Monday, December 23, 2024
spot_img

WANAKITA KIZULU, NINAKITA KISWANGLISH

Simba Gembagu Ngw’ana Njamiti
NIMEKUTANA wa Wazulu, nimekutana nao nchini kwao huku bondeni kwa mzee Madiba. Lakini mzee Madiba anaumwa sana, tumuombee.
Wazulu, kama walivyo waafrika wengine wana mbwembwe za kibantu asilia, wanapenda sana kujivunia vya kwao, wanajivunia uafrika wao, wanawadharau sana wakuja bila kujali kama ni  waafrika kama wao au lah.
Eti! Walifikia hatua ya kunidharau hata mimi mzee Mikito. Kila nilipojikita kukitukuza Kiswahili wao walijikita kwenye lugha yao ya Kizulu, wakanilazimisha kuongea Kiswanglish. Watu wa ajabu sana.
Hata hivyo, pamoja na katabia kao ka ujivuni ni watu wakarimu sana kwenye kinywaji. Wanaheshimu kinywaji nadhani kuliko kazi, hasa wanaoishi kwa kukitana.
Wakiwa katika vikao vya wanamikito, humkaribisha yeyote kujiunga nao. Lakini karibu yao ina walakini, ukijongea sharti ujinunulie bia mwenyewe. Hukuna cha bure huku.
Wiki iliyopita, nilikuwa nalanda landa katika vitongoji vya Soweto, nilikwenda kuweka kambi Zone Five ndani ya kilabu maarufu kinachoitwa ‘gogo store.’ kinapendelewa sana na waswihili wanaoishi eneo hilo.
Ilipotimu saa moja kamili usiku kwa majira ya huku, huko nyumbani saa mbili kamili wateja waswahili wawili waliomba kuangalia taarifa ya habari ya nyumbani Tanzania.
Dada muuzaji alikubali, akaweka ITV nikajiunga na wale waswahili wawili waliokuwa katikati ya kundi la vijana wa Kizulu kusikiliza taarifa ile.
Wazulu, wake kwa waume walitaka kutafasiriwa kinachoripotiwa. Mzee Mikito haraka nikajipa kazi ya ukalimani na niliifanya kwa usafaha.
Kizulu nilipata kijifunza enzi hizo katika masomo yangu ya elimu dunia.
Ghafla wakati taarifa ya habari inaendelea alionekana afande mkubwa, anaitwa Suleiman Kova, akiwashukuru wananchi wa Dar es Salaam kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa mapokezi ya Rais wa Marekani, Barack Obama.
Afande Kova
Ninamfahamu Kova ni mwanamikito wa Dar es Salaam, ni rafiki yangu sana huyu tangu tukiwa vijana kule mkoani Mwanza.
Niliamua kumfagilia rafiki yangu Afande Kova kwa wazulu kwa sababu najua anapenda kusifiwa. Siyo dhambi kusifiwa kwa sababu hayupo asiyependa sifa.
Nilianza kusifia mavazi yake ya rangi ya bluu aliyokuwa amevaa siku hiyo kama alivyoonekana kwenye televisheni.
Halafu nikaeleza jinsi jamaa alivyo mchapakazi. Nilijikita kutoa sifa hadi za uongo, nilipoona nakaribia kuishiwa nilijikita kueleza jinsi alivyojikita kusimamia fukuza fukuza ya wamachinga ili Obama atakapokuwa anapita asiwaone wanavyohangaika juani kutafuta ngama.
Dah! Nilidakwa mdomoni na Wazulu. Wa kwanza alipayuka, ‘eeei wena, foseki, nkuruma ini,’ akimaanisha ninazungumza nini.  Nikanyamaza. Yeye akasimama, akapayuka tena, ‘wena ntombi, nginigeze ebia, Heineken.’ Moyo ukatokota kwa hasira, nikajua jamaa kanitukana.
Waswahili wenzangu wakaniambia hajatukana, bali alikuwa anaagiza bia, eti! Ntombi ni msichana. Lugha ya ajabu kweli kweli.
Hakunijali, akajikita kutoa kauli za kumponda afande mkubwa Kova kwa kujikita kusimamia operesheni ondoa machinga,  alimponda vilivyo baba wa watu, eti! Kwa cheo chake, kwa jinsi alivyoonekana na magwanda yake, kusimamia fukuza fukuza ya machinga kunaashiria kwamba hana kazi ya kufanya. Aliniudhi kweli.
Kuepusha balaa, nikajikita kuzungumza Kiswanglish ambacho nilijua atakuwa anaelewa japo hivyo hivyo. Nikaanza kuelezea mipango ya mbeleni ya serikali ya kuhakikisha Dar es Salaam linakuwa jiji safi kuliko mengi barani Afrika na pilika pilika zinazoendelea sasa za ujenzi wa miundombinu na mambo mengine mengi.
Akanikata kauli tena, akarudi kule kule alikokuwa amejikita mwanzoni, akahoji, Dar es Salaam itakayokuwa safi ni ipi? Ni hiyo inayoonekana kwenye televisheni jinsi ilivyopangiliwa hovyo hovyo kuliko maeneo ya ushenzini ya Soweto au?
Hakunipa nafasi ya kuzungumza, akajikita kunieleza jinsi viongozi wa Tanzania wanavyofika Afrika Kusini mara nyingi na kuona miji ilivyojengwa, lakini wameshindwa kuiga walau robo ili kujenga huko nyumbani.
Kwa dharau ambayo siwezi kuieleza hapa kwa sababu najua nitawaliza wakubwa serikalini, akasema, Dar es Salaam ilipaswa kujengwa mithili ya New York ndani ya miaka kumi kama kungekuwa na viongozi wenye utashi wa kulitumikia taifa, lakini kwa hawa waliopo, hadi mwisho wa dunia itaendelea kuwa jiji la hovyo lisilotazamika machoni hata na watoto wanaoishi uswahili katika vitongoji vya Soweto.
Taka zilizotupwa ovyo jijini Dar es Salaam
Nilivuta picha Dar es Salaam na kuona jinsi ilivyo chafu nikaona jinsi waswahili wenzangu wanavyotupa maganda ya ndizi na machunga barabarani, nikaona msululu wa foleni barabarani, nikajiinamia kwa aibu.
Kama alivyofanya yeye na mimi kwa sauti ya kilevi nikapayuka, ‘wena ntombi, nginigeze ebiere, Castel,’ huku moyoni nikijiapiza kuufikisha ujumbe huu kwa afande mkubwa Kova na wenzake wanaohusika hata kama utawaudhi ili walau nao waone aibu kama hii iliyonikuta mimi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya