MACHI 2, 2018
KAKONKO WAOMBA WATAALAM WA MIAMBA
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo |
KAKONKO
Wananchi wa Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma wameiomba Serikali isaidie kuwapatia wataalam wa miamba watakaotafiti na kubainisha kiasi cha madini yaliyogundulika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ambaye yuko katika ziara ya kikazi wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala alisema Madini ya Dhahabu yamegundulika katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alitaja baadhi ya maeneo yaliyogundulika kuwa na madini hayo ni pamoja na Nyamtukuza, Kasuga na Muhange lakini haijaweza kufahamika ni kiasi gani kilichopo.
“Tunakuomba utusaidie upatikanaji wa wataalamu ili kujuata kwimu sahihi za kiasi cha madini kilichopo kwenye maeneo yaliyogundulika,” alisema.
Kanali Ndagala alisema wilaya hiyo ina madini mengi chokaa katika Hifadhi ya Pori la Akiba la Moyowosi lakini hayachimbwi kwa sababu ya sheria za hifadhi haziruhusu.
Akijibu maombi hayo, Naibu Waziri Nyongo alisema Serikali itafanya tafiti mbalimbaliza madini nchini kwa kuwatumia wataalamu wa jiolojia kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).
“Tutawaelekeza wataalam wetu wafike hapa Kakonko kufanya utafiti,” alisema Nyongo.
Aidha, aliahidi kulifanyia kazi suala la upatikanaji wa Madini ya Chokaa katika eneo la hifadhi.
Naibu Waziri Nyongo, anaendelea na ziara yake ambayo itahitimishwa mkoani Kigoma baada ya kuitembelea mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa nne kutoka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kakonko.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kakonko, ofisini kwa mkuu wa wilaya hiyo jana.
|