017 unaendelea vizuri na hivi sasa barabara zote mbili za juu zimefunguliwa kwa majaribio.

“Kwa mara ya kwanza Mei 30, 2020 tuliifungua barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro kwa majaribio ambapo tuliruhusu magari kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam Nujoma ilifunguliwa kwa majaribio.

“Ni matarajio yetu kuwa ifikapo Disemba 30, 2020 ujenzi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wataendelea kufaidi barabara hiyo,” amesema Mhandisi  Mmari.

Amesema lengo la ujenzi wa barabara za juu ni kuondoa msongamano katika makutano ya barabara hizo eneo la Ubungo uliokuwa ukisababisha watu kuchelewa kufika  kwenye kwenye shughuli zao kwa wakati na kupoteza muda mwingi ambao ungetumika kuwaongeza kipato.

Akizungumza kuhusu matumizi ya barabara hiyo kwa madereva amesema katika eneo hilo kuna barabara ngazi (ghorofa) tatu, ya chini, ya kati na ya juu, ambapo ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka Mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda Mjini.

Amesema itatumiwa pia na magari yote yatakayokuwa yanapinda kushoto kwenye maungio hayo.

Mhandisi Mmari amesema ngazi ya kati  itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara na ngazi ya juu itatumiwa na magari yanayotoka  Mwenge kwenda Buguruni na  Buguruni kwenda Mwenge.

Aidha, Mhandisi Mmari amesema barabara za juu zimejumuisha njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi. 

Kuhusu ajira, Mhandisi Mmari amesema mradi huo umetoa ajira kwa watanzania wengi wakiwemo wananchi wa kawaida mpaka wahandisi ambao wanashughulika na kazi za kihandisi katika kutekeleza ujenzi kwa ufanisi.

“Tumeajiri wafanyakazi kati ya 800 hadi 900 kwa mwezi na kati ya hao Wafanyakazi wa nje ni asilimia 10 tu huku wafanyakazi wazawa wakiwa asilimia 90, kwa hiyo ujenzi huu umeleta faida kwa watanzania wengi hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,” Amesema Mhandisi Mmari.

Kwa upande mwingine, Wananchi wa Ubungo waliozungumzia mradi huo hawakuficha furaha yao kwa kufunguliwa kwa majaribio barabara hizo.

“Tunaishukuru Serikali kwani foleni sasa hakuna, magari yanapita vizuri na sisi tunapita vizuri tu, naamini tunakoelekea tutafanya mambo mazuri zaidi ya haya,”  ameeleza Bakari Juma.

Naye Johnson Mwakalukwa amesema barabara hiyo imesaidia wasafiri kutoka mikoani kwani sasa wakifika Mbezi wanakutana na barabara ya njia nane na wanakuja kumalizia na Ubungo ‘Interchange,’ hivyo kuokoa muda mwingi waliokuwa wakiutumia kwenye foleni.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya