Monday, December 23, 2024
spot_img

KWA SABABU YA UCHAGUZI 2010 MUNGU ATUJALIE MATESO NA KILIO


YAPATA miezi nane sasa tangu nilipowaonya wapiga kura wa Tanzania waliokuwa wakifurahia kupewa ubwabwa na maharage, khanga, tisheti na kofia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ili wawachague waliokuwa wakiwahonga kuwa si muda mrefu watakuwa wakinung’unika, wakilia na hata kufa kwa makosa yao wenyewe ya kutumia kura zao vibaya kwa kuchagua bora viongozi badala ya viongozi bora.

Katika makala ile niliandika kufafanua yale ambayo nilikuwa nikiyaandika katika mfululizo wa makala zangu za maswali elfu lela na moja kwa rafiki yangu Rais Jakaya Kikwete.
Ingawa niliandika kwa lugha nyepesi mno kueleweka ajabu alifeli yote kwa ujumla wake kwa sababu hakujibu hata moja.

Kama nilivyoandika miezi hiyo nane iliyopita, leo, ambapo watanzana wengi wapo katika mateso makali yanayosababishwa na ugumu wa maisha ninaandika tena maneno mapesi kabisa huku nikiepuka kugusia mambo mazito yanayoumiza mioyo kuwakumbusha wapiga kura wa Tanzania kuwa mateso watakayokutana nayo sasa wanayastahili kwa sababu ya uzuzu wao.

Tukubali au tukatae, watanzania wana kila sababu ya kuishi maisha magumu kwa sababu walikubali kuyauza maisha bora waliyokuwa wakiyachungulia kwa thamani ya ubwabwa na mahagare, khanga, tisheti, kofia na wakati mwingine kwa sh 5,000 au 10,000 baada ya kufanya kazi kubwa ya kuimba kwa sauti kubwa nyimbo za masifu kwa chama kinachowatesa sasa.

Ni wapiga kura hawa wanaolia kutokana na ugumu wa maisha ndiyo waliokuwa wakichukua shoka na mapanga kwenda kuwashambulia wenzao waliokuwa wakitaka kuking’oa mamdarakani chama kinachowatesa sasa kutokana na kukosa sifa zinazostahili za kuendelea kuiongoza nchi yetu. Wapuuzi wao na machozi yao.

Wamesahau kuwa kwa makusudi licha ya makala nyingi za upendo na zilizojaa maonyo nilizokuwa nikiwaandikia kuhusu kutokufanya kosa la kuchagua bora viongozi walinipuuza. Wakawachagua. Walifanya kosa la kukataa kuyakimbilia maisha yenye matumaini, sasa wanajuta.
Nami kwa nafsi nyeupe kabisa namsihi mwenyezi azidi kuwapa maisha magumu yenye kulia na kusaga meno.

Namuomba mwenyezi mungu anisamehe kwa kuwaombea maisha magumu na yenye kila aina ya suluba ndugu zangu ninaokula na kunywa nao kwa jasho la damu. Ninafanya hivi kwa sababu ninaamini ndiyo njia pekee ya kuwafundisha kufikiri sawasawa.
 
Ninaamini kuwa watakapokuwa wanakufa kwa kukosa huduma ya vidonge vya kutibu maralia katika hospitali zetu za umma huku hao waliowapa kura kwa kughilibiwa na vipande vya khanga na wali na maharage wakienda kutumbuliwa vipele Ujerumani na Amerika, ndipo watapojifunza maana ya kutumia kura zao vizuri kwa kukataa kurubuniwa kijinga.

Ni jambo la ajabu kwa watu walioishi chini ya mfumo wa uongozi wa chama kinachowatesa kwa takribani miaka 50 sasa, wanaojua jinsi chama hicho kilivyochoka na kinavyobaka demokrasia kuendelea kukikumbatia kwa kudanganywa kipuuzi kuwa, eti! Bila chama hicho Tanzania haitakalika.

Kwa watu wanaofikiri sawasawa ni jambo lisiloingia akili kukiingiza madarakani chama ambacho kinalundo la watu wasiokuwa na sifa za uongozi lakini wanaong’ang’ania madarakani kwa gharama kubwa ya fedha za umma.
Watu hawa, hata walipojifanya wamesahau walikumbushwa kwa lugha nyepesi kuwa ili kuifikia Tanzania yenye neema tunahitaji mabadiliko ya uongozi lakini ajabu waliziba pamba masikioni.

Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi wenye akili ambao walikuwa wakifuatilia mwenendo wa kampeni na hata uchaguzi wetu, wapiga kura wa Tanzania waliyakataa maisha bora wakachagua maisha magumu.
Leo hata kabla maisha hayajawakamata sawa sawa wameanza kupiga kelele za maisha magumu. Naiomba serikali isiwasikilize, izidi kuwahimiza wafunge mikanda kabla ya baa la njaa la kujitakia halijafika. Waanze sasa kuzoea maisha yenye ukakasi usiovumilika.

Ni watanzania wenzangu ambao wengi ninaishi nao huku uswahilini waliowabeza watumishi waliokuwa wakiomba kututumikia ili kwamba kutokana na utumishi wao kwa taifa letu, siku moja watoto wetu waweze kusoma bure.
 
Leo ninapowatizama, wakiwa wanahimizwa na serikali iwakopeshe hela za kuchapishia mitihani na ripoti za mitihani ya watoto wao, nawaona wana sura za majuto.
Wanasononeshwa na serikali waliyoichagua wenyewe miezi michche iliyopita kuishiwa hela za kusomeshea watoto wao na kubakiza hela za posho za semina, kuketi bungeni na chai na vitafunwa kwa wakubwa wanapotembelewa na wakubwa wenzao wenye maisha bora.
Kwa yeyote asiyesadiki maandishi haya, aje huku uswahili kwa wachokonozi asikilize wanavyolia kwa uchungu kutokana na kupanda kwa bei ya umeme ambao haupatikani.
Wapo ambao wameshaanza kununua vibatari kwa sababu kulingana na kipato chao hawataweza kumudu gharama za umeme. Wameamua kurudi kuishi maisha ya enzi za ujima katika karne hii ya 21 ya sayansi na teknolojia, tena wakiwa wanakaribia kabisa kuazimisha miaka 50 ya uhuru wao.
Katika hali halisi ya maisha ya mtanzania kwa sasa, pambio la maisha bora kwa kila mtanzania yanawezekana ni upuuzi na linatia hasira. Lakini acha kibwagizo chake kiendelee kujirudia masikioni mwa watanzania ili kiwaongoze katika majuto ya kweli.
 
Kilio kiko kila mahali kwani hata kwa wale wenye uwezo wa kujikamua na kulipa gharama za umeme, umekuwa lulu, unapatikana kwa mgawo na katika sehemu nyingi za uswahili unapatikana usiku.

Mchana shughuli zote zinalala, watu wanashinda wanapiga soga nje ya ofisi zao. Matumaini ya kutekelezwa kwa ahadi lukuki za kusambaza umeme sehemu mbalimbali nchini yameyeyuka, yamebaki majuto ya kukosekana kwa umeme na ukali wa mgawo wa umeme.

Majuto haya yanastahili kutokea kwa watu wanaojuta kwa makosa yao ya kuendekeza uroho wa ubwabwa na maharage na kutelekeza haki yao ya msingi ya kutochagua majuto.

 
Ngelleja
Ninapotafakari sana nikiwa katikati ya lundo la watanzania maskini wanaolizwa na kauli ya William Ngeleja, waziri kijana wa Wizara ya Nishati na Madini, ambaye siku chache baada ya kuteuliwa aliwaambia watanzania kuwa tatizo la umeme limefikia kikomo, ninaziona mbongo dhaifu za wazee na watu kadhaa wa umri wa makamo zisizokuwa na uwezo wa kifikiri kama walionao vijana wa sasa.

Katikati ya lundo hili la maskini wa kitanzania walio katika majuto baada ya kuyatelekeza matumaini, wanaolia wengi ni wazee na watu wa rika linalokimbilia uzeeni. Wanalalamika kuwa walidanganywa kuwa mambo yatakuwa mazuri baada ya uchaguzi na wakapewa mifano ya jinsi vigogo kadhaa walivyofikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali za ulafi.

Kutoka huko kwa vigogo wanaokabiliwa na tuhuma za ulafi wakageuzwa upande wa pili na kuonyeshwa sinema kadhaa za bunge zilivyokuwa zikichezwa. 
Rambo
Wakaonyeshwa tamthilia ‘feki’ ya Dowans ambayo waigizaji wake wakuu sasa wanafahamika dunia kote kwa umaarufu walionao kama wanavyofahamika akina na Rambo na Van Damme na wakati wakiangalia tamthilia hizo hawakukosa viburudisho vya khanga, fulana, kofia na ubwabwa na maharage vilivyoiharibu kabisa akili yao.
Van Damme

Siku chache baada ya wapigakura kulipa fadhila kwa waliokuwa wakiwahonga khanga hizo kwa kuwapigia kura ya ndiyo, tamthilia ya kweli ya Dowans imeingia Tanzania, hii inaonyesha jinsi watanzania watakavyokamuliwa jasho laokulilipa dude tulilosadikishwa na serikali kuwa ni ‘zimwi.’

Na ukitaka kujua mbivu na mbichi za chama cha maulaji angali tamthilia hizi mbili za Dowans, hii iliyochezwa bungeni na iliyochezwa kwenye mahakama ya kimataifa huko kwa wenzetu walioendelea.
Ukitazama vizuri picha hizo ndiyo utajua kuwa bila kukiondoa chama cha maulaji madarakani, chama ambacho watu walioanza kuchoka kiumri wanaking’ang’ania sana, Tanzania italiwa na itakwisha.

Zinajieleza vizuri tu, ukiangalia waigizaji wetu wa hapa nyumbani waliokwenda kuisaka Dowans ughaibuni wanaeleza kuwa ni zimwi lisiloonekana hivyo hakuna haja ya kuendelea na mkataka nalo ikizingatiwa kwamba liliingia nchini na kuanza kufanya shughuli zake kinyemela.

Tena katika kunogesha igizo lao wakaenda mbali kiasi cha kumtisha mkuu wa kaya kuwa yakiyafumua yote waliyoyabaini kuhusu zimwi hilo basiserikali yake yote yaani na yeye akiwemo itaanguka, lakini kwa sababu wanampenda sana mengine yanayaficha.
Huko kwa wenzetu Dowans imethibitika kuwa ipo, sio zimwi, imekwenda mahakamani imeshinda kesi na sasa tunalazimika kuilipa. Matumaini tuliyopewa yameyeyuka, tunajuta kwa kuiamini tamthilia ya waigizaji wetu wa hapa bongo.

Ni lazima tulipe bila kujali kama tutashinda na njaa, tutakufa kwa kukosa fedha za kununulia dawa kutokana na makali ya kulipa deni hilo au tutashindwa hata kununua chaki za kufundishia watoto wetu huku uswahilini. Serikali na chama kinachotutawala ndiyo msimamo wao.
Jambo la msingi ambalo wapiga kura wa Tanzania wanapaswa kulifahamu ni kwamba hivi sasa wanalazimika kuishi maishi magumu kwa sababu chama chetu kiko katika mchakato wa kufidia kama sio kurejesha mabilioni ya fedha kiliyoyatumia kuwahonga wao ili wakichague.
Ni lazima wengi wetu tule mlo mmoja kwa siku au tulale na njaa kwa sababu tuna deni la kulipia gharama za mabango ya picha za mgombea urais wetu yaliyokuwa yamesambazwa nchi nzima wakati wa kampeni zake za kurejea madarakani.
Sote tunajua kuwa gharama hizi zilikuwa za lazima ili kumuwezesha kushinda na tunaopaswa kuzilipa ni sisi, hivyo asitokee wa kulalamika kwa sababu kinachotekea sasa binafsi niliwahi kuwadokeza Watanzania.

Kama kunamtu asiyejua hilo nikumbushe kuwa niliwahi kuhoji hivi; ‘rais aliyechaguliwa kwa kura nyingi na kukaa madarakani kwa miaka mitano, inakuwaje anahangaika kutumia mabilioni ya fedha ili kuwashawishi wapiga kura wamchague?

‘Fedha hizi wangepewa akina Nicholaus Mgaya si wangepunguza kupiga miayo ya njaa na kutishia kugoma kufanya kazi? Matumizi haya ya CCM kumnadi mgombea wao  kwa nchi maskini kama hii ambayo ina watu wanaoishi chini ya dola moja kwa siku sio ufisadi?’

Sasa ili haya yaweze kuthibitika, mwenendo wa maisha yetu ya kila siku utatuongoza kufika huko kwa kuyafuta matumaini ya maisha bora na kubaki tukijuta kwa kujikosesha kwa makusudi maisha bora katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya