![]() |
Mbatia |
Nimeanza kwa kuukiri ukweli huu kwa sababu wahenga wana msemo wao usemao “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.” Hivyo pamoja na ukweli kwamba sasa anaonekana kupwaya katika nafasi nyeti aliyonayo ya kiongozi wa chama cha upinzani.
Ninamfahamu Mbatia tangu mwanzo wa harakati zake miaka ya 1991 katika kambi ya upinzani. Nilimfahamu na niliendelea kumfahamu hata alipofanikiwa kuingia bungeni na baadaye alipoukosa mwaka 2000. Lakini katika kipindi chote hicho sikupata kufikiri kuwa atakuja gharimu muda wangu kumjadili hasa kwa mambo ya hovyo.
Sikupata kufikiri hivyo kwa sababu mwanzoni mwa harakati zake alijipambanua kamakijana mweledi na mpigania haki wa kweli miongoni mwa vijana. Alikuwa na misimamo isiyoyumba na alifanikiwa kujenga imani kubwa miongoni mwa vijana wenzake na hata kwa watu wazima.
Lakini ni bahati mbaya sana baada ya kushindwa ubunge mwaka 2000 na chama kuanza kupita kwenye wakati mgumu wa kufanya siasa katika mazingira ya ukata, ndipo nilipoanza kuushuhudia upopo wa kisiasa wa Mbatia.
Ni kipindi hicho, ndipo alipoanza kuwa mwanasiasa mwenye kutumia akili sana katika kushabikia na kushadadia watalawa na wenye fedha. Staili aliyoitumia katika kutekeleza hilo ni kujifanya mtaifa aliyepitiliza na mwanasiasa asiyefungamana na siasa kali.
Kwa wenye akili, wanajua kuwa ukiona mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa na msimamo thabiti wa mwelekeo wa kimapinduzi anaanza kucheza na maneno ya utaifa huku akipunguza hasira za raia waliochoka na kukata tamaa, mwanasiasa huyo anakuwa mfu.
Ili kuondoa dhana inayoweza kujengeka miongoni mwa mashabiki wake kuwa ninamuweka katika kundi la wanasiasa mfu wa kambi ya upinzani kwa sababu binafsi ninataja sababu za kuamini kuwa kwa sasa ni mwanasiasa mfu.
Akiwa mmoja wa viongozi wa chama cha upinzani ambao kazi yao kubwa ni kuwaongoza wafuasi wao kukiondoa chama tawala madarakani, aliibuka na hoja kwamba kutomtambua rais aliyetangazwa na Tume ya uchaguzi ni uhaini kikatiba.
Kwangu mimi, hilo lilikuwa doa jeusi la kwanza kwa Mbatia. Nilianza kupata shaka na mwenendo wake kisiasa.
Maswali haya yanajengwa katika ukweli kwamba Mbatia kama mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alikuwa anajua fika kuwa chama chake hakikuwepo Zanzibar hivyo hakikuwa na wagombea. Hakikuwa na cha kupoteza badala yake kama ilivyo ada kilipaswa kuwaunga mkono CUF. Ajabu kikawapinga. Kwa maana nyingine kilitaka chama tawala kiendelee kutawala.
Historia iko wazi katika hili, kuwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini Zanzibar ina vyama viwili tu vinavyoshindana kuchukua dola, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CUF.
Vyama vingine vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP, JAHAZI, nk, viko Zanzibarkutokana na masharti ya muungano tu.
Na katika uchaguzi huo, Mbatia na chama chake hawakuvuna kitu kutokana na uamuzi wao wa ukibaraka? Lakini anayepaswa kulaumiwa katika hiloni Mbatia.
Leo hii, ninapowasikia vijana wapambanaji katika kambi ya upinzani kupitia CUF wakimtaja Mbatia kuwa Mwenyekiti wa CCM ingawa hawafafanui ninaamini kuwa wanampa cheo hicho kwa sababu wanamuona si mwenzao katika kambi ya upinzani, bali ni pandikizi wa CCM katika upinzani.
Mbatia mwenyewe, naamini kwa sababu ya kuisha na pengine kwa sababu anafahamu kuwa kinachosemwa ni kweli hajajitokeza kukanusha kauli hiyo. Tunachopaswa kujiuliza wachokonozi kutokana na kauli hiyo ya wanaCUF ni kwamba Mbatia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa gani? au Wilaya gani? au Tawi gani? au ni kweli kwamba NCCR Mageuzi ni tawi la CCM?
Kwa sababu hiyo, nikitambua kuwa NCCR-Mageuzi ni chama cha upinzani, sikushangaa niliposikia kauli ya wazee wa chama hicho ya kumtaka Mbatia apumzike. Kwangu niliona huo ni mwanzo wa ufufuko wa chama hicho.
Niliamini hivyo kwa sababu ninakubaliana nao kuwa Mbatia anapaswa kuondoka sasa katika wadhfa wa uenyekiti kwa hiari yake au kwa kulazimishwa, ninaamini hivi kutokana na imani nyingine niliyo nayo kuwa kiwango ambacho watawala wamemtumia Mbatia kimempausha kisiasa, kimemfanya asitamanike tena miongoni mwa wanamageuzi.
Kauli za namna hii ndiyo zimewafikisha Watanzania kwenye kupoteza imani dhidi ya Mbatia na chama chake. Ni mwenendo wa namna hii uliosababisha apoteze imani kwa wanamageuzi wenzake nchini.
Huo ndiyo msingi wa kushindwa kwake kila anapogombea tangu awe mwenyekiti anashindwa. Watu wake wana imani na upinzani lakini hawana imani na yeye kwa sababu ya upopo wake kisiasa.