Monday, December 23, 2024
spot_img

RAIS KIKWETE, HISTORIA ITATUHUKUMU (1)

 
 

Kikwete



RAFIKI yangu Rais Jakaya Kikwete, siku nyingi zijazo baada ya kufa kwetu historia itatuhukumu.

 Wakati huo utakapofika, natabiri miaka alfu lela na moja ijayo, wajukuu wa wajukuu wa wajukuu zetu, watapokuwa wakisoma maandishi ya kichokonozi ya safu zenye akili za aina ya Mchokonozi, nikizitaja kwa uchache pamoja na Mchokonozi; Tuendako, Wazo Jepesi, Maswali Magumu, Usn’zibe Mdomo, Fikra zangu na Mtegemea Nundu ambazo nina hakika zitadumu na kudumu katika mioyo ya vizazi vingi vijavyo, watakuwa wakitoa hukumu dhidi yetu kulingana na maandishi, maneno na matendo yetu ya sasa.

 Kwa kuongozwa na maandishi hayo ya kichokonozi, wajukuu zetu hao, katika ulimwengu wao wa wakati huo watakao kuwa wakiishi, ambao nimekuwa nikiuota mara kadhaa katika ndoto zangu za kichokonozi kuwa utakuwa bora mno kuliko huu wa sasa. Ambao hata hivyo utapatikana baada ya mateso na machungu mengi, wakiwa wanasoma, watakuwa wanasema;

‘Hakika dunia ya wakati ule, miaka mingi iliyopita, baba wa babu zetu waliishi na wachokonozi waliokuwa na fikra pevu.

 Walisoma maandishi yenye kufikirisha ya rafiki mwema wa watawala aliyekuwa akizungumza nao kwa upendo wa kichokonozi kuhusu mwenendo wa utawala wao, lakini kwa sababu ya kiburi cha kijivuni cha watawala hao, hawakumsikiliza jambo lililosababisha anguko lao lililozaa vuguvugu la mapinduzi ya uongozi wa kufikirika yaliyozaa ulimwengu wetu wa sasa.

Na pengine, kama ninavyowaota kwenye ndoto, watakuwa wakisema; nchi yetu ya Tanzania miaka mingi iliyopita ilikuwa sawa na paradiso, lakini kwa sababu ya ujinga wa watawala waliigeuza ikawa sawa na kuzimu. Wanastahili laana kwa uongozi wao wa kipuuzi, uliojaa tamaa, ubinafsi na kila aina ya mbwembwe za kijuha.

Watakaokuwa wakijisema hivyo ni wale wataokuwa wakisoma maandishi yatakayokuwa yametunzwa katika vitabu vya historia ya mapinduzi mapesi ya Tanzania ninayoyafikiria kutokea hivi karibuni.

Watakuwa wakisoma kwa mshangao jinsi wachambuzi wa wakati tulionao sasa walivyokuwa wakiisaidia serikali ya CCM kuona ilivyoshindwa kuongoza nchi, jinsi ilivyogeuka kutoka katika misingi yake ya awali ya kuanzishwa kwake ya chama cha wakulima na wafanyakazi na kujigeuza kuwa chama cha wafanyabiashara walafi na ‘misheni town.’

Wanasiasa wa sasa na hasa rafiki yangu rais Kikwete, atakuwa maarufu sana katika vitabu vya historia ya siasa miaka hiyo mingi ijayo. Wengi watakuwa wakimsoma jinsi alivyoiongoza Tanzaniakuelekea katika anguko la kiuchumi na utawala wa kidemokrasia.

Watakuwa wakifurahishwa na maandishi ya kichokonozi kuwa enzi hizo, Mwenyekiti wa CCM, rais Kikwete, huku akijua kuwa chama anachokiongoza kinaporomoka kutoka katika umaarufu wake kiliojengewa na walio kiasisi alikiacha kiporomoke hadi kianguke ili chama cha upinzani chenye nguvu kiweze kushika hatamu za uongozi kwa sababu ambazo wachambuzi wa siasa za Tanzania wa wakati huo wataamini kuwa alijua hakina tena uwezo wa kuendelea kuongoza.

Hapo rafiki yangu Kikwete atakuwa akipongezwa. Historia itakuwa inamsifia kwa ujasiri wa kukiongoza chama chake kufa. Wajukuu wa wajukuu zake watakuwa wakijipiga kifua kulionea fahari jina lake kutokana na ujasiri wake wa kushiriki kuua kilicho chake kwa faida ya watanzania.

Watakuwa wakisoma safu ya Mchokonozi katika vitabu vilivyochakaa vya historia ya kale katika madarasa ya wakati huo kuwa; alikuwa na kila sababu ya kukiacha kife kwa sababu alikosea kuchagua wasaidizi wake wa kuongoza naye serikali baada tu kuukwaa ukubwa wa Tanzania.

Wa kwanza atakayekuwa akitajwa kuwa rafiki yangu rais Kikwete alimteua kutawala naye kimakosa ni Kapteni Edward Lowassa, ambaye si vibaya kama itakuwa imeandikwa kuwa alikuwa kilanja mkuu wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na rafiki yangu rais Kikwete ambaye pia alikuwa rafiki yake.

Na haina shaka kwamba kumbukumbu zitakazokuwepo, zitakuwa zikionyesha kuwa rais Kikwete ndiye rais wa kwanza wa Tanzaniaambaye serikali yake ilitikiswa na Bunge hadi akalazimika kuivunja.

Kwamba ndiye rais wa kwanza ambaye Bunge lilimchunguza na kugundua madudu fulani kwake lakini kwa sababu ya ukubwa aliokuwa nao likamfichia siri.

Na kwa sababu historia hunakiri zaidi mambo ya kuhuzunisha, ninashawishika kuamini kuwa itakuwa ikieleza jinsi watu waliokuwa karibu na Kapteni Lowassa walivyohuzunishwa na anguko lake.

Lowassa

Katika hilo, mkewe, Regina atakuwa akitolewa mfano wa jinsi alivyobubujikwa machozi wakati mumewe akitangaza kujiuzulu.
 

Maandishi yatakayokuwepo katika historia hiyo ya kale yatakariri baadhi ya maneno ya uchungu aliyoyamtaka Kapteni Lowassa wakati akijuzulu, kwamba; uwaziri mkuu ndiyo uliomponza…. Alifadhaika sana, alidharirishwa sana na kuonewa, …kwa mapenzi ya chama chake na serikali aliyokuwa akiitumikia, si nchi yake, akaamua kuuachia uwaziri mkuu.
 
Kwa sababu historia ni somo, wanafunzi watakao kuwa wakisoma somo la historia za viongozi wa Tanzania kwa kuchambua ubora wao wa kiuongozi. Watakuwa na mengi ya kujiuliza kuhusu Kapteni Lowassa na rais Kikwete.
 
Watakuwa wakichambua mwenendo wa maisha ya Kapteni Lowassa tangu alipozaliwa, elimu yake, utumishi wake serikalini na katika chama na makando kando yake mengine.

Na katika uchambuzi huo kwa sababu maandishi yapo na nina hakika yatadumu, watagundua kuwa Kapteni Lowassa alikataliwa kuwa kiongozi na Baba wa Taifa ambaye wao watakuwa wakimuita babu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 Kwa wenye kufikiri sawasawa, watakuwa wakishangazwa na uamuzi wa rais Kikwete kumkweza Kapteni Lowassa hadi kwenye uwaziri mkuu huku akijua kuwa mzee mchonga alimkataa.

Historia huzungumzia mambo ya kale hivyo ni wazi kuwa watakaokuwa wakizungumzwa na historia wakati huo watakuwa hawapo. Kwa vijana wa wakati huo hawatakuwa na woga wa kumkosoa rais Kikwete kwa sababu hatakuwepo.

Wanafunzi wa mchepuo wa sanaa ambao somo la historia lazima watakuwa wakilisoma kwa bidii, watakuwa wakijiuliza ni kwa namna gani mtu aliyechunguzwa na Bunge na kutiwa hatiani, Bunge hilo likamtaka apime mwenyewe kama anastahili kuendelea kuwa mkubwa au hapana!

Naye kwa busara zake akaona hastahili, akaachia ngazi kwa hiari yake kwa sababu ya kujiaminisha kuwa hastahili kutokana na kashfa aliyohusishwa nayo.

 
Si gele ya uwaziri mkuu kama alivyokuwa akisononeka siku alipodharirika sana kwa sababu kama angekuwa anastahili asingeachia ngazi.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya