Monday, December 23, 2024
spot_img

TUTAKUMBUKWA KWA KIFUNGO CHA SIKU 90


Historia ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania, Afrika na ulimwengu kote haiwezi kusomeka kwa usahihi pasipo kuitaja Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Gazeti la Mtanzania toleo la siku ya Jumatano na safu ya Mchokonozi.
Kwa sababu hiyo, Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Gazeti la Mtanzania toleo la siku ya Jumatano na safu ya Mchokonozi vitakumbukwa duniani miaka mingi ijayo kwa sababu ya kufungwa kifungo cha siku 90 na serikali.
Hivi ndivyo imekuwa ikitokea duniani. Historia inaonyesha kuwa watu waliopata kufungwa au kushtakiwa kwa sababu ya kutetea ukweli, au taasisi iliyofungiwa kwa sababu ya kutekeleza majukumu yake kiufasaha hukumbukwa vizazi na vizazi kwa sababu ya machungu waliyoyakabili katika kifungo na hasa uamuzi wa kifungo unapokuwa umefikiwa katika mazingira yenye utata.  
Kifungo cha gazeti la Mtanzania ingawa kilikuwa na athari mbaya kwa watanzania wengi lakini kimesaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza Kampuni ya New Habari, gazeti lenyewe na safu ya Mchokonozi kwa watanzania, waafrika, waasia, wazungu na hata wale wasio kuwa na utaifa wa aina yoyote. 
Kimelisaidia gazeti la Mtanzania kujipambanua kwa walimwengu kuwa halifanyi kazi ajili ya maslahi ya mtu bali ya umma, kimeuthibitishia ulimwengu kuwa ni chombo cha habari kinachotimiza wajibu wake wa kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha kwa mujibu wa taratibu, kanuni na miiko ya kitaaluma bila kuangalia makunyanzi ya mdogo au mkubwa.
Wanataaluma wa kweli hawatalisahau hili.
Waliokuwa wakilitazama gazeti la Mtanzania kama kipeperushi cha kusambaza maneno ya watawala, kifungo cha siku 90 kimewaondoa kwenye mtizamo huo. Sasa wanalitizama gazeti hili kama moja ya vyombo vya habari huru, gazeti ambalo halifungamani na mtu au kikundi cha watu katika kutekeleza majukumu yake ya kihabari.
Watanzania wengi wanaotamani mabadiliko ya kiuongozi na kimfumo, wanaotamani uhuru wa habari na uhuru wa kutoa mawazo uheshimiwe na watawala na watawaliwa, wanaopinga sheria zote kandamizi ambazo jitihada za muda mrefu za kuziondoa hazijafanikiwa watalikumbuka gazeti la Mtanzania na safu ya Mchokonozi kwa kuongoza harakati za matamanio yao.
Ndani ya mioyo, siku 90 za kifungo zimekuwa za mateso ya kukosa habari, kukosa elimu na kukosa burudani. Watabaki wakikumbuka kuwa walipata kuteseka kwa miezi mitatu kwa kukosa haki yao ya kikatiba ya kupata habari.
Watawala wa sasa, waliohusika na hata wale ambao hawakutia mikono yao katika kuhukumu au kukazia hukumu ya siku 90 watalikumbuka gazeti la Mtanzania kuwa moja ya vyombo vya habari vilivyotekeleza majukumu yake ya kupasha habari, kuburudisha na kuelimisha kwa ustadi uliowatesa kwa sababu hawakupata kuuona hapo awali hivyo ulikuwa mgeni kwao.
Ndani ya mioyo yao watabaki na kumbukumbu mbaya ya kutumia sheria kandamizi kuhukumu magazeti. Wataishi maisha ya wasiwasi ya kuwa mfano wa watawala waliopata kuumiza wengine na watakuwa wakiwahofia watu walioumizwa kwa uamuzi wao.  
Viherehere na makuwadi wa wakubwa ambao hufanya waliyotumwa na wasiyotumwa bila kuangalia athari zake kwa lengo la kuwafurahisha wanaowatumikia na pia kuhalalisha ukiherehere na ukuwadi wao ambao haina shaka kuwa Mungu atawajalia maisha marefu ili waje waone madhara ya vitendo na maneno yao, kwa miaka mingi ijayo watakuwa wakiikumbuka safu ya  Mchokonozi kwa ubaya.
Haina shaka hata kidogo kuwa kuanzia sasa watakuwa wanawahi kununua nakala za gazeti hilo na kuisoma kwa umakini na utulivu safu ya Mchokonozi. Watakuwa wanasoma neno kwa neno, mstari hadi aya, wataangalia mpangilio wa koma, nukta, matumizi ya alama ya kuuliza na hata ile ya mshangao kwa lengo na kutafuta kosa la kulazimisha litakalohalalisha kuchukua hatua za kumfunga tena Mchokonozi.
Kwa lazima, itabidi wasome maandishi yanayofurahisha na kuburudisha yanaposomwa na wachokonozi lakini kwao, yanayoudhi na kukera kwa sababu huwafikirisha mambo ambayo hawapendi kuyafikiria, huwaonya na wakati wengine kuwakaripia wale waliojivika ubwana pasipo kuwa na sifa stahiki.
Wakubwa wanaoteswa na ukweli kwa sababu hawaupendi, gazeti la Mtanzania na safu ya Mchokonozi vitabaki katika kumbukumbu zao hata baada ya kuondoka katika ukubwa walionao sasa kwa jinsi walivyohangaika kulishughulikia na namna walivyoteswa na uamuzi wao wa kutoa adhabu kali ya kifungo. 
Popote walipo sasa na huko watakapokuwa baadaye, hawatamsahau Mchokonozi kwa sababu aliwachokonoa. Wakiwa nje ya ulingo wa utawala, watakuwa wanasoma maandishi ya kichokonozi yaliyojaa ukweli na ambayo yataendelea kuwepo miaka mingi na kukubali kuwa ndiyo ukweli ambao wanaupinga sasa kwa sababu ya woga, kiburi au upofu wa madaraka.
Ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, waandishi wa habari na wafanyakazi wengine wote, wao na familia zao, watakuwa wanakikumbuka kwa machungu kifungo cha siku 90 cha gazeti la Mtanzania jinsi kilivyowasababishia ugumu wa maisha. 
Watateswa kifikra kwa muda mrefu kwa namna walivyoathirika na hukumu ile.
Kwa waandishi wa habari chipukizi wa New Habari, watabaki na kumbukumbu ya kudumu ya jinsi kaka na dada zao katika fani ya uandishi wa habari walivyotofautiana kimtizamo na msimamo pasipo kupigana kuhusu utata wa kifungo hicho.
Bila shaka jina la Absalom Kibanda, Mhariri mwenye nguvu anayeteswa na maguvu ya Mchokonozi halitafutika katika kumbukumbu zao kwa jinsi alivyoumizwa na uamuzi wa wakubwa wa kulifungia gazeti la Mtanzania kwa taratibu ambazo si za kawaida na pili maandishi ya kichokonozi ambayo kwa kiwango kikubwa ndiyo yaliyotumiwa na wakubwa kuhukumu gazeti kifungo hicho.
Waandishi wa habari chipukizi waliopita katika mikono ya Mchokonozi na wale waliopata kuwa karibu naye kikazi, siku zote watakumbuka kuwa alikuwepo Mchokonozi ambaye jina lake lilikwezwa duniani na kifungo cha siku 90 kilichotolewa kwa sababu ya kutekeleza matakwa ya kazi yake kwa usahihi uliopitiliza.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya