Friday, September 12, 2025
spot_img

RAIS MAGUFULI AUZWA KWA REKODI YAKE

 

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapunduzi (CCM), Kassim Majaliwa jana amemuuza mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Pombe Magufuli kwa rekodi yake ya kupigiwa mfano ya utendaji kazi.

Majaliwa ameutangazia umma wa watanzania kuwa mgombea huyo wa CCM ana rekodi ya kutukuka ya utendaji kazi katika kipindi cha miaka 20 alipokuwa waziri katika wizara mbalimbali.

Akiwahutubia wakazi wa Ushirombo, Okotoba Mosi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe mkoani Geita, amesema Dk. Magufuli ana rekodi nzuri ya utendaji kazi.

“Dk. Magufuli tunamjua. Alikuwa waziri katika nchi hii kwa miaka 20. Alikuwa Waziri wa Ujenzi akajenga barabara ambazo sote leo tunaziona. Alipoenda Wizara ya Ardhi, akapiga marufuku watumishi wa wizara hiyo kujilimbikizia viwanja vinne vinne.

“Nimekuja kuwaomba kura zenu. Ni lazima tumpe kura mtu ambaye tunaijua historia yake ya kwamba aliwahi kuwa kiongozi na ameweka historia,” amesema.

Majaliwa amewataka wananchi wamchague kiongozi ambaye anaweza kuisimamia serikali yake.

“Usipokuwa makini unaweza kumpa mtu nchi halafu akashindwa kuisimamia. Kiongozi anayefaa, mwenye uwezo wa kuratibu rasilimali zetu na kuzisimamia, si mwingine bali ni Dk. Magufuli,” amesema.

Amehimiza watanzania wawachague wagombea wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja. “Ni muhimu tuwe na madiwani ili waunde baraza lao la madiwani, waongee lugha moja na wapeleke hoja zao kwa mbunge wao,” amesema.

Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko na mgombea udiwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga.

“Dk. Magufuli amekuwa rais kwa miaka mitano, aliyoyafanya katika kipindi kifupi tunayaona. Dk. Magufuli huyu, wala rushwa ndiye kiboko yao. Leo niko mbele yako, bila kujali chama chako cha siasa, ninakuomba umpigie kura Dk. Magufuli. Niko mbele yenu, ninawaomba kura za wagombea wa CCM,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema Wilaya ya Mbogwe imetengewa sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya wilaya hiyo.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji Kabanga – Nhomolwa ambao ulipatiwa sh. bilioni 1.2. “Fedha nyingine zilizotolewa ni shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Mbogwe ambao utanufaisha maeneo ya Kasosobe, Bwelwa na Iboya.”

Amesema upanuzi wa mradi wa maji Nyakafuru umepatiwa sh. milioni 633 ambao utanufaisha maeneo ya Lulembela na Nyakafuru, Shinyanga A & B pamoja na usimikaji wa nguzo za umeme huko Nyakafuru, Shenda na Masumbwe.

Majaliwa amemaliza ziara yake mkoani Geita na anaendelea kutafuta kura katika Mkoa wa Shinyanga.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya