Thursday, December 26, 2024
spot_img

TRA YAUZA SHEHENA YA SABUNI ISIYOFAA

 

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)  imeuza kwa njia ya mnada shehena ya sabuni ya unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha.

Shehena hiyo ya sabuni iliingizwa nchini kutoka nje na kukaa bandarini bila kulipiwa ushuru kwa muda mrefu kabla TRA haijaamua kuiuza.

Habari za uhakika zilizokusanywa na Tanzania PANORAMA Blog zimeonyesha kuwa shehena hiyo ilikuwa na mifuko 1,800 ya sabuni ya unga aina AKO na imeuzwa kwa njia ya mnada na maafisa wa TRA huku wakijua kuwa wanatenda kosa linaloweza kuwa na athari mbaya kwa watakaoitumia sabuni hiyo.

Tanzania PANORAMA Blog limedokezwa na vyanzo vyake vya habari kuwa shehena hiyo ambayo thamani yake ni sh milioni 300, ilikuwa imehifadhiwa katika bandari kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam na imepigwa mnada mapema mwezi huu kwa sh milioni 20

“Watanzania tunaumizana wenyewe kwa wenyewe. Sabuni iliyopigwa mnada na TRA imekwisha muda wake wa matumizi na TRA walilijua hilo, sasa wameiingiza mtaani bila kujali kama itasababisha magonjwa kwa watakaoitumia,  wewe waulize uone kama watajibu, watababaisha tu maana wanajua siku hizi hakuna watu wa kichimbua mambo,” alisema mmoja wa watoa habari wa Tanzania PANORAMA Blog.

Alipoulizwa juzi, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo  haraka haraka alikanusha kuwa taarifa hizo hazina ukweli na kutaka atumiwe ushahidi wa uwepo wa shehena hiyo na alipotumiwa sehemu ndogo ya ushahidi aliotaka aliomba apewe muda kidogo afuatilie.

Hadi juzi jioni Kayombo alishindwa kutoa majibu kwani kila alipopigiwa alisema maafisa wanaohusika na minada na wale wa forodha wote wametoka ofisini hivyo anaendelea kuwasubiri na alipoombwa namba zao za simu alikataa kutoa.

Jana asubuhi,  Tanzania PANORAMA Blog lilimtafuta tena Kayombo ili kuzungumzia tuhuma hizo lakini hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani akikumbushwa ahadi yake ya kutoa kauli kuhusu tuhuma hizo na pia kutimiza wajibu wake alijibu kuwa kuna taarifa moja anaisubiri kutoka kwa wahusika wa mnada.

Tanzania PANORAMA Blog lilimtumia ujumbe mwingine likimshauri awe anapokea simu yake na kutoa taarifa hata kama hajafanikiwa kupata majibu husika na yeye alijibu kuwa akiwa kwenye kikao huwa hapokei simu kwa sababu siyo nidhami nzuri.

Kayombo


Baadaye mchana, Kayombo alitafutwa tena lakini hakujibu chochote na majira ya jioni alipiga simu na kueleza kuwa ni kweli shehena hiyo ya sabuni ilikuwepo TRA na imeishauzwa lakini haweza kusema kama muda wake wa matumizi umeishaisha au bado.

“Sasa bwana ni hivi. Ni kweli huo mzigo unaousema ni kweli ulikuwepo TRA. Ni kweli kabisa. Na mnada wake wa kwanza ulikuwa Agosti 24, 2020 lakini aliyeshinda hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndiyo ukauzika

” Ni kama kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zikiushindania kwa sababu yule mnunuzi wa kwanza hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndipo shehena ile ikachukuliwa kwa sh. milioni 21.5 ,” alisema Kayombo.

Alipoulizwa mnada wa pili uliofanyika lini na kukumbushwa kujibu swali aliloulizwa kuwa TRA inadaiwa kuuza shehena ya sabuni iliyokwisha muda wa matumizi huku ikijua kuwa inaweza kuwa na athari mbaya kwa watumiaji alisema maswali hayo hawezi kuyajibu.

“Hivi unaandikia chombo gani siku hizi……..  sasa hayo maswali mengine mimi siwezi kuyajibu we fahamu tu mnada umefanyika mara mbili,” alisema Kayombo.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya