Monday, June 23, 2025
spot_img

DK. KASHILILAH: BUNGE LA SAMUEL SITTA


DK THOMAS KASHILLILAH

NA CHARLES MULLINDA
Mwandishi Mwandamizi wa Jarida la Umoja, Charles Mullinda alifanya mahojiano ya ana kwa ana na Katibu Mkuu wa Bunge, Dk.Thomas Kashillilah kuhusu alama zilizoachwa na Bunge la Tisa lililomaliza muda wake hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo, Dk. Kashililah anaeleza kwa undani safari ngumu ya utendaji kazi wa Spika, wabunge na Bunge kutokana na kuibuka kwa masuala kadha wa kadha mazito wakati wa kipindi chote cha Bunge hilo na namna walivyojipanga ndani ya Ofisi ya Bunge kukamilisha kazi ngumu waliyoikuta na wanayoiendeleza.
UMOJA: Ni nini tathmini yako kuhusu mwenendo wa shughuli za Bunge la Tisa lililomaliza muda wake mwezi uliopita?
DK. KASHILLILAH: Nikiwa mtendaji mkuu wa mhimili huo wa dola, nasema bila kusita kuwa halikufanya vizuri sana, baadhi ya wabunge walipwaya, huo ndiyo ukweli.
Na hapa nieleze kirefu kidogo. Mimi niliteuliwa kushika wadhfa wa Katibu wa Bunge mwaka 2009, lakini nilikuwa mtumishi wa Bunge kabla ya hapo.
Bunge ndiyo chombo cha kutekeleza shughuli za Serikali, hivyo hotuba ya kwanza ya Rais kwa Bunge huwa ni mwongozo kwa Bunge katika kutimiza wajibu wake.
Bunge lilikuwa linatekeleza yale yote yalioyozungumzwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kwanza ya Disemba 2005.
Tatizo lililojitokeza ni uelewa mdogo wa wabunge wengi kuhusu mambo ya kibunge ndiyo maana Spika akalazimika kuunda tume ya kufanya tathmini na kuchambua kanuni za Bunge, ambayo baadhi ya wajumbe wake walikuwa Dk. Harrison Mwakyembe, Hamad Rashid, Dk. Willibrod Slaa na Nimrod Mkono.
Hawa hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mambo ya kibunge isipokuwa Dk. Slaa. Lakini walifaidika kwa kutembelea mabunge ya nchi nyingine ambako walijifunza.
Tatizo la uelewa mdogo wa kanuni za Bunge kwa wabunge lilifanya fursa nyingi zilizotajwa kwenye kanuni hizo kutotumika kwa sababu wabunge walikuwa hawajui kuzitumia.
Nitatoa mfano, wabunge wengi walishindwa kutoa dukuduku au malalamiko ya wananchi katika utaratibu unaofaa. Hakuna mbunge hata mmoja, awe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) au upinzani aliyewasilisha maombi ya matatizo ya jamii, hakuna, na hii ni changamoto kubwa iliyoko mbele yetu. Wabunge wengi walikuwa wanatumia muda mwingi kulalamika badala ya kutoa maombi.
Angalia kwa mfano, marehemu Chacha Wangwe alikuwa na mambo mazito ya jimboni kwake lakini badala ya kutoa maombi aliishia kulalamika tu na hakuwa tayari kuja kuomba msaada wa ushauri wa nini afanye ili alichokikusudia kifanyiwe kazi na Bunge.
Wananchi wanaweza kuandika waraka wao wa malalamiko au jambo lolote halafu wakamfuata mbunge yeyote asiyekuwa wa jimbo lao wakamuomba kuuwasilisha bungeni kwa sababu mbunge wao kikanuni haruhusiwi kwa vile anakuwa na maslahi na jambo hilo. Ikiwa hivyo, Bunge ni lazima liutizame na kuushughulikia hadi mwisho.
Kinyume chake, akina Dk. Slaa na Hamad Rashid walikuwa wanatumia muda mwingi kulalamika badala ya kufuata utaratibu huu, hawakutumia fursa hii. Sasa  kwa ujumla wao kwa kutotumia fursa hizo vizuri Bunge lilionekana halishughulikii vizuri mambo mengi ya msingi.
Hamad Rashid alipoleta hoja ya kutaka kubadili Katiba bungeni, alikosea na hakutaka kujua. Huwezi kupeleka hoja hiyo bungeni mpaka upande wa Serikali uwe umetaarifiwa.
Alikuwa hajui na hakuomba msaada. Haya, hoja ya nyumba za Serikali, TRL, TICTS, Bandari na hata Kiwira ziligonga mwamba kwa sababu walioziwasilisha walikuwa hawajui kanuni.
Na katika hili tatizo ni wabunge wenyewe, taratibu za Bunge ziko wazi lakini ni wavivu kusoma, hawasomi matokeo yake baadhi ya mambo yanakwenda vibaya na wao wanabaki kupiga kelele za malalamiko tu.
Nayasema haya kwa faida ya taifa letu, angalia kwa mfano issue ya Riochmond. Bunge lilitoa maazimio kisha wabunge wakayang’ang’ania bila kujua kuwa wanapoteza muda, matokeo yake pamoja na kung’ang’ania angalia jambo hilo lilivyokwisha.

Wangekuwa wanasoma, wangejua kuwa baada ya Kamati Teule ya Bunge kutoa mapendekezo walipaswa kuziachia kamati za Bunge kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya na kuja kutoa taarifa bungeni.
Na kama kulikuwa na umuhimu, Bunge lingeweza kuunda kamati nyingine ya kuchunguza yaliyotokea katika ripoti ya Kamati Teule. Lingeweza kabisa kwa sababu lina mamlaka haya kama kuna mambo ambayo kulikuwa na umuhimu wa kuchunguzwa na Bunge. Na kamati hii inakuwa tofauti na ile teule, hii inakuwa ya kuchunguza.
Lakini kuna madhara yake. Iko hivi, Kamati Teule ya Dk. Mwakyembe  wakati ikifanya kazi ilikuwa ikijigeuza kama mahakama, sasa mashahidi wote iliowaita na kuwahoji na wao wakatoa ushahidi wanakuwa na kinga ya kutoshtakiwa mahakamani na wanapewa cheti cha kinga hiyo, hivyo hawawezi kuitwa na mahakama yoyote kwa shauri hilo.
Mfano hai ni kesi ya Augustine Mrema, ile ya milioni 800. Aliitwa akahojiwa, akapewa hati ya kinga ya Bunge hivyo alivyoitwa mahakamani akatoa ile hati ya kinga akapona.
Sasa walioitwa na Kamati ya Dk. Mwakyembe hawawezi kuhojiwa tena na mahakama yoyote na ndiyo maana hata Serikali ilikuwa inapata shida sana kulishughulikia suala hili.
Wabunge hili walikuwa hawajui ndiyo maana wakahangaika nalo kwa miaka miwili huku wakiacha mambo mengi ya msingi. Katika hilo naweza kueleza hivyo.
UMOJA: Kama hivyo ndivyo ni mambo gani basi ambayo unaweza ukasema Bunge lililopita lilifanikiwa kuyatekeleza?
DK. KASHILLILAH: Limefanikiwa, katika mambo yote yaliyofika mbele ya mikono yake yalitolewa maamuzi. Limeendelea na kazi yake ya kutunga sheria, limeshirikiana na asasi za kiraia katika mambo mengi yaliyokuwa na utata na kuyapatia ufumbuzi.
Mfano suala la Mfuko wa Jimbo lilikuwa na malalamiko lakini baada ya Bunge kukaa na wadau lilimalizika vizuri.
Limefanikiwa pia kuwa na bajeti yake ingawa hili linapaswa kutolewa maelezo zaidi, lina Tume ya Utumishi iliyoundwa upya na kazi zake ni kusimamia ajira na nidhamu.
Limeibana Serikali ikakubali kujenga ofisi za wabunge majimboni, limerekebisha kanuni zake, limefanya mageuzi katika uendeshaji wa shughuli zake kama kuwa na kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu na mengine mengi.
Kiutendaji, kamati zote za Bunge zimefuatilia sana shughuli za Serikali, lakini maboresho yanatakiwa hapo.
Kamati zina wajumbe wengi wanaoongeza tu gharama. Katika Jumuiya ya Madola kamati huwa zina wajumbe wachache, kwetu ni wengi pasipo sababu za msingi.
Ikumbukwe Bunge linakua, lakini muda wake wa kufanya kazi ni ule ule hivyo pamoja na kukua kwa Bunge lakini bado kazi zimefanyika vizuri, ni mafanikio.
Kwa usahihi zaidi niseme kwamba mafanikio ya Bunge ni kielelezo cha mafanikio ya Serikali.
Kama nilivyosema hotuba ya Rais wakati wa kuzindua Bunge ndiyo inayotoa mwelekeo wa utendaji kazi kwa Bunge. Kwa mabunge ya Jumuiya ya Madola ndivyo ilivyo, hata Uingereza, Malkia Elizabeth huwa anahutubia Bunge baada tu ya kuchaguliwa kwa Serikali mpya ili kutoa mwelekeo wa utendaji kazi wake.
RAIS MSTAAFU JAKAYA  KIKWETE AKIHUTUBIA BUNGE, WENGINE NI SPIKA WA ZAMANI MAREHEMU SAMUEL SITTA NA RAIS ZA ZANZIBAR, DK. ALI MOHAMED SHEIN

Rais katika hotuba yake ya kwanza kwa Bunge alitoa mwongozo wa kazi, aligusa maeneo ya mpasuko wa Zanzibar, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa madarasa na mengi mengine na yote yamefanyika. Hayo ni mafanikio.
UMOJA: Mchango wa Bunge miaka mitano iliyopita kwa jamii ukoje?
DK. KASHILLILAH: Kielelezo cha Bunge kuibana Serikali ndiyo mchango wake kwa jamii. Bunge limejisogeza zaidi kwa wananchi na sasa mwamko wa wananchi kufuatilia shughuli za Bunge ni mkubwa. Wananchi wanashiriki shughuli za Bunge na wabunge wanashiriki shughuli za jamii. Wabunge wanashiriki maonyesho mbalimbali na mambo mengine.
Wabunge wamekuwa mstari wa mbele kufuatilia utendaji wa halmshauri, hiyo ni kujibu kero za wananchi.
UMOJA: Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu kiasi kikubwa cha mishahara na posho wanazolipwa wabunge, unazungumziaje jambo hilo?
DK. KASHILLILAH: Wanavyolipwa watendaji wote wa Serikali ndivyo wanavyolipwa wabunge. Mshahara wa mbunge ni sawa na mshahara wa mkurugenzi, unakatwa kodi.
Mshahara wa jaji ni mara mbili ya mbunge. Jaji ana mafao ya uzeeni asilimia 80 ya mshahara uliopo wakati huo, mbunge hana. Ila inawezekana inasemwa hivyo kulingana na makundi yaliyopo katika jamii.
Sheria Namba 4 ya mwaka 1988 inampa Rais mamlaka ya kuamua mishahara na posho za watumishi wa Serikali na anasaidiwa na Katibu Mkuu Kiongozi na yeye anasaidiwa kufanya kazi hiyo na Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Niweke sahihi jambo hili, wabunge hawahusiki na kupanga mishahara wala posho zao, isipokuwa wanapendekeza, muamuzi ni Rais.
Utaratibu huu ndiyo unaotumika sehemu nyingi za nchi za Jumuiya ya Madola ili kuondoa wigo wa mtu kujipendekezea mshahara anaoutaka.
Mbunge katika kazi zake anapaswa kuwa na msaidizi anayelipwa kutokana na posho yake, akipenda anakuwa na dereva, gharama za mafuta ya kuzungukia jimbo na matengenezo ya gari na simu kwa siku 12 kwa mwezi anazokuwa jimboni, yote hayo yamo kwenye posho hiyo.
Posho ya mbunge ni shilingi milioni tano kwa mwezi na mshahara wake hauzidi sh. milioni mbili. Wana mkopo wa gari hivyo kila mwezi wanakatwa huo mshahara na posho hizo unaweza kusema ni kiasi kikubwa kweli kwa mlolongo huo wa matumizi?
Mimi ndiye Mtendaji Mkuu wa Bunge, nakuhakikishia kuna wabunge kwa mwezi wanachukua shilingi 400,000 tu kutokana na kukatwa mikopo yao.
Ni kwa nini wanafuatwa wabunge wakati kuna watu wanalipwa au kujilipa mamilioni hapa nchini? Mbona hao hawafuatwi kuulizwa?
Angalia pale PPF, posho zao wale kwa siku ni shilingi milioni moja, amini usiamini, bandarini kuna watu wanalipwa shilingi milioni 300 kwa miaka mitatu tu ya kufanya kazi.
Pale kuna watu wanafanya kazi kwa mkataba hivyo akichukua mkataba wa miaka mitatu akimaliza analipwa hizo milioni 300 na hapo akishalipwa anaweza tena kusaini mkataba mwingine na akalipwa, Benki Kuu ya Tanzania viwango vyao mmh!
Mimi sielewi kwanini wabunge wafuatwe wakati hawa jamaa ndiyo wanakula nchi ile mbaya, hawa ndiyo wanakula jasho la wananchi. Hebu kabla ya wabunge watizame kwanza hao.
UMOJA:  Spika wa Bunge anayemaliza muda wake, Samuel Sitta amekuwa akiandamwa sana kuwa anapenda maisha ya kifahari kwa kuishi kwenye nyumba ya gharama kubwa, kununuliwa gari lenye thamani kubwa na hata ujenzi wa ofisi yake ya ubunge imegharimu mamilioni ya fedha, hili nalo unalielezaje.
DK. KASHILLILAH:  Spika ni kiongozi wa kitaifa kama viongozi wengine wa kitaifa, kimaslahi hana tofauti na Jaji Mkuu. Anastahili kupewa makazi na Serikali, anapewa gari la kazi kwa stahili yake ambalo halitofautiani na la Jaji Mkuu na hilo alilo nalo sasa halitofautiani na la Jaji Mkuu, lakini Jaji Mkuu amekuwa nalo miezi tisa kabla Spika hajapewa.
Ni utaratibu wa kawaida kwamba kila baada ya miaka mitatu viongozi kulingana na nyadhifa zao wanapaswa kubadilishiwa magari, Spika alikuta lililokuwa likitumiwa na mtangulizi wake tangu mwaka 2004 akaendelea kulitumia hadi hivi karibuni alipobadilishiwa.
Spika hana maamuzi ya kununua gari lake la kufanyika kazi, makazi yake ya kuishi wala Bunge halina, ni Serikali.
Hapa nchini hakuna makazi ya Spika ndiyo maana anapangishiwa nyumba kulingana na wadhifa wake. Kuna majaji wamekaa katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski kwa miaka mitano wanalipiwa na Serikali, hao hawaulizwi ila inapofika kwa Spika inakuwa ni nongwa.
Kuhusu ofisi yake. Ofisi za wabunge zinajengwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, makatibu tawala wa mikoa ndiyo wahusika si Ofisi ya Bunge. Ofisi ya Mbunge wa Urambo ni Ofisi ya Spika, gharama ya mchoro na ujenzi ni tofauti na wabunge wengine.
Ni sawa na ofisi za mawaziri wakuu wastaafu majimboni mwao, ni tofauti na za wabunge wengine, ndiyo maana hata ofisi ya Mbunge wa Mpanda ni tofauti kwa sababu ni ya Waziri Mkuu. Hawa wana walinzi na wasaidizi, ndiyo maana ni tofauti.
Na ukweli ni kwamba gharama halisi iliyotolewa na RAS (Katibu Tawala) wa Tabora ambayo nakala ninayo gharama ya ofisi hiyo ni shilingi milioni 290.
Kwa wenzetu hasa nchi za Jumuiya ya Madola, katika uchaguzi Spika huwa anapewa upendeleo, hakuna mtu anayesimama kupambana naye wakati wa uchaguzi mkuu na hiyo ni kwa sababu kazi yake ya uspika inamkosesha fursa ya kwenda kumpigia magoti waziri kumsaidia mambo ya jimboni kwake wala haulizi maswali bungeni. Mpanda, Waziri Mkuu, Pinda hana mpinzani. Wale wameelewa.
UMOJA: Katika Bunge lililopita, Serikali mara kadhaa ilijikuta ikibanwa na wabunge kuhusu usiri wa mambo ambayo walidai yanapaswa kujadiliwa nao kwanza, unayazungumziaje madai haya?
DK. KASHILLILAH

DK. KASHILLILAH: Si kila kitu cha Serikali lazima wabunge wakijue ingawa katika sheria ya haki na madaraka ya Bunge, wabunge wanaruhusiwa kuitisha nyaraka zozote za Serikali isipokuwa zilizozuiliwa.
Nyaraka za majeshi ya ulinzi na usalama haziko wazi, lakini wabunge tena wa upinzani wanataka kuziona.
Haiwezekani kabisa kwa sababu kama taifa hata kama nia hiyo ya wabunge ni njema, ikiwa hivyo mnaweza kujikuta mnatoa taarifa zenu za siri nje.
Sheria imeainisha vizuri kabisa mambo haya, sasa kulazimisha tu haiwezekani na kuna mabadiliko ya kanuni ambayo yameeleza vizuri kabisa kuwa hata mikataba, ni ile tu inayoruhusu mtu wa tatu kuiona ndiyo inaonwa na watu wengine.
Kuna wabunge wanashupalia mambo haya, lakini wanajua kuwa haiwezekani, kama ni hivyo mbona hawaombi mikataba ya kununua vifaru au bunduki?
Mabingwa wa kulazimisha haya mambo wanajua ili kuona nyaraka yoyote ya Serikali ni lazima kuandika barua ya maombi kwa Katibu wa Bunge na yeye ndiye anashughulika na kukutafutia hicho kitu kama kinaruhusiwa.
Huwa tunawauliza kwa nini wanalazimisha mambo ambayo hayawezekani nao wanasema tunajua lakini lazima tupige kelele, lazima tusumbue, hivyo huwa wanafanya makusudi ili wasikike.
Hata kung’ang’ania washirikishwe kupitisha mikataba ya Serikali nacho ni kitu cha ajabu tu. Mbunge anang’ang’ania awe sehemu ya kupitisha mikataba ya Serikali wakati yeye ndiye msimamizi wa Serikali, ikiwa mibovu nani atahoji? Mambo ya mikataba ni jukumu la Serikali, si la wabunge.
Tatizo kama nilivyosema wabunge wetu wengi ni wavivu wa kusoma ili kuelewa mambo vizuri.
Kama wabunge wangeshiriki kupitisha mikataba ya ununuzi wa rada kwa mfano na mingine inayopigiwa kelele, sasa nani angeihoji Serikali? Wabunge wamepewa kazi ya kusimamia Serikali, wafanye kazi hiyo.
Haipaswi washirikishwe kwenye mikataba ya Serikali wala kuwa wajumbe wa bodi ya mashirika, si jambo sahihi kwani kupitia kamati zao ndiyo wanaoshughulika kufuatilia bodi hizo, sasa ikitokea bodi imefanya madudu na wabunge ni wajumbe si mambo ya ajabu! Nisema tu kuwa katika usiri, Serikali iko sahihi.
UMOJA:  Bunge lililopita limeacha kumbukumbu ya vituko vingi, vikiwamo vinavyohusu madai ya ushirikina na mengine yanayohusu baadhi yao kudai kuugua katika mazingira ya kutatanisha. Unayazungumziaje haya mambo pia?

DK. KASHILLILAH: Yalipokuwa yakitokea hayo ndiyo kwanza nilikuwa nimekabidhiwa ofisi. Kile kituko cha ushirikina kilikoanzia ni tofauti na kilivyoisha.
Ni  upuuzi ambao umechafua sura ya Bunge lililopita. Nadhani ni vema nikaeleza kidogo ingawa jambo hili silipendi kabisa, nafanya hivi kuweka kumbukumbu sawa.
Sijawahi kulizungumza hili na mwanahabari yeyote. Wewe unakuwa wa kwanza.
Nilifuatwa ofisini kwangu nikaambiwa niende bungeni kuna jambo zito limetokea. Nikahoji ni nini? Nikaambiwa kuna mtu amekamatwa akiwanga kwenye viti vitatu ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Baadaye hadithi ikageuka kuwa mtu huyo alikuwa anaweka dawa kwenye kiti kimoja. Aliyeanzisha jambo hili alikuwa na lengo lake maalumu, ni mtu kutoka Kanda ya Ziwa.
Mimi nilifuatilia kwa karibu jambo hili na kubaini kuwa kuna mwanasiasa kutoka Kanda ya Ziwa alikuwa anatafuta dawa ili kurekebisha mambo yake.
Mwanasiasa huyo alikuwa ameukosa uwaziri na kwa majibu ya taarifa nilizopata alikuwa anatizamwa vibaya na watu na hata baadhi ya marafiki zake walikuwa hawapokei simu zake, akaambiwa kuna dawa ya Kisukuma ambayo mtu kama ana mikosi akiitumia mikosi inakwisha.
Mwanasiasa huyo alienda kwa mganga akapewa dawa. Alipofika huko akaambiwa hata mwanasiasa mwenzake, Andrew Chenge naye alikuwa hapo kwa ajili ya dawa hiyo hiyo, basi huyo alipotoka hapo kufika Dodoma akasambaza maneno kuwa Chenge kapewa dawa kwa ajili ya kuweka bungeni.
Katika kufuatilia, nilikwenda kwenye kamera za wataalamu, tuliangalia kwa makini sana huku tukirudia rudia hatukuona mtu katika kamera akimwaga unga kwenye viti kama ilivyokuwa ikielezwa. Kumbuka kuwa kulikuwa na maneno eti kamera za Star TV zimewanasa watu hao wakati wakitenda jambo hilo. Hatukuona kitu kama hicho.
Kwa sababu ya uzoefu katika mambo haya, nikiwa Mtendaji Mkuu wa Bunge niliamua kujiridhisha kwa sababu madai kuwa kuna unga unga umemwagwa bungeni yalikuwa yananipa wasiwasi kuwa isije ikawa wamemwaga sumu ambayo inadhuru taratibu, baadaye waheshimiwa wakaanza kudhurika.
Niliamua kuita wataalamu kwa ajili ya kufanya uchunguzi na nilifanya hivyo kwa maamuzi yangu si maelekezo ya mtu. Wakafanya uchunguzi wakabaini hakukuwa na kemikali zozote.
Miongoni mwa watu waliodaiwa kuingia bungeni na kuweka dawa hizo za kishirikina ni mmoja wa maofisa wa Bunge, naye ni Japhet Sagasii.
Huyu nilikuwa nimemtuma mimi mwenyewe kumtafutia Chenge kiti. Wanasiasa ni watu wa ajabu sana, wakaamua kumsingizia ofisa huyo wa Bunge.  Niliporidhika kuwa ni upuuzi nikatulia.
Ajabu jambo hili lilipofikishwa katika vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Spika alipoulizwa ilikuwaje, yeye kwa sababu ya woga wake akanitaja mimi kuwa nilimwambia. Wenzake wakamwambia usimsingizie huyo mtendaji kwa  sababu ukweli unajulikana. Na mimi sikuwa na neno naye, najua alikuwa akijitetea.
Sasa nilichobaini ni kwamba wanasiasa ni watu wa kuchafuana, jambo hili lilipikwa makusudi kwa ajili ya kumchafua Chenge, lakini halikuwa na ukweli hata punje.

DK. MWAKYEMBE
Na hata kuugua kwa Dk. Mwakyembe hakukuhusiana kwa namna yoyote na mambo ya kishirikina. Dk. Mwakyembe siku moja kabla ya kujisikia vibaya alikuwa amekunywa pombe nyingi, tulikuwa Dodoma Hotel, sasa asubuhi yake alipoingia bungeni ndiyo hali ya kujisikia vibaya ilipompata, hakukuwa na sababu nyingine yoyote. Huo ndiyo ukweli. Hivi vituko ni vya wabunge wenyewe kwa sababu zao wenyewe.
UMOJA: Watumishi wa Bunge wamekuwa wakitajwa kuwa na utajiri uliopitiliza vipato vyao, ukweli ukoje katika hili?
DK. KASHILLILAH: Ni kweli, hili lipo ninajua kuwa linasemwa sana na wanaosema baadhi ni waliokuwa wabunge, lakini wanasema hivyo kwa sababu ya tofauti zao binafsi na wafanyakazi wa Bunge.
Ofisi ya Bunge ni kati ya chache zinazolipa wafanyakazi wake vizuri, hili lieleweke na kila baada ya mwezi mmoja na nusu kuna vikao vya Bunge vinavyotanguliwa na vile vya Kamati za Bunge.
Katika muda wote huo wa vikao watumishi hulipwa posho kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na wanapokuwa Dodoma, kwa siku 10 mfanyakazi anaweza kupata milioni 1.8 za posho. Sasa mtumishi huyo kumiliki gari dogo ni jambo la ajabu kweli?
Hapa bungeni, hata wahudumu wana magari na nyumba moja au mbili na wanamudu kupata vitu hivyo kulingana na vipato vyao vinavyotokana na kazi zao nzito, lakini tatizo liko kwa baadhi wabunge ambao hawapendi kulipwa sawa na watumishi wa Bunge, hao ndiyo wanaoanzisha vimaneno hivi kuhusu watumishi hawa. Lakini kila kitu kiko wazi.
UMOJA:  Mara kadhaa, Bunge limekuwa likiingia katika migogoro na waandishi wa habari au vyombo vya habari kwa madai kuwa waandishi wanakiuka maadili ya kazi yao, unalielezaje hili?
DK. KASHILLILAH: Kwanza haitakiwi kuwepo misuguano wala migogoro kati ya Bunge na waandishi wa habari.
Unajua zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za Bunge ni za Serikali, hii ni mihimili ya dola, lakini ‘media’ nao ni mhimili wa dola.
Ili mambo yaende sawa, Serikali, Bunge na Mahakama zinapaswa kufanya kazi kwa karibu na mhimili wa nne wa dola ambao ni vyombo vya habari.
Vyombo vya habari ndiyo daraja la muhimili hii mitatu na wananchi kwa hiyo haya mambo yanayojitokeza, yapo kweli lakini tunapaswa kuyatafutia ufumbuzi wa uhakika. Na mimi nasema ni lazima kuwe na ushirikiano wa karibu.
Misuguano na migogoro kati ya mihimili hii ipo sehemu nyingi tu duniani, haijaanza leo na chanzo kikubwa cha hali hiyo ni waandishi kukiuka taratibu.
Kila kitu kina taratibu zake, upo mahakamani unakatazwa kupiga picha, haiwezekani uingie uanze kupiga picha, hamtaelewana. Hata kwa Bunge ni hivyo hivyo, taratibu lazima zifuatwe ili tufanye kazi vizuri.
Ukiangalia kwa undani kiini cha tatizo hili utagundua kuwa pamoja na baadhi ya waandishi kuwa na elimu ndogo, pia hawapo waandishi walio –specialize kuandika habari za Bunge.
Leo wanakuja hawa ni wapya baada ya wiki kadhaa wanakuja wengine nao ni wapya, wanakuwa hawapo wenye uelewa wa mambo ya Bunge. Kungekuwa na waandishi maalumu wa Bunge, wakalisoma Bunge linavyofanya shughuli zake haya yasingekuwepo, naamini hivyo kabisa.
Ndiyo maana waandishi wanaandika Spika kajinunulia samani za mamilioni nyumbani na ofisini kwake bila hata kuchunguza taratibu zinasemaje kuhusu ununuzi huo. Spika hana mamlaka ya kununua kitu chochote cha ofisi yake, ni lazima zabuni itangazwe na mimi ndiye ninayeteua watu wa kuchambua zabuni hizo.
Nikishawateua sina mamlaka nao, ni kama Rais anapomteua jaji, hana uwezo wa kumfukuza mpaka jopo la majaji wa Jumuiya ya Madola likae na kuchunguza.
Hao nao wanafanya kazi yao na wanawasilisha ripoti yao kwa Bodi ya Manunuzi ambayo inapitia na kutoa maamuzi ndiyo yanaletwa kwangu. Kazi yangu hapo ni kusaini tu si kuongeza wala kupunguza. Ila kama hakuna pesa ndiyo nina uwezo wa kukataa kusaini nikawarudisha au nikaamua kuifuta zabuni.
Waandishi wa Bunge wanapaswa kufahamu mambo haya, unapomwandika Spika, mbunge au Bunge negative wakati si kweli unachafua, ndiyo maana misuguano inatokea. Tunalitazama hili, linatatulika na mimi nitasimama kidete ili kuweka mambo sawa.
UMOJA:  Ni yapi matarajio ya Bunge la 10 linalotarajiwa kuanza kazi mwishoni mwa mwaka huu?
DK. KASHILLILAH: Nina hakika kabisa hadidu za rejea za maswali yako zitatuwezesha kupima mafanikio.
Bunge la 10 hatutaki lirudie makosa, mathalani kurudia rudia hoja moja na kuifanya kuwa ndefu huku ikikwamisha shughuli za Serikali wakati utatuzi wake ni mdogo tu.
Changamoto hizi na nyingine zitatusaidia kuwapa elimu ya ufahamu wa kutosha wabunge wa jinsi wanavyopaswa kufanya kazi zao. Tutajitahidi kuwafanya wafanye kazi zao kwa mujibu wa kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Hatutaki wabunge warudie makosa ya kutojua hata kuuliza maswali kiasi cha kumlazimisha Waziri Mkuu kuomba msaada wa wataalamu wa Bunge kuwafundisha wabunge kuuliza maswali.
Ni aibu watu wanauliza maswali kama vile wanajieleza kwenye majukwaa ya siasa badala ya kuuliza maswali ya kisera yenye majibu ya jumla.
Tunajipanga kuwasaidia wabunge wajitegemee wenyewe katika shughuli zao. Wanahitaji msaada mkubwa na wanapaswa kujituma na kusoma sana. Wasiposoma mambo ya kibunge lini watajua kuwa mahali fulani wamedanganywa?
Inasikitisha kuna wabunge hodari sana wa kusoma magazeti mpaka ya udaku lakini hansard ya mwaka jana mbunge anataka umsimulie! Ni lazima wawe na tabia ya kusoma hata wanapokuwa majimboni kwao.
Zaidi ni kwamba nitajitahidi ili watumishi wa Bunge wasitumike vibaya, wabunge wanawatumia vibaya watumishi wa Bunge. Hawa watumishi wa Bunge wote wana shahada, lakini ndiyo wanaotumwa chai na vimemo na wabunge. Ni watendaji lakini wabunge hawataki kuwatumia vizuri.
Hili tutalibadilisha, yale mazoea kwamba watumishi wa Bunge ni makarani tutalibadili.
Bunge lijalo tunatarajia liwe la kazi kweli kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kibunge. Tutawafanya wabunge wajue kuwa watumishi wa Bunge wakiwatumia vizuri watajua mambo mengi sana. Hii ndiyo changamoto yetu kubwa.
UMOJA: Nakushukuru sana Dk. Kashillilah.
DK. KASHILLILAH: Asante Mullinda, karibu tena wakati wowote.          
MAHOJIANO HAYA YALICHAPISHWA KATIKA JARIDA YA UMOJA OKTOBA 2010
                                    

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya