Machi 2, 2018
MADIWANI WA CHADEMA WAFICHWA
Joseph China |
MBEYA
Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakitajwa kuwa na nia ya kukihama chama hicho kwenda kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) walichukuliwa na kufichwa eneo la siri ili wasitekeleze azma yao.
Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Mbeya, Joseph China ndiye aliyethibitisha kufichwa kwa madiwani hao wakati akizungumza na waandishi wa habari wiki hii.
China aliwaeleza waandishi wa habari kuwa baada ya kusikia tetesi kuhusu mpango wa madiwani hao kuhamia CCM aliitisha kikao cha dharura cha madiwani wote wa Chadema walio kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa ajili ya kuwahoji.
“Ni kweli, wiki hii niliitisha kikao cha dharura. Kilianza saa mbili 2.00 na kumalizika saa 10.00 jioni. Nilitaka kuwasikia wao wenyewe waliokuwa wanatajwa kutaka kuhamia CCM. Baada ya kuwahoji walihifadhiwa sehemu kwa muda.
“Hilo siyo jambo la ajabu kuwaita na kuwahoji kwa sababu nilikuwa na taarifa zote kuhusu mpango wao wa kutaka kukikiacha chama na kwenda CCM. Na walipanga kulitekeleza hilo siku ya mkutano wa CCM, ambao Katibu Mwenezi wa chama hicho, Humphery Polepole alikuwa anauhutubia,” alisema China.
Alisema kwa wadhfa wake wa mwenyekiti wa chama wa mkoa hakuwa tayari kusubiri aibu hiyo imkute.
China alisema madiwani wote ambao majina yao yalikuwa yakitajwa kuwa kwenye mpango huo walikanusha kuhusika nao na badala yake walitoa sababu za kuhusishwa na jambo hilo.
Alisisitiza kuwa hayuko tayari kuona Chadema kinakimbiwa na wanachama na hasa madiwani kipindi hiki ambacho kuna wimbi kubwa la wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM.
Alisema wana Chadema wenye nia hiyo wanapaswa kusubiri hadi wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2020 ndiyo watekeleze nia yao.