Salma Said |
NA MWANDISHI WETU
MWANAHARAKATI Salma Said amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni zikumuhusisha na uhusiano wa kimapenzi na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Akizungumza na TANZANIA PANORAMA Blog jana kuhusu taarifa za ndoa yake kuvunjika baada ya kufumaniwa na mumewe akiwa na Zitto, alisema haijavunjika na hana uhusiano naye wala hafahamiani naye.
Salma alisema taarifa zinazo muhusisha kimapenzi na Zitto aliziona mitandaoni tangu Ijumaa wiki iliyopita lakini alizipuuza kwa sababu anajua zina lenga kumziba mdomo ili asisimamie anayoyaamini katika shughuli zake za kiunaharaka.
Hata hivyo, Salma ambaye pia ni Mwandishi wa habari alihoji kama maswali anayoulizwa na TANZANIA PANAROMA Blog yanalenga kutumika kuandika habari na alipoelezwa lengo ni hilo aliomba habari hiyo isiandikwe.
“Wananichafua, Zitto siyo mpenzi wangu wala simjui. Sina chama mimi ni mwanaharakati. Wanataka tu kunifunga mdomo lakini siogopi wala sinyamazi.
“Yaani hata sijui kwanini hawa watu wa CCM na serikali wananiogopa. Tatizo la Zanzibar ukisema ukweli wanakuita mpinzani. Lakini mimi nilishazoea kuzushiwa kama unakumbuka hata nikipotekwa wakati ule walizusha kuwa nilikuwa nimefichwa na bwana mahali.
“Hiyo kitu sisi tuliiona mitandaoni tangu Ijumaa na nilipoiona tu nilimrushia mume wangu, yeye yupo Dar, akaniuliza nani kaandika nikamwambia apuuze,” alisema Salma.
Zitto |
Alipotafutwa Zitto simu yake ilionyesha inatumika muda wote na alipofatutwa Afisa Habari wa ACT Wazalendo, Arodia Peter alisema hana taarifa kuhusu hilo na kushauri atafutwe Zitto mwenyewe kulizungimzia na kutoa namba ya Zitto inayopatikana.
TANZANIA PANORAMA Blog lilimpigia tena Zitto kwa namba iliyotolewa na Arodia ambayo pia ilionyesha inatumika muda wote na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake hakujibu.
Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita kumekuwa taarifa zinazodai kuwa Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto amevunja ndoa ya Salma na kwamba mume wake amehamia jijini Dar es Salaam.