Saturday, April 19, 2025
spot_img

NINAKUAMKIA JULIUS KAMBARAGE NYERERE


J.K Nyerere
MWALIMU Julius Kambarage Nyerere, ninakuamkia shikamoo. Habari za miaka 12 iliyopita?
 
Ninatambua umetu‘miss’ sana watanzania wako ambao hutujakuona kwa muda mrefu sasa baada ya kuondoka bila kutuaga.
Hukutuaga wala hatukukuaga kwa sababu ulifia mbali, ugenini kwa wazungu. Hao ndiyo waliokuona ukikata roho, wakakufunika macho na kuunyoosha mwili wako vizuri.
Sisi watu wako tulipokea kiwiliwili chako na kukifukia ardhini. Basi. Inauma sana kwa mtu tuliyekupenda kutuacha bila neno la mwisho.
Kama wewe ulivyotu‘miss’ nasi ni hivyo hivyo. Tumeku‘miss’ mno. Na amini usiamini, siku si nyingi tutakutana tena huko uliko.
Tuko mbioni kufa kutokana na ugumu wa maisha unaosababishwa na upumbavu wetu wa kukiuka yale uliyokuwa ukitukaza. 
 

Umaskini

Tangu ulipotuacha tumesahau kabisa mema na mazuri uliyotufanyia na kutufundisha. Tumekumbatia mambo ya hovyo na ya kipuuzi ambayo yanatuumiza na kutusababishia mateso na majuto makuu mioyoni mwetu.
Ni kwa sababu hiyo ya kutosikia kwetu ndiyo maana tunaelekea kufutika ulimwenguni pasipo mapenzi yetu wala ya muumba wetu. Tunastahili kulaaniwa kama hatuteswi na laana ya kukupuuza.
Mwalimu, tangu ulipoondoka bila kutuaga na nadhani hukutuaga kwa sababu uliona hakuna haja hiyo kutokana na uzumbukuku wetu, Tanzania yenye neema uliyotuachia sasa imegeuka kuwa yenye laana.
Tunatawaliwa kwa nguvu na mafisadi. Wanatukamua mpaka jasho la damu. Makaburu uliokuwa ukiwapiga vita sasa wamejaa nchini mwetu, tunawaita wawekezaji.
Wako kila pembe ya nchi wakichuma rasilimali zetu ambazo enzi za uhai wako ulizilinda kwa gharama kubwa, wanachukua na kuzipeleka kwao, ughaibuni na wanafanya hivi kwa baraka za wakubwa wanaotutawala.
Mwalimu, Tanzania yako uliyoiasisi sasa inatawaliwa na watu uliowakataa kwa nguvu zako zote kuwa watawala. Walitumia miaka kumi kuutafuta utawala wakafanikiwa.
Sasa wanatutawala kweli na staili yao ya utawala ni kushiba wao kwanza, kisha marafiki zao na mwisho ndiyo sisi.
Wameunda genge la kihalifu walilolipachika jina la wanamtandao. Genge hili ndilo linalotuchagulia viongozi. Linaongozwa na maburushi wala rushwa wakubwa ambao enzi zako ulikuwa ukiwacharaza bakora bila huruma.
Genge la kihalifu la wanamtandao sasa limekiteka chama, ndilo linalokiongoza na linaowapa nafasi za uongozi ni wezi, wazinzi, wababe na kidogo sana utakuta kuna waadilifu wawili watatu.
Linawatumia vijana wetu wa ulinzi na usalama kutukandamiza, wanatupiga kweli hasa tunapojaribu kutumia haki yetu ya kuandama kwa amani kushinikiza kupatiwa haki zetu za msingi. Mwalimu, tunaonewa kweli.
Miaka 12 baada ya kutuacha tumetambua kwa nini ulikuwa unakataa watawala wa sasa wasiwe watawala. Katika utawala wao taifa limefika pabaya, linaelekea shimoni, tumaini la kuiona kesho halipo.
Ni katika utawala huu ndiyo nchi imekumbwa na mabalaa ya kila aina. Njaa imekuwa yetu mwaka hadi mwak, elimu uliyokuwa ukiitoa bure nayo sasa imekuwa anasa, tunalazimishwa kuilipia, eti kusoma bure katika nchi inayotiririka madini na aina nyingi za rasilimali zilizoko hapa duniani ni dhambi.
Waliosoma wakaelimika kwa kutumia rasilimali hizo ni wale uliowasomesha wewe. Ajabu ni hao hao uliowasomesha bure ndiyo ambao sasa hawataki wenzao wasome bure. Watu wa ajabu, wana roho mbaya. Hakika ulisomesha ibilisi wa kuja kutusindikiza kwenda motoni.
J.K Nyerere
Mwalimu, wajukuu zako wanaookoteza kila senti za wazazi na walezi wao ili wapate walau bora elimu kwa sababu elimu bora uliyokuwa ukiitoa wewe sasa hawawezi kuipata wanakukumbuka sana wanapokuwa katika mateso ya kukong’otwa na virugu vya Askari Polisi wa kikosi maalumu cha ‘fanya fujo uone’ (FFU) kutokana na kudai haki yao ya msingi ya kupatiwa elimu.
Wakiwa katikati ya mateso hayo wanakukumbuka babu yao kwa kukuita jina nililokuwa napenda kukuita mimi rafiki yako Mchokonozi, jina la mchonga. Nadhani unalikumbuka.
Wakiwa katika hali hiyo huwa wanasikitisha sana, fikiria hata wale ambao hawakuwahi kukuona zaidi ya kusikia simulizi za jinsi ulivyokuwa ukiwapenda watanzania kwa moyo wako wote kiasi cha kujitolea maisha yako kuwaongoza kuishi maisha ya utu na si ya kinyama jina lako haliwatoki mdomo.
Kila wanapokong’otwa na matarishi wa watawala hawaishi kujutia kwa maneno ‘kama babu mchonga meno angekuwepo, haya yasingetukuta.’
 

Vurugu maandamano ya wanafunzi

Tena wakati mwingine huwa wanaimba kuwalaani watawala wa sasa uliotukataza kuwapa utawala. Wanawalaani kwa kuimba hivi ‘kama sio juhudi zako Nyerere, kama sio juhudi zako Nyerere, mafisadi mngesoma wapi?’
Itoshe tu katika hili kukufahamisha kuwa Tanzania yako ya sasa ina kizazi cha vijana wengi wasio kuwa na elimu bora. Ina lundo la vihiyo. Hawa ndiyo viongozi katika sekta nyingi nyeti. Ndiyo wanaoipeleka nchi shimoni.
Na katikati ya giza hilo la upofu wa elimu nchi imekumbwa na njaa kama nilivyodokeza hapo juu. Wakati wewe uliasisi kilimo cha kujitegemea wanzako huku wameasisi kilimo kwanza. Kilimo cha kufikirika, kilimo cha kuombea kura na kupitishia bajeti za ulaji wao. Najua unaelewa maana ya ninachokisema kwa sababu wewe ni mwelewa sana.
Ule uhuru ulioupigana unatimiza miaka 50 kesho kutwa lakini amini usiamini katika umri huo wa miaka 50 ya uahuru, watanzania hawana uhakika wa mlo wao wa siku, wanaamkia chai na kashata, wanashindia mihoga ya kuchoma kwa pilipili na wanalalia chai kwa maandazi.
Ardhi ya kulima ipo, mabwana shamba wapo lakini hakuna tena anayetaka kujishughulisha na kilimo. Wote wanataka kukaa mjini kwa sababu kilimo hakilipi. Kinacholipa ni siasa, ufisadi na ujanja ujanja.
Hivyo kwa sababu ya kukosa chakula tumebaki kuwa omba omba. Kila kukicha mkubwa wetu yuko safarini kwa wenzetu ambao ulipokuwepo tulikuwa tunalingana nao kwa uzalishaji wa chakula na hata bidhaa za viwandani kwenda kuomba misaada.
Anakwenda huko kuomba omba ili walau tuione kesho. Lakini uhakika wa kuiona wiki ijayo haupo ndiyo maana nikasema siku yoyote jiandae kutupokea huko uliko. Tutakuja tukiwa hoi kimwili, kiroho na kiakili, tofauti kabisa na ulivyotuacha.
Mwalimu, ingawa umri wa miaka 12 kwa watanzania wako ni mrefu sasa kutokana na ugumu wa maisha. Kwamba huku uswahilini kwa wachokonozi ukiishi umri huo unakuwa umeyaona mengi kiasi kwamba hata ukifa unakuwa na mengi ya kusimulia, hivi sasa umri huu tunaona mfupi mno. Tumebaki kujuta kwa kutenda uliyotukataza wakati ukiwa hai.
Na kwa salamu hizi, tambua kuwa hili ni ungamo tosha la kukiuka maagizo na maelezo yako ya kuwapa nchi wale uliotukataza kutokana na tamaa yetu ya kukubali kuuza kura zetu kwa rushwa ya sh 10,000,  fulana, tisheti, kanga na pilau.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya