NA MWANDISHI WETU
RAIS John Pombe Magufuli ndiye mtu pekee mwenye uwezo wa kiungozi kati ya wote waliojitokeza kugombea urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Hayo yameelezwa jana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Kata za Lubuga na Ilungu zilizopo Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.
Majaliwa yupo katika ziara ya kisiasa ya nchi nzima ya kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais Magufuli na amekuwa akitumia majukwaa ya kisiasa kuwanadi pia wagombea ubunge na udiwani wa CCM.
“Rais Magufuli anastahili kupewa nchi kwa sababu ana uwezo wa kuisimamia. Tanzania imekosa maendeleo ya haraka kwa sababu kulikuwa na tabia ya watu wachache ya kula rushwa na kuwaathiri wananchi wa chini wasipate mafanikio. Tunataka kiongozi wa nchi anayeweza kupambana na rushwa na mafisadi. Na huyo ndiye kiongozi tunayemtaka,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alisema chini ya uongozi wa Rais Magufuli, sera ya tiba kwa akinamama wajamzito na watoto na wazee ni bure. Huduma ya mama mjamzito kujifungua ni bure na kwamba Serikali ya Rais Magufuli imekwishatoa sh bilioni 10.8 kwa ajili ya huduma hizo.
“Tunayo Bima ya Afya ambayo tunataka tuiimarishe ili iwe ya kitaifa. Na leo tayari tunao muswada wa Bima ya Afya, tunataka tuunganishe wafanyakazi na wananchi wa kawaida ili watanzania wote wawe na Bima ya Afya.
“Si kila mara mtu anakuwa na pesa taslimu wakati anapopata mgonjwa kwenye familia na ndiyo maana inasisitizwa watanzania wote wawe na Bima ya Afya.
” Unapata kadi wewe na mkeo au mumeo na wategemezi wanne. Leo tuna watoto wanatoka Magu lakini wanasoma Chuo Kikuu cha Dodoma. Una mtoto yupo hapa lakini anasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, una mtoto mwingine anasoma Bwiru, akiugua huko na kuulizwa kitambulisho anatambulika kuwa ni mtoto wa fulani, anatibiwa.
“Haya yote niliyoyasema yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Dk. Magufuli na ndiyo sababu leo namuombea kura ili awe rais wa nchi hii,” alisema Majaliwa.
Aliongeza kuwa serikali imetoa sh bilioni 1.4 kwa Wilaya ya Magu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya .
Alisema kituo cha Afya cha Kahangara kimepata sh milioni 500 na ujenzi wake umekamilika, Kituo cha Afya Lugeye kimepata sh milioni 500 na ujenzi wake umekamilika na Kituo cha Afya Kabila kimepata sh milioni 400 na ujenzi wake upo katika hatua za mwisho.
Akizungumza kuhusu fedha za ununuzi wa dawa, Majaliwa alisema serikali imetoa sh bilioni 10.1 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba kila mwezi Wilaya ya Magu inapokea wastani wa sh milioni 108.
Kuhusu ujenzi wa barabara, Majaliwa alisema Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh bilioni 10 kupitia TARURA na TANROADS kwa ujenzi, matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi na madaraja kwa barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami ya Magu mjini yenye urefu wa kilomita 5.7 ambayo tayari imekamilika ikiwa imegharimu sh bilioni 2.7
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni Kisesa – Bujora yenye urefu wa kilomita 0.4 ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami, barabara ya Usagara – Kisesa yenye kilomita 16.14 kwa kiwango cha lami na usanifu wa kina wa barabara ya Magu – Ngudu – Hungumalwa yenye urefu wa kilomita 70.