Makinda |
LEO ni sikukuu ya maboksi (boxing day) watu wanapeana zawadi kwenye maboksi wakati wakiendelea kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu kristo, sikukuu kubwa kwa wakristu duniani kote.
Kwa sababu ya ukubwa wa sikukuu hii, ofisi nyingi hasa za serikali zimefungwa. Hakuna kazi, wafanyakazi wanapumzika. Miongoni mwao ni wafanyakazi wa Idara ya Mahakama kubwa ambako siku chache zilizopita niliwasilisha ‘chaji shiti’ namba moja ya mwaka ujao wa 2012 dhidi ya polisi.
Leo nilipaswa kuwasilisha ‘chaji shiti’ namba mbili ya mwaka 2012 dhidi ya polisi lakini kwa sababu mahakama kubwa haifanyi kazi nimeshindwa, nitafanya hivyo Alhamis ya Desemba 29, 2011.
Hata hivyo, ieleweke kuwa safu ya Mchokonozi haina sikukuu wala mapumziko, niko kazini na safu hii haiwezi kuacha kuchokonoa.
Ninarejea katika mjadala ambao bado unatokotoka lakini ulipozwa kidogo na hii kamata kamata inayofanywa na maafande dhidi ya waandishi wa habari.
Mjadala wa ongozeko la posho za wabunge na namna Spika anavyoshabikia zioongezwe.
Anne Semamba Makinda, Spika wa Bunge lililojichafua kwa ufisadi, anaweza kuwa kuwadi wa ufisadi? Hivyo ndivyo nimekuwa nikijiuliza kwa siku kadhaa sasa.
Kwa nini nimekuwa najiuliza hivyo! Moja; jitihada zake za kuusadikisha umma kuwa yeye sio fisadi.
Historia isiyotunzwa katika vitabu vya historia ya mafanikio ya wakubwa wa taifa letu inaonyesha kuwa Spika Makinda ndiye Spika wa kwanza katika taifa letu aliyetajwa kufanikiwa kuupata wadhfa huo kutokana na kubebwa na mafisadi.
Kwenye wenye kumbukumbu zilizo na mashaka, napenda kuwakumbusha kuwa kabla kidogo na baada ya kuukwaa uspika, kulikuwa na tetesi kuwa aliandaliwa kuwa Spika na kundi la watuhumiwa wa ufisadi.
Kisa! ni vita iliyokuwapo wakati huo na inayoendelea hadi sasa baina ya kundi la wanasiasa wanaojitambulisha kuwa ni wapambanaji wa ufisadi dhidi ya wale wanaodaiwa kuwa ni mafisadi.
Iko wazi kuwa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta na timu yake ambao wako katika kundi la wapambanaji wa ufisadi walikuwa katika vita kali na kundi walilokuwa wakilituhumu kuwa ni mafisadi na kwamba lilikuwa likiwaandama ili kuwanyamazisha wasiendeleze jitihada za kupambana na ufisadi.
Hivyo basi, Sitta baada ya kuenguliwa katika kuwania uspika kwa kipindi cha pili kwa kile kinachoelezwa hadi sasa kuwa ni geresha ya kutoa nafasi kwa wanawake kuongoza muhimili huo muhimu kwa dola, kelele nyingi zilipigwa kuwa alienguliwa kwa nguvu za mafisadi ambao waliweka mtu wao, yaani Anne Makinda.
Ili kulainisha madai hayo, Spika Makinda, muda mfupi baada ya kuapishwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alilazimika kujitetea kuwa yeye si muumini wa ufisadi na kamwe hakupachikwa kwenye wadhfa huo na mafisadi.
Lakini maswali muhimu yaliyokosa majibu katika utetezi wake huo ni haya. Mosi, ni kwa nini aliamua kuwania nafasi ya bosi wake wakati akijua kuwa bosi wake huyo amekwishaonyesha nia ya kutaka kuendelea na ulaji wake na utamaduni wa chama alichomo ni kuachiana nafasi ikiwa mkubwa bado anautaka ukubwa?
Pili, inawezekana aliamua kumkomesha bosi wake kwa kumpoka wadhfa wake kutokana na hasira alizozitunza tangu siku ambayo bosi wake alipomshusha kuwa ana uwezo mdogo kwa kumzuia kusimamia mjadala wa kashfa ya Richmond uloikuwa ukiwahusu baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi? Na ni kwanini Sitta hakutaka Makinda asimamie mjadala huo? Alikuwa ana mashaka naye kuwa ana uhusiano nao?
Tatu, ni kweli kwamba mali zote alizonazo Makinda zinazotajwa tajwa sana hivi sasa huku uswahili, nyumba za ghorofa, shule zinazomilikuwa na ndugu zake. Hoteli kadhaa, kama kweli zipo alizipata kwa njia halali ikiwemo ya kukopa kama alivyowahi kusema? Mengine katika hili nayahifadhi.
Mbili; jitihada zake za kuhakikisha serikali haibanwi katika kashfa yoyote yenye harufu ya ufisadi.
Historia ya utendaji kazi wa Spika Makinda tangu alipochaguliwa kushika wadhfa huo ina viashiria vinanyoesha kuwa ni mfuasi wa ufisadi.
lema |
Hapo napo nina sababu kadhaa, ya kwanza. Mbunge wa Arusha mjini alipombana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni kuwa amesema uongo, Spika Makinda alikuja juu, akamkaripia Lema na kumtaka athibitishe kauli yake.
Lema naye, kwa mbwembwe za kijivuni akatoka akijigamba kuwa atathibitisha kauli yake, akawaahidi wananchi kupitia kwa waandishi wa habari kuwa atawasilisha ushahidi dhidi ya uongo wa Waziri Mkuu na akawataka waandishi siku atakapouwasilisha wambane Spika autangaze.
Alipouwasilisha, akarudi kwa waandishi wa habari kwa ujivuni ule ule akasema kazi tayari, kamwambieni Spika awaonyesha nilivyothibitha uongo wa Waziri Mkuu. Lakini Spika Makinda alipofuatwa na waandishi wa habari akaruka kihunzi. Sote tunajua kilichotokea na hadi leo amekalia uthibitisho huo wa Lema.
Kwetu sisi huu ni ufisadi, na hapa unaweza kutohoa kuwa ni ukuwadi wa ufisadi. Hii ni kwa sababu kuwadi kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Oxford, kuwadi ni mtu anayepeleka habari za siri kutoka kwa mtu fulani kwenda kwa mwingine.
Utohoaji huu unajengwa katika msingi mmoja kwamba inawezekana kuna uswahiba baina ya Spika na Waziri Mkuu, nadhani niko sahihi. Mawazo haya yanajengeka akili mwangu kutokana na jinsi Spika Makinda alivyomjia juu Lema baada ya kumtuhuma Waziri Mkuu kusema uongo na alipowasilisha uthibitisho wa uongo huo Spika Makinda hakuwa tayari kuutoa bungeni.
Sasa hapa inawezekana Spika Makinda aliuchukua uthibitisho wa Lema akampelekea Waziri Mkuu na labda wakabainika kuwa kweli yule mkubwa pale alidanganya. Wakaamua kufunika kombe mwanaharamu apite. Hapa ndipo msingi wa dhana kuwa inawezekana Spika Makinda ni kuwadi wa ufisadi unapojengeka. Kama siyo vivyo, iweje hadi leo jambo hilo limefumbiwa macho?
Mizengo Pinda |
Kumtuhumu Waziri Mkuu kwa uongo ni jambo kubwa mno, kwa Waziri Mkuu mwenyewe, Spika, Serikali na wananchi wote. Kwa sababu ya ukubwa wa jambo hilo, si rahisi kwa Spika aliyekuwa na nia ya kumsafisha Waziri Mkuu kukaa kimya. Hivyo kuwaza hapa kuwa kuna harufu ya ukuwadi, katika mazingira kama haya, nadhani siyo dhambi.
Tuendelee; turudi kwenye issue ya Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Huyu naye alikwishawahi kulituhumu Baraza la Mawaziri kwa ufisadi, kwamba lilihongwa na tuhuma hiyo aliitoa bungeni. Nani alilihonga na kwa nini, huko sitaki kwenda.
Tuhuma za kuhongwa zinatosha mno kuonyesha uzito wa ninachokiandika hapa, tena zikiwa zimetolewa na Mbunge ndani ya kikao cha Bunge.
Spika Makinda alimtaka Zitto kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo, Zitto akaahidi kufanya hivyo, haijalishi kama aliomba aongezewe muda wa kuwasilisha ushahidi wa kutolewa kwa hongo hiyo au lah. Lakini ninachoamini ni kwamba alishawasilisha ushahidi wake kwa sababu muda aliopewa na Spika kufanya hivyo ulishapita siku nyingi.
Hadi leo hatujasikia tamko la Spika Makinda kuhusu baraza la mawaziri kuhongwa na Zitto kama alikwishawasilisha ushahidi wake na ukabainika kuwa ni kweli au wa uongo.
Zitto |
Baraza la mawaziri ndiyo serikali, linapotuhumiwa kuhongwa sisi waumini wa kweli wa Mwalimu Julius Nyerere hatulielewi! Na hii ni kwa sababu kwetu sisi, serikali yetu inayotuongoza kuwekwa mfukoni mwa mtu mmoja ni moja ya maajabu ya dunia.
Ni ajabu kwa sababu mtu huyu, anayeweza kuhonga serikali yenye mawaziri zaidi ya hamsini, ukiwajumlisha na rafiki yangu Rais Jakaya Kikwete, makamu wake, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu, na jinsi walivyo na matumizi yenye kufuru, mtu huyo mwenye uwezo wa kutoa hongo kwa serikali hii lazima awe na mfuko mkubwa kweli kweli.
Lakini inawezekana hapo napo Spika Makinda alifanya kazi ya ukuwadi. Kwamba baada ya Zitto kuwasilisha vithibitisho vyake kuhusu kuhongwa kwa mawaziri wetu, Spika alivipitia na kubaini kuwa vina ukweli, akavibeba kwa siri akawapelekea mawaziri ambao walipoviona na kubaini jinsi watakavyoumbuliwa iwapo vitawekwa hadharani ndani ya ukumbi wa Bunge wakamtaka avifiche. Kama hivyo ndivyo, ndiyo maana hadi leo amevikalia. Huu ni ukuwadi.
Sababu nyingine inayonifanya nijiulize kama Spika Makinda ni kuwadi wa mafisadi ni hii hatua yake ya kushikia bango nyongeza ya posho za wabunge kuketi kitini.
Katika hili, swali la msingi ninalojiuliza ni moja tu. Kwamba, kwanini Spika Makinda anashabakia sana maisha ya anasa kwa baadhi ya watu walio na maisha bora tayari ndani ya watu wanaozungukwa na umaskini wa kutupwa.
Spika wa watu masikini anayeujua vizuri umasikini wa watu wake anawezaje kuwa shabiki katika hili kama hajatumwa na mafisadi wasio na uchungu na fedha za umma wala maisha ya watanzania kuwanyang’anya kidogo walichonacho na kuwaongezea ambao tayari wanacho kingi?