MACHI 2, 2018
ZITTO AACHIWA ‘NYUMBA’
Zitto Kabwe |
DAR ES SALAAM
Waasisi wawili wa Chama cha ACT- Wazelendo na viongozi waandamizi 10, leo wamekipa kisogo chama hicho wakikiacha mikononi mwa Kiongozi Mkuu, Zitto Kabwe wanayemtuhumu kutoa kauli za kuhamasisha Serikali iliyoko madarakani iangushwe.
Tukio hilo lilitokea jana asubuhi katika Hotel ya Silver Paradise, iliyopo Tip Top, Masenze ambako walifanya mkutano na waandishi wa habari, walioundaa kwa ajili ya kutangaza uamuzi wao.
Waliokipa kisogo ACT- Wazalendo ni Ramadhani Ramadhani, aliyekuwa Makamau Mwenyekiti wa Kwanza wa Taifa (Zanzibar) na mwanzilishi wa chama aliyekiandikisha kwa msajali, Leopold Lucas Mahona, Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza (Bara) na pia mwanzilishi aliyeshiriki kukiandikisha chama kwa msajili na Hudson Mwakyambiki ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini.
Katika orodha hiyo wapo pia Ernest Kalumna, Katibu wa Chama Mkoa wa Dar es Salaam, Mikidadi Ramadhan Kirungi, Katibu wa Jimbo la Ubungo, Khalfan Sidadi, Katibu waJimbo la Kibamba, Sadick Mohamed Msangi, Katibu Mwenezi Jimbo la Ubungo, Swaumu Hamis Msipu, Mwenyekiti Ngome ya Wanawake Jimbo la Ubungo na Robert Kihiri, Mwenyekiti Ngome ya Vijana Jimbo la Ubungo.
Wengine ni Mtangi Hatibu Semwanza, Mwenyekiti wa Kata ya Manzese Jimbo la Ubungo na Ally Hamis Semwanza, Katibu wa Chama Kata ya Manzese, Jimbo la Ubungo.
Katika tamko lao la kujivua uanachama na kujiunga na CCM walilolisoma mbele ya waandishi wa habari, ACT- Wazalendo ambacho awali kilijipambanua kuwa tumaini jipya kwa Tanzania kikiwa kama chama mbadala kimeacha misingi yake.
Walieleza awali, ACT- Wazalendo kilichojinasibu na misingi 10 bora ya uzalendo, usawa, uwazi, utu, kupinga ubaguzi, demokrasia, uhuru wa mawazo na matendo, uadilifu, uwajibikaji na umoja.
“Leo haijulikani ni upi kati ya misingi hii unatekelezwa sawia. Tunaumia tunapoona chama chetu kupitia kwa viongozi wa juu wa chama, nasi leo tunaungana na wanaohujumu juhudi za Serikali kupigania maslahi ya wanyonge wa taifa hili. Uzalendo ambao ni msingi mama wa chama chetu uko wapi?
‘Tumesikia wajumbe wa kamati kuu wakilalamika na wengine wakihama chama kwa sababu hakuna tena kamati kuu siku hizi. Kuna kakikundi ka wapambe wachache wanaoamua mazito ya chama,’ walieleza katika tamko lao.
Aidha, walitoa mfano kuwa uamuzi wa kujitoa katika chaguzi bila vikao halali hawauafiki kwa sababu ACT- Wazaledo siyo kampuni ya mtu mmoja na wapambe wake bali chama cha siasa.
Kwamba baada ya kubomoa misingi bora waliyoijenga, chama hicho kimebaki kuwa kikundi cha wanaharakati tu huku ofisi zake zote za mikoani na katika majimbo zikifungwa imebaki na kusalia za mkoani Mwanza na Kigoma.
Zitto |
‘Viongozi wala hawashtuki, wanadhani chama ni makao makuu na mitandao ya kijamii. Tumeshtushwa zaidi na kauli za karibuni za Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe kuhamasisha viongozi wa Chadema wakae na kufanya maamuzi anayodai sisi tutawaunga mkono huku akimalizia kwa kusema Serikali hii ni rahisi sana kuiangusha.
‘Hii ni ishara ya juu sana ya kiongozi wa chama kufilisika kisiasa na kitendo cha kamati kuu ya chama kushindwa kukutana kutoa tamko la kupinga kauli hizi, maana yake ni kweli kwamba kwa sasa chama hakina kamati kuu na tunakubaliana na wale wanaosema chama siku hizi kinaendeshwa na mtu mmoja na wapambe wake.
‘Tumejiuliza sana juu ya Serikali anayotaka kuiangusha Zitto Kabwe. Ni ya rais huyu huyu ambaye alimsifia sana kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Novemba 2015? Mbona hajawahi kutuambia ni jambo gani ambalo Rais Magufuli (Dk. John) aliliahidi kwenye hotuba yake hiyo ambalo halitekelezi? Ni hii hii ambayo aliisifia sana kwa kupeleka sheria mpya ya rasilimali za taifa bungeni?
‘Ni ya rais huyu huyu aliyemsifia sana kwa hatua alizochukua baada ya ripoti ya kamati za makinia? Ni ya Rais Magufuli huyu huyu ambaye akiwa ziarani mkoani kwake Kigoma mwaka jana alimsifu na kumwambia jinsi wana Kigoma akiwemo yeye wanavyompenda kwa sababu ya kuleta maendeleo? Mbona hajatuambia sasa Rais Magufuli haleti tena maendeleo?’ walisema.
Walisema kwa kuzingatia mwenendo usioridhisha wa chama hicho wameamua kujivua uanachama na kujiunga na CCM.
Mikoto brog itawaletea uchambuzi wa mwenendo wa kisiasa na anguko la ACT-Wazalendo. Usikae mbali.