NA MWANDISHI WETU
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa aseme serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero watanzania wanaojishughulisha na uvuvi.
Majaliwa ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mji wa Nansio, Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli.
Amesema katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, serikali iliondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio.
“Pia tumepunguza ada ya leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji baridi. Serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero wavuvi.
“Tumeweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa vifaa bora vya uvuvi, kuzuia uingizaji na uzalishaji wa zana haramu za uvuvi na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa zana na vyakula vya samaki,” alisema Majaliwa