DAR ES SALAAM
Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL) inayomiliki mashamba ya Mkonge yaliyoko Tanga, imesema inatekeleza kwa awamu agizo la Serikali la kuyaendeleza mashamba hayo.
Mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo ameeleza kuwa baada ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula kuipa 24 za kuyaendeleza mashamba hayo ilianza kuliyafanyia kazi agizo hilo.
Afisa huyo alisema uendelezaji huo unafanyika kwa awamu kwa sababu siyo jambo rahisi kuliendeleza eneio lote kwa wakati mmoja na tayari imekwishawasilisha mpango wake ya kuaendeleza mashamba hayo kwa Serikali.
Maelezo hayo yanajibu taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa sekta ya Katani kuwa agizo la Serikali lililotolewa na Naibu Waziri Mabula, halijatekelezwa tangu mwaka jana ingawa kampuni hiyo iliandika barua serikalini ikieleza namna itakavyotekeleza kwa awamu uendelezaji huo.
Disemba 8, mwaka jana, MeTL ilipewa siku 24 na Serikali kuyaendeleza mashamba hayo yenye ukubwa wa hekta 9,418 ambayo miongoni mwake hayajaendelezwa na badala yake yamegeuka kuwa pori.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani maarufu kwa jina la Profesa Majimarefu ambaye aliambatana na Naibu Waziri Mabula katika ziara hiyo ya mwaka jana, alieleza kuwa MeTL ilimilikishwa mashamba hayo mwaka 2000 lakini tangu wakati huo ilishindwa kuyaendeleza kikamilifu.