RIPOTA PANORAMA
WIKI ya elimu kwa mlipa kodi inatarajiwa kuanza Machi 5 hadi 9, mwaka huu katika mikoa yote nchini.
Kwa mujibu ya taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Koyombo lengo lililokusudiwa katika wiki hiyo ni kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto na kupokea mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa walipakodi.
Taarifa ya Kayombo ilieleza kuwa pamoja na masuala mengine TRA itatumia wiki hiyo kutoa elimu ya ulipaji kodi ya majengo kwa njia ya kielektroniki, elimu kuhusu mkataba wa huduma kwa mlipa kodi na matumizi sahihi na umuhimu wa kutumia Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs).
Ilieleza zaidi kuwa pia itatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kudai na kutoa risiti kila wanapouza au kununua bidhaa na huduma mbalimbali na kufanya usajili wa walipakodi wapya kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 ambapo TRA imekusudia kusajili walipakodi wapya milioni moja nchi nzima.