Kibanda |
NIMEPATA fursa ya kukaa kitako na Absalom Kibanda na kuzungumza naye mambo mengi huku anakotibiwa baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya na genge la wahuni wanaojijua. Katika mazungumzo yetu nimegundua kuwa Kibanda hana shukrani hata kidogo.
Nafasi hiyo nimeipata baada ya kumtembelea nchini Afrika Kusini aliko sasa. Tumezungumza mengi sana lakini katika mazungumzo yetu hakuna hata mara moja Kibanda alitoa shukrani kwa watu wanaoonekana kuwa wema mno kwake wakati huu anapouguza majeraha aliyonayo.
Kibanda hawashukuru wale wanaoonyesha kumpenda ghafla hivi sasa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa, anatilia mashaka upendo wao, haamini kama upendo wa ghafla wa baadhi ya watu hawa kwake ni wa kweli. Kwa maana nyingine hawa anawaona wanafiki tu.
Hawashukuru kwa namna yoyote waandishi wa habari wote wanaoonyesha kiherehere kilichopitiliza cha kuripoti kila neno linalosemwa na hao wanaojifanya wema sana kwake hivi sasa.
Ukimsikiliza kwa makini utagundua kuwa anachokiamini ni kwamba waandishi hawa wanatumika, hawajui au wanajua wanachokifanya lakini kwa makusudi wameamua kukubali kutumika ili kupotosha ukweli wa kuteswa kwake.
Polisi na makachero nao ni hivyo hivyo. Wanasiasa wambea na wapenda sifa ndiyo kabisa hataki hata kuwazungumzia kwa muda mrefu kwa kile anachosema kuwa ukisikiliza waongo watakuchanganya.
Kibanda haamini kuwa maadui zake anaowajua na asiowajua wanastahili kuanza kushambuliwa kwa maneno ya kuwahusisha na kuteswa kwake mpaka hapo uchunguzi utakapowabaini kuhusika. Anawapenda maadui zake na sababu ya kuwapenda anayoieleza ni kwamba wanamsaidia kuishi kama Absalom Kibanda.
Shukrani zake za dhati anazielekeza kwa Mwenyezi Mungu aliyemnusuru na kifo. Hajali sana ulemavu alioupata kwa sababu anaamini mwanadamu kabla hajafa hajaumbika.
Anamuomba Mungu uchunguzi wa suala lake ufanywe kwa uhakika ili watakaobainika kumtendea ubaya wabebe mzigo wao kwa haki. Kwa sasa hataki kumuamini mtu yeyote, yuko tayari kwa matokeo ya uchunguzi wa haki na anatamka bayana kuwa uchunguzi huo ukibaini waliomuumiza, hata kama mama yake mzazi atatajwa, hatamhurumia, atamuacha abebe msalaba wake.
Kwa wanaomfahamu Kibanda naamini watakubaliana na mimi kuwa siyo jambo rahisi kubadili kile anachokiamini, hivyo kumfanya abadilike, awe na shukrani hata za uongo kwa waliompenda ghafla baada ya kuumia ni jambo gumu.
Nilijaribu pasipo mafanikio jambo hilo. Katika mazungumzo yetu nilimwambia kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi kubwa ya kuandika kwa kina mwenendo wa hali ya afya yake na wanafuatilia kwa karibu uchunguzi unaofanywa na makachero kuhusu kuvamiwa na kuteswa kwake.
Nilimtajia magazeti yanayoongoza kwa kuandika habari za tukio lake huku nikiamini kuwa atatoa pongezi na shukrani kwa waandishi wa magazeti hayo kwa namna wanavyojitoa kufuatilia tukio hilo lakini ajabu alisema hafurahishwi hata kidogo na mwenendo wa utoaji wa taarifa zake katika magazeti hayo.
Hakunificha hisia zake, alinieleza kuwa anafuatilia kwa karibu uandishi wa waandishi wenzake wa hapa nyumbani lakini haumfurahishi. Hafurahi kwa sababu wapo waandishi ambao wamekuwa wakichukua mawasiliano yake binafsi kwenye mitandao na kuyafanya habari.
Aidha, alinieleza kuwa amebaini uwepo wa kundi la waandishi ambalo linafanya kazi ya kundi la watu fulani linalotiliwa shaka kuwa huenda linajihusisha na utesaji wa raia kwa sababu za kipuuzi tu za kusaka tonge kubwa.
Anaamini pia kuwa wapo waandishi wanaotumiwa na wanasiasa kupotosha ukweli wa tukio lake na wapo wanaotumiwa na viongozi fulani kuandika uongo wenye lengo la kuwakinga na hisia zozote mbaya kutoka kwa wananchi kuhusu matendo yao maovu.
Waandishi anaofurahishwa nao ni wale wanaofanya kazi zao kwa umakini, wanaochunguza kila aina ya taarifa wanayoipata kabla ya kuiandika. Hata hivyo, nao hawapi asante. Kisa! Anakijua mwenyewe, ingawa nadhani anaamini kuwa muda wa kuwashukuru kwa kazi yao nzuri haujafika.
Kibanda haamini tetesi, anataka ukweli. Ukweli ambao kwa Tanzania yetu kuubaini siyo jambo jepesi. Kuamini katika ukweli kwa Tanzania ni sawasawa na kuamini katika ndoto. Uchunguzi wowote wa kichokonozi ambao huegemea zaidi katika kudhani anausikiliza lakini hauamini.
Hajali kabisa kazi kubwa na ngumu ya kukusanya umbea katika mitaa ya uswahili kwa wachokonozi inayofanywa na wachokonozi wenyewe ambayo mara nyingi imekuwa na matunda mazuri ya kuibua yale yaliyojificha.
Siku chache kabla sijaondoka Johannesburg, tukiwa tumezama katika mazungumzo mazito, nilimueleza Kibanda kuwa zipo hisia kwa wachokonozi zinazohusisha tukio lake na mambo ya kishirikina.
Nilimweleza kwa utaratibu sana kuwa wachokonozi wamefuatilia rekodi za vifo vya watu katika ofisi aliyokuwa akiifanyia kazi zamani na kubaini kuwa upo utaratibu maalumu wa kutokea matukio ya vifo kwenye ofisi hiyo.
Kwamba kila mwaka kuna mfanyakazi mmoja anayekufa katika ofisi hizo na inaaminika chanzo cha vifo hivyo ni ushirikina.
Vifo vya namna hiyo huhusishwa na nguvu za giza ambazo hutumiwa na wenye tamaa ya pesa kupitiliza kulinda utajiri wao au kuuongeza.
Ili kumuaminisha na uchunguzi huo wa kichokonozi nilimwambia pia kuwa taarifa za makachero wa kichokonozi zimebaini kuwa mara kadhaa, yeye Kibanda alikwishapewa taarifa na wafanyakazi wenzake za kukutwa kwa matone ya damu katika mlango wa ofisi yake hiyo ya zamani hivyo inawezekana kabisa kuwa akiwa katika ofisi hiyo alikuwa akiwindwa kuuawa pasipo mafanikio na baada ya kuondoka hao waliokuwa wakiitaka roho yake kwa nguvu za giza waliamua kuisaka kwa nguvu za kigaidi.
Kibanda haamini taarifa hizo za kiitelijensia za wachokonozi. Haamini katika nguvu za giza. Waliojitoa kuifanya kazi ngumu ya kuwapeleleza wanga wanaodaiwa kumchawia ofisini kwake pasipo mafanikio hawashukuru kwa sababu haamini katika ulozi. Kibanda ni mtu wa ajabu sana, licha ya kukiri kufikishiwa taarifa hizo na wafanyakazi wenzake wakati huo, bado haamini.
Katika mazungumzo yetu hayo, nilimdokeza pia kuwa baadhi ya waandishi wa habari marafiki zake wenye roho za kutu, wanafiki, wanaojifanya wema kwake wakati ndiyo wabaya wake wamenaswa na kamera za kichokonozi wakitafuta mawasiliano ya simu ya watu walio karibu naye kifamilia ili wawashawishi washiriki kupindisha ukweli wa kushambuliwa kwake.
Nilimweleza mwenendo mzima wa uchunguzi wa kichokonozi ulioonyesha kuwa marafiki zake hao walipojaribu kuunganishwa na watu walio karibu naye ili wapatiwe namba hizo za mawasiliano waligoma katakata, walikuwa wanafanya jambo hilo kwa siri kwa sababu wana lengo baya.
Ajabu, Kibanda baada ya kusikiliza maelezo hayo kwa umakini mkubwa alisema anawajua, taarifa zao anazo, fitna zao kwake anazijua muda mrefu, hivyo hata haya wanayoyafanya sasa wakiamini kuwa hayatajulikana yeye hashangai. Eti! anamuachia Mungu anayeona hila na uovu wao kwake kwa sababu anawaona na atawalipa kwa matendo yao.
Hata hivyo, neno zito aliloniambia Kibanda muda mfupi kabla hatujaagana ni hili; kwamba maadui wa mawazo na misimamo yake wako katika Kampuni anayofanyia kazi sasa ya New Habari (2006) Ltd, CCM, Chadema, CUF, baadhi ya waandishi wa habari, polisi hadi wana usalama, hivyo inategemea ni nani aliyemuudhi sana kuliko mwingine pasipo yeye mwenyewe kujua.
kibanda akifarijiwa na Bashe |
Sasa, kwa sababu Kibanda ataendelea kutawala mjadala wa safu ya Mchokonozi kwa kipindi kirefu kijacho, kauli yake hii nailaza kiporo hadi Jumatano ijayo kutokana na umuhimu na uzito wake.