RIPOTA PANORAMA – 0711 46 49 84
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limewaua watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya wizi toka maungoni, kuvunja na kuiba katika nyumba na maduka nyakati za usiku, unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa pikipiki.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai imeeleza kuwa watuhumiwa hao waliuawa wiki iliyopita katika eneo la Mbezi Luis wakati wakipambana kwa risasi na polisi wa kikosi maalumu cha kupambna na majambazi cha Mkoa wa Kinondoni.
Katika taarifa yake hiyo, RPC Kingai alieleza kuwa X.F. 407. CLP Bundala Said Kimenya na X.F. 1205 CLP Muhidin Sadick Mhina, ambao ni askari waliofukuzwa jeshini kutokana na matendo yao kihalifu waliuawa baada ya kukurupushwa na polisi wakijiandaa kufanya tukio la kihalifu.
“Mnamo tarehe 26/11/2020 majira ya saa 12 jioni huko maeneo ya Kimara Luguruni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni lilikuwa na taarifa fiche kuwa kuna majambazi wamepanga kufanya uhalifu kwa kutumia silaha katika eneo la Kiluvya.
“Kikosi maalumu cha kupambana na majambazi Mkoa wa Kinondoni kiliweka mtego Luguruni eneo la Sheli iitwayo hapa kazi tu karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, ambapo majambazi hayo yalikuwa yakitokea Kimara kulekea Kiluvya kupitia Morogoro Road.
“Walipofika eneo hilo wakiwa na gari lenye namba za usajili T 889 DKG, Toyota Brevis, rangi ya Silver walisimamishwa na askari polisi lakini hawakusimama, waligeuza gari yao kwa kasi kurudi walikotoka ndipo askari walipoanza kuwakimbiza majambazi hao lakini wakaanza kufyatua risasi hovyo.
“Walipofika eneo la Mbezi Luis karibu na Shule ya St. Anne Pr & Sec School, askari walifanikiwa kupiga tairi risasi ambapo gari lilipoteza mwelekeo na kuingia mtarono, jambazi mmoja aliuawa pale pale na watatu walikimbia huku mmoja akiwa amejeruhiwa mguu,’ inasomeka sehemu ya taarifa ya RPC Kingai.
Aidha, inaendelea kuwa baadaye polisi wakiwa katika ufuatiliaji walijulishwa kuwepo kwa jambazi eneo la standi ya Kibo aliyekuwa akitaka kupanda gari huku akiwa amejeruhiwa mguu ambapo askari walifika haraka na kumtia mbaroni akiwa na silaha.
Tatarifa inaeleza zaidi kuwa Mhina na Kimenya ni askari waliofukuzwa kazi kabla ya kuuawa kutokana na matendo yao ya kihalifu na kwamba watuhumiwa wengine wawili wanaendelea kutafutwa. Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mloganzila.