![]() |
Kibanda |
NIKO nchini Afrika ya Kusini kwa takriban wiki moja sasa. Nimekuja kumjulia hali kaka, bosi na Mwalimu wa wachokonozi, Absalom Kibanda ambaye alivamiwa, akashambuliwa na kujeruhiwa vibaya na wahuni fulani ambao wanajijua
.
Kibanda alinipokea Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, yeye na mkewe na saa chache kabla sijaondoka Tanzania nikiwa uwanja wa ndege Dar es Salaam, alinipigia simu na kunitaka ninunue magazeti ya Mtanzania, Tanzania Daima na Raia Mwema, nimempelekee. Nilifanya hivyo.
Nikiwa angani kuja Johannesburg, picha tofauti tofauti zenye sura ya Kibanda zilikuwa zikinijia japokuwa nilikuwa nabugia kilevi kwa wingi ili nilewe, ajabu haikulewa. Akili yangu ilikataa kulewa, ikaendelea tu kuniletea sura za akina Kibanda wengi.
Nilipotua, ni Kibanda aliyeniona kwanza pale uwanja wa ndege wakati nashangaa shangaa. Aliniita, ‘dogo, nimekufuata usije ukapotea.’
Alinikumbatia kwa furaha. Aliniuliza mambo mawili matatu ya huko nyumbani huku akicheka kicheko chake cha kijivuni, kicheko cha wachache. kisha akasema ‘nimekumbuka sana nyumbani!
Kibanda ni yule yule, sura yake ni nzuri kama ilivyokuwa kabla hajajeruhiwa, anazungumza kwa sauti ile ile yenye kigugumizi kwa mbali, mwili wake ni ule ule uliojengeka kwa misuli hasa ya kiume, isipokuwa anavaa mivani nyeusi machoni.
Majeraha aliyokatwa na panga kichwani na kupigwa nondo sasa yamekauka. Kidole chake kimoja kilichokatwa bado kimefungwa bandeji. Taya lake lililovunjwa vunjwa kikatili na watesaji limeumbwa upya. Meno yake yaliyolegea kwa kupondwapondwa yamefungwa waya maalumu ili kuyaimarisha upya. Akitabasamu au kuzungumza ni Kibanda wa siku zote.
Mguu wake uliotobolewa kwa kitu chenye ncha kali nao umefungwa bandeji nyeupe peee ya kizungu. Anatembea mwenyewe lakini siyo mwendo mrefu. Anatia moyo.
Nilikuwa na hamu ya kumuona, nilichukua dakika kadhaa kumuangalia na nikiwa namuangalia juu hadi chini huku nikiishangaa zaidi miwani yake nyeusi anayovaa machoni, aliniambia, ‘dogo, wamening’oa jicho la mwilini, lakini wameniachia jicho la rohoni. Ninajiona nimezaliwa upya.’ Sikumuelewa, nikawa nimeduwaa tu, alichokifanya ni kunishika mkono kuniongoza kuondoka pale uwanja wa ndege.
Nilichokigundua kwake ni kwamba anajitahidi sana kufanya mazoezi ili mwili wake urudi kwenye hali ya kawaida. Anafanikiwa kidogo kidogo, hajaweza kutembea mwendo mrefu akitembea kwa dakika kadhaa anasikia kizunguzungu, anakaa chini.
Analazimika kufika hospitalini kila mara kusafishwa vidonda na kupatiwa tiba na madaktari bingwa wanaomtibu. Bado anasubiri kufanyiwa ipasuaji kwa mara ya pili kuwekewa jicho.
Kwa muda wa siku saba za kuwa na Kibanda hapa Johannesburg tumezungumza mengi. Nimemsimulia mengi ya nyumbani na yeye amenisimulia mengi ya huku ugenini. Yapo yanayohuzunisha na mengine yanayofurahisha.
Ukizungumza na Kibanda kwa sisi wachokonozi unapata picha ya nini kinachoendelea. Unaweza kuhisi ni nani ambao walihusika kumtenda unyama kama huo. Nasisitiza unaweza kupata picha ya mambo hayo iwapo tu una akili za kichokonozi.
Kati ya mengi tuliyozungumza, mambo mawili nitayaeleza hapa kwa sababu naamini yana ujumbe mahususi ndani yake.
Mosi. Kibanda amewamiss sana watanzania, hapokei tena simu nyingi kama alizokuwa akipokea kutoka kwa wasomaji wake wa safu ya Tuendako na wala hapokei simu toka kwa watu mbalimbali kama ilivyokuwa awali kabla hajajeruhiwa wakati akitekeleza kazi zake za uandishi wa habari.
![]() |
Mbowe |
Lakini Kibanda amewamiss zaidi Freeman Mbowe, Dk. Willbrod Slaa, John Mnyika na waandishi wa habari wenzake.
Katika mazungumzo yetu, Kibanda aliniambia ‘wapo marafiki zangu waandishi nimewamiss sana, natamani kuongea nao lakini hawajanipigia. Ningekuwa na simu zangu huku ningewapigia tuzungumze mawili matatu.
‘Bwana mdogo Eric Antony sijamsikia kabisa, huwa anautani utani wa kufurahisha yule dogo. Said Kubenea naye nina muda mrefu sana, tangu tulipoachana nyumbani alipigia mara moja au mbili hivi kwa simu ya Eric Kabendera au wife nadhani, baada ya hapo amekuwa kimya, ukirudi nyumbani kawasalimie sana.
Anakaa kimya kidogo halafu anaendelea ‘Mbowe, Mbowe, Nasikia alikuja hospitalini pale Muhimbili siku ile nilipoumizwa, sikuweza kumuona, nilikuwa na hali mbaya sana. Ni rafiki yangu Mbowe, nadhani ametingwa, hajanipigia kabisa.
‘Yes! Na Mnyika, John Mnyika na Dk. Willbrod Slaa nimewakumbuka, rafiki zangu hawa wana kazi nyingi sana, hawajanipigia. Acha wachape kazi.’
Hivi ndivyo Kibanda anavyowakumbuka baadhi ya watu huko nyumbani, naamini moyoni mwake anashangaa inakuwaje watu hawa aliokuwa nao karibu katika mambo mengi hawajamjulia hali tangu alipoumizwa? Hata hivyo, sina maana kuwa nawafundisha cha kufanya, hapana, nilikuwa nafikisha ujumbe tu.
![]() |
Mnyika |
Jambo la pili lililonigusa katika mazungumzo yangu na Kibanda ni mtizamo wake kuhusu waandishi wa habari wanavyoshughulika na sakata la kutekwa na kuumizwa kwake.
Kwa maneno yake mwenyewe anasema, ‘ninakerewa sana na namna baadhi ya waandishi wa magazeti ya Mtanzania na Tanzania Daima, wanavyoripoti suala hili. Kwa makusudi tu mnapotosha. Mullinda, mnanikera sana nakwambia, acheni kupotosha, fanyeni uchunguzi wa kina kabla ya kutoa taarifa zenu.’
Haishii hapo, anafafanua kuwa, zipo habari zinazoandikwa kumuhusu yeye ambazo siyo za kweli. Zinapikwa kwa sababu ambazo hazijui. Kwamba waandishi wanamuwekea maneno mdomoni.
Kibanda anaeleza kuwa waandishi wamekubali kutumika katika suala la kuumizwa kwake. Wanaingilia hadi mwenendo wa uchunguzi unaofanywa na makachero wa polisi. Kwamba wamekuwa viherehere kupitiliza kwa kunasa kila fununu na pasipo kuifanyia kazi wanaiandika gazetini.
Huku akionyesha kusikitishwa na mwenendo huo wa uandishi, anasema waandishi wanapaswa kujua kuwa wahalifu wanaweza kujifanya watu wema sana na kuwajaza kila maneno ya kuwaumiza kuhusu yeye yatakayowasukuma kuandika habari potofu dhidi ya sakata lake ambazo lengo lake ni kuwaweka kando wahalifu hao na sakata zima.
Haya ni maneno yenye kufikirisha sana. Nadhani waandishi wanapaswa kuyachukulia kwa uzito unaostahili ili kuepuka kuingia katika mtego wa kuwakinga wanaoweza kuwa wahusika wa sakata hili na mkono wa sheria.
Kwa mtu yeyote mwenye macho makini naamini atakubaliana na mimi kuwa anayoyasema Kibanda yanapaswa kuzingatiwa kwa sababu zipo dalili za wazi kabisa zinazofanywa kwa makusudi na baadhi ya watu za kuhakikisha kuwa genge la watu fulani lionekane lina uchungu sana na jambo hili na kamwe haliwezi kwa namna yoyote hata kufikiriwa kutekeleza uhalifu.
Tukubali kujitazama upya.