*Awasihi waweke kando itikadi za vyama, wajali kupata maendeleo
NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka watanzania wamchague Dk. John Pombe Magufuli ili awe Rais wa Tanzania.
Alitoa wito huo leo Jumanne, Oktoba 27, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kata za Nakapanya na Namakambale, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma katika mkutano alioufanya akiwa njiani kuelekea Nachingwea, mkoani Lindi.
“Tupeni viongozi wa CCM ili waweze kukamilisha yale tuliyoaanzisha. Leo saa 10 jioni Rais wetu, Dk. John Pombe Magufuli atazungumza na Taifa kupitia kwenye vyombo vya habari. Tukae tumsikilize, yeye bado ni Rais wetu. Bado anawapenda watanzania, bado anataka kuwatumikia wananchi wake. Tumpe kura zetu zote za ndiyo.”
Alisema Rais Dk. Magufuli ana dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi na akawataka bila kujali itikadi zao, wampe miaka mingine mitano ili atimize malengo yake katika kuwaletea miradi ya maendeleo. “Hata kama uko ACT, CUF au CHADEMA, mchague Dk. Magufuli sababu maendeleo hayana chama,” alisisitiza.
Majaliwa alikuwa wilayani Tunduru ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Hassan Zidadu Kungu na wagombea udiwani wa kata hizo.
Akielezea utekelezaji wa Ilani iliyokwisha, Majaliwa alisema Serikali ilitoa sh. bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vyoo, mabweni, mabwalo, ukarabati wa shule kongwe za sekondari na uboreshaji wa miundombinu ili wanafunzi wafaulu zaidi.
“Tulileta sh. bilioni 3.4 za kufanya ukarabati kwenye sekondari za Matemanga, Nakapanya, Masonya, Mataka na Tunduru. Tumeanza kujenga mabweni ili watoto walale hukohuko, wasome vizuri na waweze kufaulu,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Majaliwa amewataka wakazi hao wajiandae kunufaika na fursa mbalimbali zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara hadi Mbamba-bay.
“Upembuzi yakinifu umekamilika, uchoraji wa ramani umekamilika na hii reli itaanzia Mtwara itapita Mnazi Mmoja hadi Masasi. Itapita hapa Nakapanya, itaenda Namtumbo, Songea mjini, Peramiho hadi Mbamba-bay.”
“Itakuwa reli ya umeme, itabeba abiria na mizigo. Na reli hii ikianza kujengwa, italeta ajira kwa wote katika maeneo yote itakapopita,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewataka wakazi wa Tunduru Mjini wakichague Chama Cha Mapinduzi kwa sababu ni chama chenye sera zinazotekelezeka.
Alitoa wito huo jana Jumatatu, Oktoba 26, 2020 wakati akizungumza na wakazi mji wa Tunduru na vitongoji vyake waliofurika kwenye viwanja vya uwanja wa ndege, kata ya Majengo.
“Sera za CCM zinatekelezeka kwa sababu ziko kwenye Ilani. Mafanikio yote haya mnayoyaona, yaliainishwa kwenye ilani. Ile imekwisha na sasa tumekuletea ilani nyingine ya uchaguzi yenye muendelezo wa yale yaliyobakia.”
Aliwataka wakazi hao wasikubali kugawanywa kwa misingi ya ukanda, ukabila wala udini.