Saturday, December 28, 2024
spot_img

HATUENDI KWENYE UCHAGUZI KWA JAZBA – MAJALIWA

 

NA MWANDISHI WETU

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka watanzania wasichague kiongozi kwa sababu ya jazba au hasira.

Alitoa wito huo leo Jumatatu, Oktoba 26, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Nalasi, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Katani.

Majaliwa alizuru Wilaya ya Tunduru akimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli.

“Hatuendi kwenye chama kwa jazba wala kwa hasira. Hatari ya kipindi hiki unaweza kujikuta unaenda kwenye chama ambacho hakina sera wala hakieleweki. Chama makini kinapaswa kuwa na viongozi wanaoeleweka,” alisema.

Akitoa mfano, Majaliwa alisema leo hii kuna chama viongozi wake wamegombana na wala hakina mgombea urais. “Je ukikichagua chama hiki na ukawa na changamoto inakukabili, utaipeleka wapi? Au utampelekea nani? Na ukimchagua diwani au mbunge wa chama hicho, hayo masuala yako atayawakilisha kwa nani?”

“Ninawasihi, unapochagua viongozi, usichague chama kwa sababu maendeleo hayana chama. Chagueni chama ambacho kina mwelekeo na kinajali kutatua shida za watu. Ukienda kupiga kura, chagua diwani, mbunge na Rais anayetoka Chama cha Mapinduzi. Keshokutwa, tumchague Dk. Magufuli kwa kura nyingi za ndiyo,” alisisitiza.

Majaliwa yuko wilayani Tunduru ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Adimu Mpakate na wagombea udiwani wa kata nne za jimbo hilo.

Akiwa njiani kuelekea Tunduru, Majaliwa alifanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya stendi ya mabasi ya Mangaka, wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akizungumza na wakazi wa Mangaka, aliwasihi Watanzania wasikubali kuandamana kwa kisingizio cha kutokubali matokeo ya uchaguzi kwa sababu huko ni kuvunja sheria.

“Ninawasihi vijana mjihadhari, msikubali kuandamana kwani mtakuwa mnavunja sheria na mtajikuta mnajiingiza matatizoni. Kuna mtu anakuja hapa na anatulazimisha kuandamana, huyo hafai kuwa Rais wa nchi.”

Majaliwa alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Nanyumbu, Yahya Muhata na wagombea udiwani wa kata zote za jimbo hilo.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya