Saturday, May 31, 2025
spot_img

ANAKITWA ANAKITA KUJIKITA MZEE MIKITO

Simba Gembagu Ngw’ana Njamiti
KUKITWA ni kukitwa na kukita ni kukita. Kukita na kukitwa sasa ni fasheni, mikito imekuwa sehemu ya maisha.

Imekuwa kita nikukite, umekuwa mwendo wa mikito. Wakubwa kwa wadogo wanakitana kwa staili tofauti tofauti. Hayupo asiyejua kukitwa au kukita. Watanzania wamekuwa watu wa kukitana usiku na mchana.

Aliyekitwa safari hii ni mzee wa Mikito, amekitwa mkito dhaifu kwa nyuma kisha wakitaji wake wakatoka mbio kwa hofu ya kukitwa kwa mbele huku wakishangilia ukitaji wao dhaifu waliomkita mzee wa Mikito.

Waliomkita walimuwinda chamani kwao, wakamuweka kati, wakaanza kumkita pasipo kujikita kwenye hoja, kisa kawaanika hadharani wakati ni desturi ya chamani kutoanikana.

Kwa sauti za kukoroma zilizokuwa zikitoka kwenye midomo iliyoumbwa katikati ya sura zilizopauka, waliomkita walikoroma kwa kulalama kuwa amekiuka miiko ya chamani ya kufichiana siri.

Vikina mama vya chamani kwa wana mikito navyo havikubaki nyuma, viliachama midomo na kushupaa mishipa ya shingo vikijaribu kujenga hoja zisizojengeka kuwa, eti! Amevivua nguo kwa kutoa siri sirini.

Kwa umoja wao chamani wakaungana kumkita mzee wa Mikito, wakajikita katika kumsomea mashtaka ya uongo na kweli yaliyojikita kwenye uzushi, upotoshaji na uzandiki wa kusikitisha. Kisha wakamuhukumu hukumu ya kusimama.

Kama ilivyo desturi ya wana mikito, mzee wa kukitwa hakukubali kukitwa, akajikita kwenye utetezi alioujenga kwa hoja za nguvu zilizowatikisa wakitaji wake wakatikisika, wakajawa hofu kwa mitikisiko ya hoja zile.
Kujinusuru wasikitwe, wakaisimamia hukumu yao ya kusimama. Wakageuka wakukitwa.

Wahenga walisema, anayekubali kushindwa ni mshindani. Mzee Mikito kwa sababu ni mshindani akakubali kushindwa, akajisimamisha milele chamani kwa sababu hakuwa mmoja wao bali mtalii. Alikwenda chamani kutalii na kufaidi vinono vya kitalii. Basi!

Ajabu ni kwamba, mashabiki wa mikito baada ya kusikia mzee Mikito kahukumiwa hukumu ya kusimama chamani na yeye amejisimamisha milele walishangilia kwa nderemo na vifijo kuwa eti! mzee Mikito sasa amesimama na ataendelea kusimama kidete kuwakita wakukitwa ambao ni wakitaji wake.

Wana viherehere mashabiki wa wana mikito, wanapenda sana kushabikia kukitana. Hata kabla mzee Mikito hajajikita kuwakita wakitaji wake kwa hoja zenye mashiko, wenyewe wamejikita kukusanya taarifa zote za siri za wakitwaji, ili wampelekee kwa ahadi ya kuzitumia kuwakita wa kukitwa.

Wanakusanya mafaili na karatasi za wakitwaji waliojikita kulambalamba viatu vya wanasiasa vinavyosigina soli zenye siri ili zisagike na kutoweka milele.

Ukiwatizama walivyojikita kufanya kazi hiyo, utawaona wakiwa hawana tofauti na wanawake vizabizabina wa mwembe tongwa ambao kila wanalolinusa, wanalifikisha kwa mjumbe.

Upekupeku una wenyewe na wenyewe ndiyo hawa mashabiki wa mikito. Kwa upekupeku wao, sasa wanapekenyua kila droo ya wa kukitwa na kukusanya kila kilichomo wanakitia kwapani.

Wanazoa siri za chamani zinazoonyesha kuwa kile kinachoitwa chama siyo chama, bali ni utapeli wa Mtaa wa Kongo wa kuuziwa kipande cha simu kilichotengenezwa kwa kipande cha sabuni.

Kwa upekupeku wao, wamepekenyua hadi  wakagundua kuwa kinachoitwa chama ni  kijiwe cha wavimba matumbo wanaovimbiwa makomba ya mabwanyenye.

Hakuna kabati la wa kukitwa linaloachwa wazi, yote yanafunguliwa na kupigwa sachi kusaka vielelezo vilivyofichwa na matarishi wa wenye viliba tumbo ambayo yanaonyesha jinsi walivyo wanafiki na walivyoumbwa kwa roho za plastiki ambazo zikikutana na moto mkali kidogo zinayeyuka.

Kazi ya kuwakita wa kukitwa imerahisishwa na mashabiki wa mikito, mzee Mikito sasa anasubiriwa kujikita katika hoja zinazotikisa kuwakita waliomkita.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya