Saturday, December 28, 2024
spot_img

DK. MAGUFULI KUIMARISHA MUUNGAO, DK. MWINYI KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI

 

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Zanzibar wamchague Dk. John Pombe Magufuli kuwa rais kwa sababu ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa kudumisha Muungano.

“Nawaletea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya makubwa kwenye uongozi wake uliopita. Hata kwenye wizara alizowahi kuongoza, pia amefanya makubwa. Ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa kutuunganisha wazanzibari na watanzania bara,” alisema.

Wito huo aliutoa Jumatatu, Oktoba 12, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Kairo, Kiwengwa, Wilaya ya Kaskazini B.

Alisema wako baadhi ya wagombea wanaotangaza kuuvunja muungano pindi wakichaguliwa na amewataka wananchi wa Zanzibar wawaepuke.

Alisisitiza kuwa kazi ya rais si ya mchezo na inataka mtu makini, kwa hiyo akawaomba wakazi hao wamchangue mtu ambaye ana uwezo wa kupambana na wala rushwa.

Majaliwa yuko Zanzibar kuwaombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi, wagombea ubunge wa majimbo, wawakilishi na wagombea udiwani.

Akimuombea kura Dk. Mwinyi, Majaliwa alisema Chama Cha Mapinduzi kina benki ya kutosha ya makada wenye uwezo wa kuongoza. “Chama Cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za uongozi na katika nafasi hii ya kuongoza Zanzibar, tumemleta Dk. Hussein Mwinyi.”

Alisema yapo mambo mengi mazuri yamefanywa na Dk. Ali Mohammed Shein na yaliyobakia yatakamilishwa na Dk. Mwinyi. “Masuala yote ya kipaumbele yamewekwa kwenye ilani ya uchaguzi yenye kurasa 303. Pia kitabu hiki kimesambazwa hadi kwenye shehia zenu. Kitafuteni mkisome ili muone mambo yaliyopangwa kufanyika kwa ajili ya Zanzibar.

“Maendeleo ya mifugo yamo humu, maendeleo ya uvuvi yamo humu, maendeleo ya ajira yamo, kuwezesha sekta binafsi yamo humu, kuwezesha viwanda yamo humu, kuwezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa nayo pia yamo humu,” alieleza.

Mapema, akinadi sera zake, Dk. Mwinyi alisema serikali yake itaimarisha uvuvi wa bahari kuu pamoja na bandari za uvuvi pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki ili kuongeza ajira na masoko kwa bidhaa za baharini.

Alisema ataimarisha ufugaji wa samaki ikiwa ni njia mojawapo ya kulinda mazingira. “Nitasimamia hilo la ufugaji wa samaki hasa kwenye maeneo ya mikoko kwa sababu tutakuwa pia tunalinda mazingira yetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa atashughulikia tatizo la mmomonyoko wa maadili na hasa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji wa wanawake na watoto. “Ninawaomba mtoe ushirikiano kwa sababu wanaofanya hivi vitendo mnawajua. Tusaidieni ili tuweze kudhibiti hivi vitendo vya udhalilishaji na dawa za kulevya,” alisema.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, Dk. Mwinyi alisema upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 72 na kwamba asilimia 28 iliyobakia ni ya kutoa maji kutoka barabara kuu hadi kwenye makazi ya watu. “Serikali yetu itakamilisha hiyo sehemu ndogo iliyobakia,” alisema.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuomba kura za Dk. Magufuli, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa CCM.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya