Monday, December 23, 2024
spot_img

AKILI YA RAIS KIKWETE CHANGANYA ZA MBAYUWAYU

 
 
Kikwete
RAFIKI yangu Rais Jakaya Kikwete ndiye kiongozi mkuu wa kaya yetu. Tunayatambua mamlaka aliyonayo, hatuna shaka hata kidogo na uelewa wake wa mambo hivyo tunapaswa kumsikiliza na kufuata ushauri anaotupatia.
Kwa kulitambua hilo, ni mawazo yangu kuwa ushauri uliopata kuutoa mara kadhaa akiwaasa watanzania kupima kwa usahihi mawazo au ushauri wanaopatiwa na kisha wauchanganye na akili za Mbayuwayu ili kupata uamuzi sahihi, haupaswi kupuuzwa kwa namna yoyote ile.
Tunapoenenda katika ushauri huu wa Kikwete, tunapaswa kuanza kwa kuchambua kauli zake ambazo hupasishwa na akili yake kisha tuzichanganye na akili za Mbayuwayu ili tufikie maamuzi sahihi.
Kwa wakati huu tuliona nao sasa, tuanze na hotuba aliyoitoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba alipopigia debe mfumo wa muundo wa Serikali mbili ambao hata Mchokonozi ni muumini wake; na kwa namna nzuri ya kuumba maneno, huku akijua kuwa kwa mamlaka aliyonayo anazungumza kupendekeza aina ya Katiba anayoitaka yeye, aliwaasa wajumbe kile ambacho wataona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa kwenye Rasimu wasisite kufanya hivyo.
Tukubaliane mapema hapa kwamba katika hotuba ile, kila mjumbe awe na dhana kichwani mwake kuwa rafiki yangu rais Kikwete alikuwa akieleza mambo ambayo hakuwa ameyafanyia utafiti na kama alifanya, utafiti wake ulikuwa mwepesi kwa sababu unapingana na hali halisi tuliyonayo sasa.
Hivyo basi, wajumbe wanapaswa kutafakari kwa kina alichokisema na kuichambua hotuba hiyo neno kwa neno, kila mmoja kwa wakati wake na nadhani mahali pazuri ni kwenye vyumba vyao vya kulala kwa sababu bungeni imekataliwa.
Wajumbe watafakari kwa kina kauli ya Kikwete kuwa baadhi ya mambo yaliyo kwenye rasimu ni mazuri na yanavutia lakini lazima yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili kwa sababu ipo hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa au kushtakiwa kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo.
Kila mjumbe aitafakari vizuri kauli hii kwa sababu inaonyesha woga wa serikali kulazimishwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi. Inafahamika Serikali inao uwezo wa kiuchumi wa kutekeleza wajibu wake kwa wananchi lakini inakwazwa na ufisadi uliopitiliza wa baadhi ya watendaji. Inashindwa kufanya hivyo.
Anajua Kikwete kuwa watanzania wakipata mwamko wa kwenda mahakamani kudai haki zao za msingi watazipata kwa sababu serikali inao uwezo wa kuwapatia. Imekwishashtakiwa mara kadhaa na kulipa fidia ya mabilioni kwa baadhi ya mambo iliyoyafanya ndivyo sivyo.
Ikiwa hivyo itabidi ijirekebishe kwa kuacha kucheza na haki za msingi za raia, vinginevyo italazimishwa kuachia ngazi. Hili siyo jambo jema kwa serikali na ni lazima ilikatae. Ndivyo alivyofanya rais Kikwete.
Wajumbe wanapochambua hotuba ya Kikwete, wakiongozwa na akili za Mbayuwayu waiangalie kwa umakini Ibara ya 128 (2) (d) aliyoeleza kuwa inaleta dhana ya mbunge kupoteza ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za kibunge kwa miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza.
Wasome neno kwa neno kuwa mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo, eti! kwa mujibu wa Kikwete, ni maoni ya watu wengi kuwa ni ukatili ambao haustahili kufanywa na Katiba. Watafakari kwa kina mbunge anayeugua kwa kipindi kirefu akiwa hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake anapaswa kupumzishwa au lah!
Wasiishie hapo, wajiulize, wafanyakazi wa sekta nyingine wanapougua kwa muda mrefu wakiwa kazini wanatendewa vipi? Huachwa kwenye nafasi zao muda wote mpaka wanapopona au lah?
Kama sivyo, kwanini iwe tofauti kwa wabunge? Kwa akili za Mbayuwayu wajiulize iwapo Kikwete anataka tuamini kuwa wabunge ndiyo wanaopaswa kutendewa kwa huruma lakini si watanzania wote?
Akili ya Kikwete inaamini kuwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa wabunge bila kueleza kama ni mfululizo au lah, nayo ina walakini! Yeye anaamini katika mazoea kuwa ukomo ni kwa wakuu wa nchi lakini kwa wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza kufanya hivyo.
Anaonyesha hofu ya kuinyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Wajumbe wachanganye mawazo haya yanayotokana na akili ya rais Kikwete na akili za Mbayuwayu.
Mbayuwayu
 
Kama Mbayuwayu, wajiulize ulevi wa madaraka wa baadhi ya wabunge wa sasa unasababishwa na nini? Wapime kama Tanzania ina uhaba wa watu wanaostahili kuwa wabunge isipokuwa baadhi ambao wakiondolewa kwa mujibu wa sheria itakayopitishwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Katika uchambuzi wao, muundo wa Muungano uliozungumzwa na rafiki yangu rais Kikwete waupe kipaumbele. Wapime wenyewe uzito wa hoja za Tume ya Jaji Joseph Warioba ambazo zinawiana kwa kiasi kikubwa na mapendekezo yaliyopata kutolewa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992, kundi la wabunge la G55 mwaka 1993 na Tume ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998 dhidi ya zile za Kikwete.
Wayachukue haya katika mizani ya ulinganifu kwa namna ya akili ya rais Kikwete dhidi ya akili za watu waliounda Tume ya Jaji Warioba, Tume Jaji Nyalali, Tume ya Jaji Kisanga na kundi la wabunge wa G55.
Watakafari kwa kina kauli ya Kikwete kuwa taarifa ya Tume imeonyesha kuwa watanzania waliotoa maoni yao kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664 na kati yao 47,820au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano.
Wajumbe Bunge la Katiba
 
Kwamba wananchi 303,844 sawa na asilimia 86.4 ndiyo ambao kwao muundo wa Muungano halikuwa tatizo hivyo hawakuuzungumzia kabisa. Kwa sababu hiyo wapo wanaohoji iweje asilimia 13.6 ya watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo walio wengi!
Wasiache kuangalia takwimu zilizotajwa na Kikwete kuwa katika ukurasa wa 66 na 67 wa rasimu, kati ya 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano ni 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa serikali tatu, asilimia 29.8 serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza serikali ya mkataba na asilimia 7.7walipendekeza serikali moja.
Eti kwa takwimu hizi, hoja ya watanzania wengi kutaka serikali tatu msingi wake ni upi?
Waperuzi pia takwimu za Tume, ukurasa wa 57 alizosema zinaonyesha Tume ilipokea maoni 772,211, kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine.
Warejee kauli ya Kikwete kuwa wapo wanaohoji kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa.
Wasisahau alichokisema kuwa waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4ya maoni yote hivyo wanauliza usahihi wa hoja ya watanzania wengi kutaka serikali tatu uko wapi?
Haya yote wayachanganye na akili za Mbayuwayu ambazo zitawasaidia namna sahihi ya kutafuta uwiano wa kitakwimu. Kwamba idadi ndogo ya watu haiwezi kubeba maoni ya watu wengine wengi ambao hawakutoa maoni yao.
Wauangalie mfumo mzima wa takwimu zinazotumiwa na taifa letu kuhalalisha mambo. Kwa mfano wa kasoro zilizotolewa na Kikwete kwenye takwimu za tume ya Warioba, wapime wenyewe kama kura alizopata rais Kikwete kama zinamuhalalisha kuwa mkuu wa nchi katika taifa lenye watu zaidi ya milioni 45.
Katika muundo wa Muungano, pamoja na mambo mengine mengi yaliyoelezwa na Kikwete wasiache kupitia kwa kina kauli yake kuwa muundo wa serikali tatu una gharama kubwa.
Waangalie kama muundo wa serikali mbili za sasa una ahueni katika uendeshaji wake. Warejee kwenye takwimu za mwenendo wa uchumi wa taifa kama unaridhisha, waangalie deni la taifa kama linazidi kupaa au linapungua kwa kiasi kikubwa, waangalie matumizi ya matanuzi ya wakubwa.
Wasiache kujiridhisha kama kweli mfumo wa sasa una ahueni kubwa ya gharama za uendeshaji. Wahakikishe akili za Mbayuwayu zinawaongoza ili kupata majibu sahihi.
Wachambue kwa kina kauli kwamba upo uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi washirika wa serikali ya Muungano na uwepo wa uwezekano mkubwa kwa muundo wa serikali tatu kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Swali la msingi katika tafakuri ya kauli hii liwe kama muundo wa serikali mbili za sasa hauna sera zinazokinzana au kutofautiana katika masuala ya msingi ya nchi ambayo yamezua mgogoro baina Zanzibar na Tanzania Bara.
Wasisahau pia kujiridhisha kama muundo wa sasa wa muungano hauleti tofauti kubwa za kimaendeleo baina pande mbili, kisa kikiwa kila upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Ingawa siyo jambo jema kutilia shaka maoni ya kisomo ya kiongozi msomi, kwa kile alichokisema Kikwete kuwa serikali ya shirikisho itakuwa haina chanzo cha uhakika cha mapato kinajenga uhalali wa kuwa na mashaka na hilo kwa sababu hata sasa hali ni shaghala baghala.
Kwa wajumbe shaka iwe kwenye muundo wa sasa za serikali kama ina chanzo cha uhakika cha mapato kama siyo vile vya kubangaiza.
Wapekue bajeti za serikali zinazowasilishwa na kupitishwa na Bunge waone kama chanzo cha uhakika cha mapato ya serikali ni kodi ya bia, soda, sigara, kadi za simu au kodi inayotokana na rasilimali adimu ambazo taifa limejaliwa kuwa nazo ambazo ni pamoja na  Dhahabu, Almas, Gesi na Mafuta?

Akili za Mbayuwayu ziwasukume kujiuliza kama vyanzo vya mapato vya sasa vya serikali vinaiwezesha kusimama yenyewe au inategemea misaada na kama inategemea misaada kuna dhambi gani kwa serikali ya shirikisho kujiendesha kwa kutegemea misaada?

Wajumbe wasipoteze muda wao kutafari kauli kuwa ipo hatari ya jeshi kuchukua madaraka kwa kutolipwa mishahara kwa sababu hata wananchi wanaweza kuipundia serikali kwa madai kama hayo.

Ushauri wa mwisho kwa wajumbe katika makala haya wapoteze muda mwingi kutumia hekima za Kikwete kwa kuchukua akili yake na kuichanganya na ya Mbayuwayu ili kutengeza Katiba Mpya iliyo bora.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya