Saturday, April 19, 2025
spot_img

NINAKUAMKIA KAKA ABSALOM KIBANDA


Kibanda
ABSALOM Norman Kibanda, ninakuamkia kwa lugha adhimu ya kichokonozi, shikamoo kaka.
Ninakuamkia kwa upendo uliopitiliza wa kichokonozi huko kitandani kwa wageni ulikolala ukiuguza majeraha uliyoyapata baada ya kuvamiwa, ukashambuliwa na kujeruhiwa vibaya na genge la wauaji. Wanajijua.
Waliokuvamia walikuchokonoa sehemu mbalimbali za mwili wako, wakakutoboatoboa bila huruma maungo yako kakamavu, wakakupondaponda kifua na kichwa kisha wakakusagasaga udongoni kabla ya kukutupa hapo walipokutupa ukiwa mahututi, hivyo hata ningekukuta hapo usiku ule nisingekuamkia bali ningekuzoa na kutimka nawe mbio za nyika kuelekea hospitalini kama walivyofanya waliofika kwanza hapo ulipotupwa. 
Leo ukiwa hospitalini ukiendelea na matibabu, naamini ni wakati muafaka kukuamkia, ninatumai amkio langu hili lenye heshima zilizo juu ya kuheshimu linakufikia na unalisikia.
Kibanda, ninakuamkia sasa kwa sababu tangu tulipoachana kazini usiku ule wa kuteswa kwako milango ya saa nne hivi, sijapata kukuamkia tena kwa lugha yetu nzuri ya kichokonozi. 
Ninakuamkia kama ninayekuona, ninakuamkia kama yalivyokuwa mazoea yetu ya kujuliana hali kila tulipokutana asubuhi au mchana kazini. Ukianza wewe ilikuwa lazima utabasamu kwanza ndipo utamke; dogo salama? Nami kwa mbwembwe za kuamkiwa na mtu mkubwa anayeheshimiwa mno na walio na heshima na hata wale ambao hawana nilizoe kuitikia; niko poa mkubwa, shikamoo kaka Kibanda.
KIbanda
Na pale nilipokuamkia kwanza mimi, ilikuwa hivi; shikamoo kaka mkubwa. Nawe kwa kiburi chenye akili, kiburi cha kujivunia kuamkiwa na mchokonozi, kwa sauti yako yenye kitetemeshi cha kigugumuzi uliitikia kimamlaka; marahaba dogo. Halafu basi. Ilikuwa raha sana!
Leo ni siku ya nane tangu tulipoonana na kujuliana hali kwa sababu Jumatano ya Machi Sita, nilipofika Hospitali ya Muhimbili kukujulia hali baada ya kutaarifiwa na dada yako mdogo Ratifa kuwa u mahututi kitandani, nilipokuona nilishindwa kukuamkia. Domo langu kubwa lilikuwa zito kutoa salamu, lilibaki wazi likiushangaa mwili wako jinsi ulivyokuwa umechakazwachakazwa na watesaji wako. 
Nilishindwa kukuamkia kwa sababu sikuamini kuwa niliyekuwa namuona kitandani pale ndiye Absalom Norman Kibanda, ambaye ni kaka, mwalimu na bosi wa wachokonozi.
Nilipofika kukujulia hali ulikuwa umelala kitandani umenyooka, kimya kabisa usingizini. Shikamoo yangu usingeisikia. 
Nilijaribu kukupiga ukope kukupa ishara kuwa kitandani ulipokuwa ulizungukwa na viwashawasha lakini hukuona kukonyezo langu. Ni jicho lako moja, moja tu la mkono wa kulia ndilo lililokuwa likibubujika chozi la damu bila kujali kuwa ulikuwa usingizini. Ni hilo jicho ndilo lililoniaminisha kuwa bado una pumzi yako.
Bosi Kibanda ninakuamkia ili kukubrief story za siku saba zilizopita za huku nyumbani. Ni kawaida yetu kupeana brief ya story kila siku tukiwa ofisini, sasa kwa sababu haupo kwa siku saba nzima ninakubrief huko huko kitandani.
Magazeti yote unayoyaongoza yanakwenda vizuri. Waandishi, wahasibu, wahudumu, wale akina mama wa gengeni, maofisa wa utawala, vijana na wazee wa usambazaji, magangwe na walimbwende wa sales, wadogo zako wasanifu kurasa, madereva, wahariri na Ofisa Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, tangu ulipopatwa na mkasa huo mbaya wanafanya kazi kwa nguvu na bidii kubwa utafikiri hii kazi ni ya baba yao! 
Bashe
Hussein Bashe hatulii, anafanya kazi zake na zako. Kisa! kutomuangusha Kibanda kwa kuhakikisha malengo aliyoweka ya utendaji kazi yanatimia. Brother, kama unacho kiona mbali cha wazungu hapo kitandani, chungulia hapa Sinza Kijiweni utajionea mwenyewe. Utafurahi!
Ni wachache sana wachawi, waliotofauti na wengi hapa ofisini! Wanajijua! Wanafahamika kwa sura zao zilizopauka hovyo hovyo na hivyo kuzikosesha mvuto wa kutazamika machoni. Wewe na sisi wala tusiwe na papara nao, dunia itawaeleleza.
Kibanda, kwa muda wa siku saba zilizopita story kubwa hapa nyumbani ni mkasa wa kuvamiwa na kushambuliwa kwako. Waandishi wanasaka taarifa za maendeleo ya afya yako kwa udi na uvumba. Watanzania wanafuatilia kwa karibu sana mwenendo wa afya yako, sikujua kuwa unapendwa kiasi hiki! Zile habari za nane nane na ushirika kwanza siku hizi zinatupwa ndani. Wewe unajua maana ya kutupwa ndani kaka.
Habari yako kubwa iliyozua majonzi kiasi cha watu kububujikwa na machozi ni ile ya kung’olewa jicho lako la kushoto, baada ya matabibu bingwa kushindwa kulinusuru. Hata hivyo wengi waliinua mioyo yao juu kumshukuru Mungu kwa kuendelea kukujalia uhai. Uhai wako ni muhimu zaidi kwa familia yako, ndugu zako, wanahabari wenzako, marafiki zako na watanzania wote kwa ujumla.
Story nyingine ni ile ya Jeshi la Polisi kuanza kuwasaka waliokuhunia na limekwishatangaza dau la Sh. Milioni tano kwa atayefanikiwa kutoa taarifa zitakazowesha kuwakamata. Kazi imekwishaanza, lakini nikwambie ukweli! Uswahili kwa wachokonozi watu wanachekea kwapani kuhusu uchunguzi huo, kama ujuavyo vituko vya uswahili kaka, ni umbea na upashkuna tupu!
Eti! Wanahoji hiyo tume iliyoundwa ni tofauti na ile iliyochunguza tukio jingine baya kama hilo lililokukuta wewe la kutekwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka? Wanasema kama wakubwa wanataka hiyo tume iaminike, watoe ripoti yenye akili ya tume iliyochunguza tukio la kinyama la Dk. Ulimboka. Sijui wewe unaonaje hapo? 
Kaka Kibanda, story nzuri zaidi ni ile inayomuhusu Ridhiwani Kikwete. Amefanya jambo zuri mno kwako wewe mwenyewe na kwa watanzania wote. Ameibua hisia mbaya kwa wengi, ameichafua Ikulu kwa kukumbushia mambo mabaya ya nyuma, tunapaswa kumpongeza.
 

Ridhiwan

Kwa makusudi tu ya kutaka watanzania wafikirishe vichwa vyao ili kujua ukweli wa haya yanayotokea sasa, alichukua picha yako ukiwa hoi masikini pale Uwanja Ndege wa Dar es Salaam muda mfupi kabla hujasafirishwa nje kwa matibabu, tena ukiwa na mkeo, akaipachika kwenye ukurasa wake ‘face book’ halafu akaandika kwa kuhoji hivi; Je, hii nayo ni kazi ya Rama (Afisa Usalama wa Taifa) wa Ikulu? Ndiyo ujue kaka jinsi  Ridhiwani alivyo kitatange.
Swali la Ridhiwani lilikuwa zito na lenye kuibua fikra nyingi mchanganyiko kwa wenye akili. Lilikuwa swali linalothibitisha Rama Ighondu, aliyetajwa kuwa ni mwanausalama wa Ikulu na mtu ambaye alihusika moja kwa moja na kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka yupo pale Ikulu na kazi yake ni kutesa na hata kuua, lakini katika tukio hili la kinyama ulilofanyiwa wewe, Rama hakuhusika na kama yupo ambaye anajua ni Rama tena athibitishwe kwa kujibu swali hilo la Ridhiwani.
Ingawa Ridhiwani mwenyewe juzi alikaririwa na gazeti moja akilalama kuwa mtandao wake uliingiliwa naamini alikuwa akijitetea kitoto kwa sababu imemchukua zaidi ya saa 40 kutoa utetezi wake huo, jambo ambalo katika hali ya kawaida haliwezekani kwa sababu ni nadra sana mtu kukaa kimya kwa muda wote huo wakati mtandao wake umepenyezewa ujumbe wenye kuhatarisha uzuri wa sura ya Ikulu na kuwachonganisha wananchi na kiongozi wao.
Hivyo naendelea kuamini kuwa andishi lile ni Ridhiwani limefufua upya uchungu wa wananchi dhidi ya Ikulu, limechochea hasira ya wananchi dhidi ya serikali, lakini pia limesaidia kujua ukweli kuwa Rama kweli yupo na yupo Ikulu na kazi yake ndiyo hiyo kama alivyoandika Ridhiwani ya kumtesa mtu kijasusi kiasi cha kumuua.
Kaka Kibanda, watanzania wanapaswa kuamini hivyo kama alivyosema Ridhiwani kwa kuhoji kwa sababu tangu Rama alipotajwa na Gazeti la Mwanahalisi kuwa kinara wa unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka, siyo Ikulu wala chombo chochote cha serikali waliopata kukanusha.
Hivyo basi jambo la muhimu hapa ni kwamba huu unyama uliofanyiwa nadhani Rama hakuhusika ila aliyehusika ni mtu mwingine wa aina ya Rama. Kwa sababu hiyo tukijielekeza kwenye swali la Ridhiwani nadhani utakubaliana na mimi kuwa tukio lako hili halihitaji uchunguzi wa tume.
Kwa kuutambua ukweli huo kama tulivyosaidiwa na Ridhiwani naomba ubaki na imani kuwa watanzania sasa wanajua kwa kudhani kuwa ni akina nani waliokutenda mabaya hayo, lakini hawana la kuwafanya isipokuwa kumuomba Mungu hamsini zao zifike haraka.
Kaka Kibanda itoshe kwa leo kukupa brief za story, niishie hapa. Panapo majaaliwa, nitakuamkia tena Jumatano ya wiki ijayo. Nakuacha sasa upumzike ili na mimi nipate muda wa kutangatanga.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya