NILIKUWA Dodoma mwezi uliopita, nilikuwa huko kwa zaidi ya wiki moja.
Nilikwenda kuhudhuria uzinduzi wa bunge la kumi na shughuli nyingine kadhaa za kitaifa ikiwemo kuidhinishwa na bunge kwa jina la Waziri Mkuu wa n’gwe ya pili ya serikali ya awamu ya nne baada ya kuteuliwa na rais.
Sambamba na shughuli hizo, nilikwenda kuburudika na watukufu wachache wa nchi hii. Nilikwenda kujumuika nao kula mapochopocho na kunywa mvinyo wa bei mbaya tukiwa katika mavazi nadhifu – suti – za bei mbaya na mkuki shingoni ambayo ni nadra sana kuvaliwa uswahili. Kilikuwa kipindi kifupi cha kuishi maisha bora.
Lakini pia sikusahau kufanya kazi yangu niipendayo ya kufuatilia mambo ya kipuuzi yanayofanywa na wakubwa waliokabidhiwa kazi nyeti za kuongoza baadhi ya ofisi za umma wa Watanzania.
Niliyaona mengi ambayo kwangu yalikuwa ya kipuuzi na nimerudi nayo, na bila kusita nitakuwa nikieleza moja baada ya jingine. Leo naanza na hili la mtumishi kiongozi wa idara wa habari, maelezo. Anaitwa Clement Mshana.
Ilikuwa hivi. Siku ya kuapishwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, shughuli ambayo iliyofanyikia Ikulu ndogo ya Chamwino. Spika mpya wa Bunge, Anne Makinda alikuwa ameshatangaza awali utaratibu wa wabunge kufika eneo hilo.
Waandishi wa habari za bunge – nikiwa mmoja wao- ambao Spika Makinda hakusikika kueleza utaratibu ambao ungetufikisha Ikulu ndogo ya Chamwino tuliwasiliana na maofisa wa habari wa bunge kuhusu suala hilo. Wakatuelza kuwa utaratibu utaandaliwa.
Kwa sababu ya ukwasi niliokuwa nao niliamua kutumia usafiri binafsi wa kukodi kwenda Chamwino. Sikuwa na shaka yoyote ya kuingia ndani ya viunga vya Ikulu kwa sababu nilikuwa na kitambulisho rasmi cha bunge kinachoniruhusu kufanya kazi zangu kwa mujibu wa taratibu.
Ajabu. Nilipofika Ikulu ya Chamwino nilikuta utaratibu mpya, kwamba waandishi wa habari wanaoruhusiwa kuingia ndani ya Ikulu ni wale tu ambao majina yao yamekuja na Mshana kutoka Dar es Salaam. Nilibutwaa kwa mshangaa.
Waandishi wengi waliokuwa wakitambuliwa rasmi na Bunge kuwa ndiyo wanafanya kazi ya kuripoti habari za bunge katika mkutano huo wa kwanza wa bunge la kumi walizuiliwa na maofisa usalama.
Wachache ambao majina yao yalikuwemo kwenye orodha waliingia na wengine walitumia udanganyifu kwa kutaja majina ya waandishi waliokuwa Dar es Salaam lakini wakiwa kwenye orodha hiyo ya Mshana.
Katika hili, waandishi hawa wachache wa habari walifanikiwa kuwapiga changa la macho maofisa usalama wa taifa. Wanausalama hawakuwa makini kukagua kama majina ya waandishi yaliyo kwenye karatasi ile ya Mshana ndiyo yaliyokuwa kwenye vitambulisho vyao halali.
Nilifurahi sana kuwaona wanausalama wakiwa wametinga suti zao ‘spesheli’ wakiachwa solemba na waandishi wa habari wenye akili na nadhani wenye akili kuliko wao. Watanisamehe sana kama kwa kueleza hili nitakuwa nimewaudhi. Ila ni ukweli kwamba niliwashusha sana.
Mimi niliingia kwa bahati tu, sikuulizwa, nadhani kwa sababu wanausalama walidhani nami ni mwenzao kutokana na mavazi yangu nadhifu. Nilimshukuru Mungu. Nikawaacha waendelee kuzubaa mlangoni.
Lakini nilibaki na swali moja kubwa kichwani. Kuwa, inawezekanaje Mshana, ingawa ndiye mtumishi mkubwa wa maelezo akurupuke tu na kuja na orodha ya waandishi wake kutoka Dar es Salaam wakati akijua kuwa Dodoma kuna timu ya waandishi makini iliyotumwa kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini na kuthibitishwa na ofisi ya Bunge kuwa ndiyo watakaofanya kazi ya kuripoti shughuli za bunge na nyinginezo zitakazo husiana na bunge?
Jibu la haraka lililoniijia akilini ni kwamba inawezekana mtumishi huyu alifanya hivyo kwa sababu shughuli ya kuapishwa Waziri Mkuu ilikuwa ya serikali.
Lakini bado haikuniingia akili kwa sababu sikuona mantiki ya kubeba lundo la waandishi wengine kutoka Dar es Salaam kuja nao Dodoma bila hata kuwajulisha wahariri wao ambao walishatuma waandishi bungeni Dodoma kwenda kufanya kazi zote kubwa za kitaifa wakati mkutano wa kwanza wa bunge la kumi ukiendelea.
Sikuona sababu ya kubeba lundo la waandishi wakati wapo wengine, tena waandishi makini wakiwemo baadhi ya wahariri hapa nchini. Nilifikiria sana bila kupata jibu. Mwisho fikra zangu zikaanza kunielekeza mahali wasikopenda wengi, pa kupuuzia mambo ambayo huwa naamini ni ya kipuuzi.
Nilianza kusikia halafu ya ufisadi kwa mtu huyu anayeitwa Mshana. Kwa sababu mosi; sikuona sababu ya msingi kwake kuchagua waandishi wa kuja nao Dodoma wakati kuna waandishi tayari waliotumwa na vyombo vyao kufanya kazi hiyo.
(b) Kazi ya kuchagua au kutuma waandishi wa habari kwenda kufanya kazi yoyote ya kiuandishi sio ya Mshana, ni ya wahariri ambao kwa hakika ndiyo wanaojua mwandishi yupi anafaa kufanya kazi husika kwa ufanisi.
Pili, baadhi ya waliokuwa kwenye orodha hiyo ya Mshana hawakuwepo wakati wa shughuli hiyo na tatu baadhi ya majina yalikuwa mageni kabisa. Nikajiaminisha japo kwa mashaka kuwa haka ni ka mradi ka ulaji alikokabuni Mshana!
Baada ya kujiaminisha hivyo kwa mara ya kwanza, Mshana nikamuweka kwenye genge la watu ambao mimi huwa ninawatilia shaka sana. Na pale pale nilijisemea moyoni kuwa mtizamo wangu huu hautabadilika mpaka atakapotoa sababu zenye mashiko za kuchukua uamuzi huu ambao kwangu ni wa kipuuzi kabisa.
Haikuishi hapo, baadaye jioni makubwa zaidi ya Mshana yaliibuka kiasi cha kuwafanya waandishi rasmi wa habari za bunge tuliokuwa Dodoma kwa ajili ya shughuli zote za kitaifa katika uzinduzi wa bunge la kumi kumlaani Mshana kila mmoja kwa imani na staili yake.
Ninamshukuru Mungu aliyemteua Mshana kuwa mtumishi kiongozi wa idara ya habari – maelezo hakusikia namna mteule wake alivyokuwa akilaaniwa, kwa sababu angesikia, walah! Mshana hivi sasa angekuwa hana kazi pale maelezo!
Jioni ile, Rais Jakaya Kikwete alikuwa anatoa hotuba ya kuzindua Bunge. Waandishi wa habari za bunge waliokuwa wanapaswa kuwemo bungeni wakati wa hotuba hiyo walikuwa wanafahamika. Bunge lilikuwa limewapa vitambulisho maalumu na walikuwa na eneo lao la kukaa ndani ya ukumbi wa bunge.
Katika hali ya kushangaza, Mshana kwa mara nyingine alikabidhi kwa maofisa usalama waliokuwa wakilinda milango ya bunge orodha ya waandishi wake anayoijua yeye kuwa ndiyo wanaopaswa kuripoti hotuba hiyo ya rais.
Orodha hii ya Mshana haikufahamika ofisi ya Bunge, haikufahamika kwa wahariri na hata waandishi wa habari walioipitia walishangazwa na baadhi ya majina yaliyokuwemo. Waandishi wengi waliokuwa wakitambuliwa na bunge kwa kazi hiyo wakiwemo wapiga picha wakazuiliwa nje.
Hata walipokuja maofisa wa bunge wanaoshughulika na kitengo cha habari na kueleza kuwa shughuli hiyo iko chini yao na wanawafahamu waandishi waliotumwa na vyombo vyao kutoka Dar es Salaam na kuidhinishwa na bunge kwa ajili ya kazi za bunge, wanausalama walikuwa ngangari. Walisema Mshana ameagiza!
Wakati shughuli za jioni za bunge zinaanza, waandishi na wapiga picha karibu wote walikuwa nje. Naibu Spika alipokuwa akiwaapisha baadhi ya wabunge, wapiga picha walikuwa nje, hawakulipata tukio lile. Ilikuwa kituko.
Mimi na waandishi wengine wachache sana tuliokuwa rasmi kwa ajili ya kazi hiyo ndiyo tuliokuwa ndani ya ukumbi wa bunge. Na haikuwa rahisi kuingia kwa sababu Mshana alikuwa amemwaga sumu kali kila upande.
Namshukuru mwandishi Maulid Ahmed wa Habari Leo niliyekuwa nimefuatana naye wakati tukizungushwa huku na huko katika harakati zetu za kutinga mjengoni.
Maulid Ahmed (katikati) akiwa na wanahabari wenzake |
Maneno yake matamu kwa wanausalama na nadhani ulimbwende wake, ulisaidia sana kuwalainisha jamaa wale. Wakapuuza ya Mshana wakasikiliza maneno laini lakini thabiti ya mwandishi huyu, wakaturuhusu kuingia kwenda kufanya kazi.
Maulid alifanya kazi nzuri, natamani kufanya naye kazi nyingine yenye fitna kama hii.
Eneo la waandishi lilikuwa wazi. Baadaye kidogo alikuja ofisa usalama na msululu wa wageni, walikuwa wapambe na wake wa baadhi ya wabunge na kuwaelekeza waketi kwenye viti vya waandishi wa habari, licha ya kumweleza kuwa eneo hilo ni mahususi kwa ajili ya waandishi kufanya kazi zao ndani ya bunge, aliziba pamba masikioni.
Ilibidi waandishi tumkemee mwanausalama huyo wa kike ndipo alipogeuza na kutimka huku akiwaacha wageni wale pale.
Hakuna aliyekuwa na amani moyoni kati yetu waandishi wachache tuliokuwa bungeni jioni ile.
Waandishi wa habari wenye akili tumezoea kufanya kazi kwa ushirikiano, tukicheka na kupigana vijembe vya hapa na pale jambo ambalo husaidia sana kuondoa mchoko wa ubongo hasa katika mazingira magumu ya kazi kama haya ambayo wakati mwingine husababishwa kwa makusudi tu na watu wa aina ya Mshana, waliolewa vyeo ambavyo hawajui watadumu navyo kwa muda gani.
Halikuwa jambo zuri kuanza kupingana na Mshana au kuchukua hatua yoyote ya kutengua maamuzi yake, lakini kwa sababu tulijiridhisha kuwa alichofanya ni upuuzi, tulizungumza na wakubwa wanaomzidi mamlaka, nao walishangazwa na hatua yake hiyo, wakahoji mamlaka yake ndani ya bunge, kwa sababu hapakuwa na muda wa kubishana, walimpuuza, wakawaruhusu waandishi wenzetu waliokuwa nje kwa amri ya Mshana kuingia mjengoni.
Kwa akili yangu ya kichokonozi nilianza kuwashawishi waandishi wenzangu tususie kuripoti hotuba ya Rais Kikwete na kwa sababu ya maudhi ya Mshana. Wengi waliokuwa ndani wakati huo walionekana kukubaliana na ushawishi wangu.
Lakini ni Maulid tena aliyeokoa hali hiyo kwa kueleza kuwa kosa ni la Mshana si la Kikwete. Maulid, ana akili sana.
Akawa amevuruga mpango wangu, vinginevyo kama sio Maulid, siku hiyo ilikuwa ni siku ya Rais Kikwete kususiwa.
Natamani ingetokea hivyo kwa sababu lingekuwa fundisho kwa wote wenye viherehere vya kuingilia majukumu yasiyokuwa yao kiasi cha kuvuruga utaratibu na kulazimisha hata waandishi wa habari ambao kwa kawaida ni wapole sana, kumgomea mkuu wa kaya yao ambaye dunia nzima inafahamu kuwa ana urafiki nao wa damu.