![]() |
Rais Magufuli |
RAIS John Pombe anaweza kushindwa. Anaweza kushindwa kupata mafanikio ya kuridhisha katika mapambano dhidi ya ufisadi kwa sababu jeshi lake lina wapiganaji wa kale wanaokimbia mchakamchaka huku wakiimba wimbo wasiouamini.
Yeye mwenyewe ni mpambanaji mzuri, anajua kuchora  ramani ya vita, anajua kuhamasisha majeshi yake kwa nyimbo za kimapinduzi kama ule wa hapa kazi tu na anajua kuwatungua adui.
Mafanikio aliyoyapata katika vita dhidi ya ufisadi si ya kupuuzwa na haina shaka ataendelea kuyapata. Lakini ili aendelee kufanikiwa hana budi kuachana na baadhi ya wapiganaji wake waliochoka na wanaoamini katika mbinu za kale kwenye medani ya vita dhidi ya ufisadi na mambo mengine ya hovyo.Â
Ulazima huo unatokana na ukweli kwamba vita ya ufisadi na mabadiliko yenye lengo la kujenga Tanzania mpya ina sura moja tu kwa sasa: Kwamba inapiganwa na askari wa kale, wenye silaha za kisasa, wanaoongozwa na kamanda shupavu na mwenye uchu wa kushambulia adui.Â
Mwenendo wa utendaji kazi wa serikali ya Rais Pombe unatoa taswira kwamba yeye ni jemedari shupavu wa vita ya ufisadi, anao wapiganaji shupavu na wachovu aliowateua kuunda naye serikali; na wanazo silaha nzuri ambazo ni katiba, sheria kanuni na taratibu zinazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya utendaji serikalini.
Upande mwingine wa uwanja wa vita wapo maadui ambao ni mfumo mbovu wa utumishi uliojipenyeza na kuota mizizi serikalini na katika sekta binafsi, uhuru usiokuwa na mipaka wa kufanya shughuli za kisiasa, tabia chafu na mbaya za baadhi ya watanzania, ukiukwaji wa makusudi wa sheria za nchi na kila aina ya mambo ya hovyo yaliyokuwa yakitendeka kabla ya kuanza kwa vita inayopiganwa sasa na jeshi la Rais Pombe.
Katika vita hii jambo moja liko dhahiri kwamba jeshi la Rais Pombe haliwezi kupigana na kushinda vita hii bila uwepo wake; kwamba siku akikosekana katika uwanja wa mapambano jeshi lake litachakazwa na adui.
Jeshi la maadui linamuhofia Rais Pombe na wasaidizi wake wachache kwa sababu ni kamanda shupavu na jasiri. Awapo vitani sura yake hujaa makunyanzi, dalili kwamba yupo vitani akiangamiza adui na hata sauti yake ni ya kimamlaka, inasikilizwa kwa umakini na wapiganaji wake na wakati mwingine inawatisha adui kiasi kwamba wanaitii.
Haina shaka kwamba Rais Pombe anazijua kanuni na taratibu za vita dhidi ya ufisadi. Katika vita ya aina hii, adui huwa haachwi hata anapokuwa amenyoosha mikono juu kujisalimisha bali hufungwa pingu na kutupwa msambweni kabla ya taratibu nyingine dhidi yake kufuata.
Kwa waliosikia tangazo lake la vita kuwa huwa hajaribiwi na inapobidi sheria zenye ukakasi huziahirisha ili zisitoe mwanya kwa adui kuangamiza umma na jeshi lake watakuwa na imani na uimara wake vitani.
Kwa wapiganaji wa Rais Pombe hali ni tofauti. Wapo waliopewa vikosi kuviongoza lakini badala yake vinawaongoza wao. Wapiganaji wa aina hii ndiyo wale wanaojaribu bila mafanikio kuuishi wimbo wanaouimba kila siku wa hapa kazi.
Katika baraza la kivita linalotunga sheria na kanuni za mapambano, wapiganaji hawa wapo. Wanasigana na wapiganaji wenzio kiasi cha kutaka kutwangana wenyewe kwa wenyewe. Wamegawanyika.
Huko barazani tayari wapiganaji wa Rais Pombe wamekwishapitisha azimio la kuitwa na kuhojiwa kabla ya kupokwa madaraka kwa kamanda aliyefyatua risasi ya kwanza dhidi ya wauza unga.
Bila kujali kuwa ni mpiganaji mwenzao na pia shambulio la risasi yake limeamsha morali ya vita dhidi ya mihadarati; iwe ilimpata au kumkosa adui, kamanda huyo anashambuliwa na wenzake kwa kutumia silaha nzito nzito. Wamemuelekezea tuhuma nzito nzito zikiwemo za aibu ili wamvunje moyo.
Wapiganaji wa Rais Pombe wameungana na maadui kutaka vita dhidi ya mihadarati isitishwe, kisa! wanaotuhumiwa ni watu wazito hawapaswi kushambuliwa hadharani bali kwa uficho.
Kwa tathmini ya kichokonozi, shutuma na maneno machafu ya wapiganaji wa Rais Pombe walioko barazani yanalichafua jeshi zima.Â
Mategemeo ya wananchi kwa jeshi hili yanabaki siri yao moyoni kwa sababu wanawaona wapiganaji wao wakiwa wamechoka, wanasinzia lakini wakiulizwa wanajitetea kwa ukali kuwa kusinzia ni aina mpya ya kutafakari.
Hawataki kukoselewa wala kushauriwa, anayeshauri huwa wanajiapiza kumshughulikia. Wanao uwezo wa kumshughulikia yeyote kwa sababu walikwishajitwalia madaraka ya kuwashughulikia waliowachagua.
![]() |
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ameshika mfuko wa mbolea ya Minjingu |
Jeshi la Rais Pombe linaloimba wimbo wa imani wa hapa kazi tu bila kuuamini, limeshindwa kufahamu kuwa kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Minjingu kilichopo Manyara, kinachotumia malighafi ya Tanzania kutengeza mbolea, kinaipakia kwenye mifuko iliyotengenezwa nchini Kenya ikiwa na nembo ya Kenya.Â
Bila juhudi za kamanda wao zilizobaini hilo pengine wasingegundua hadi mwisho wa vita.
Halitakuwa jambo la ajabu kwa kitengo cha propaganda cha jeshi la Rais Pombe kuibuka na kupingana na tathimini hii ya kichokonozi.Â
Ikitokea hivyo wachokonozi hawatashangaa kwa sababu wamekuwa wakikifananisha kitengo hicho na kile kilichokuwa kikiongozwa na Mahamudu Assawahaaf wa Ghuba ambaye hakupata kukiri ukweli wakati taifa lake lilipokuwa likishambuliwa na majeshi ya kigeni.
Anachopaswa kufahamu Rais Pombe ni kwamba kitengo chake cha jeshi la propaganda ni butu, hakina uwezo wa kukabiliana na kile cha adui, kinatumia mbinu za kale kusambaza propaganda hivyo hazivutii.
Na nadhani kwa sababu kudhani siyo kosa, nadhani Rais Pombe analijua hili ndiyo maana ana mapenzi ya dhati na televisheni ya mawingu na amekuwa hasiti kupangua makamanda wa vikosi vya majeshi yake.
Sasa, wakati vita hii ikielekea awamu ya pili na ya mwisho, Rais Pombe anapaswa kulipanga upya jeshi lake. Asipofanya hivyo anaweza kupigwa, kama siyo sasa basi hata wakati wa lala salama.