Monday, December 23, 2024
spot_img

MANJI AANZA SAFARI NGUMU KORTINI


Mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji jana alianza safari ngumu ya kujinusuru na tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumkuta na kesi ya kujibu.
Manji ameianza safari hiyo baada ya siku tatu za mnyukano wa kisheria mahakamani kwa upande wa mashtaka na ule wa utetezi ambao hitimisho lake lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha.
Kabla ya Hakimu Mkeha kusoma hukumu ya awali dhidi ya Manji, Septemba 23, mashahidi wawili wa upande wa jamhuri katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili Manji, walitoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha na wakiongozwa na wakili Mkuu wa serikali, Timon Vitalis.
Mashahidi hao walikuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ramadhan Kingai (42), ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa watuhumiwa wa dawa za kulevya waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Shahidi mwingine alikuwa askari wa upelelezi kutoka kanda hiyo, E 1125, Koplo Sospeter(49).
Kingai alidai mahakamni kuwa Februari 9, mwaka huu, alipokea watu wawili waliotajwa kwenye orodha ya Mkuu wa Mkoa kujihusisha na utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.
Aliwataja watu hao kuwa Manji na Askofu Josephat Gwajima ambao aliwahoji na kuwapeleka kwa mkemia mkuu wa serikali kwa ajili kuchukuliwa sampuli ya mkojo ili kuthibitisha madai dhidi yao.
Alidai kuwa baada ya uchunguzi wa mkemia, alitoa ripoti ya uchunguzi ilionyesha kuwa mkojo wa Manji ulikuwa na dawa za kulevya aina ya benzodiazepine huku majibu ya mkojo wa Gwajima yakionyesha kuwa  hatumii dawa za kulevya.
“Mara baada ya kupimwa, mkemia alirudisha majibu ambayo yalionyesha kuwa, mkojo wa Manji umekutwa na dawa za kulevya aina ya benzodiazepine wakati majibu ya Gwajima yalionyesha hatumii dawa za kulevya,” alidai Kingai.
Alidai, mara baada ya kupokea majibu hayo, ofisi yake ilimwachia Gwajima na kumpeleka Manji mahabusu kusubiri jalada lake lipelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka(DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.
Kingai aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa akiwa mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa watuhumiwa wa dawa za kulevya alituma askari kwenda nyumbani kwa Manji kufanya upekuzi lakini hawakupata kitu kinachohusiana na makosa hayo.
Shahidi wa pili Koplo Sospeter yeye alidai mahakamani kuwa alipewa amri ya kumpeleka Manji kwa mkemia Mkuu ili kwenda kuchukuliwa sampuli ya mkojo.
Kioplo Sospeter alidai kuwa wakati anapewa amri hiyo alipewa pia fomu namba 1 ya sheria namba 5, 2015 ya kuwasilisha sampuli ya mkojo kwa mkemia mkuu.
“Mara baada ya kupewa oda ya kumpeleka Manji kupimwa mkojo nilipewa kichupa na fomu ya kujaza ambayo niliisaini, nilipofika kwa mkemia walimpima na kunipa majibu ambayo yalionyesha anatumia dawa za kulevya.
“Majibu hayo niliyapeleka kwa Afande Kingai ili aweze kuendelea na taratibu nyingine kwa sababu mimi kazi yangu ilishia hapo, ”alidai.
Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi juzi kwa ajili ya kuendelea na mashahidi wengine wawili wa upande wa jamhuri.
Agosti 23, mwaka huu kesi hiyo iliendelea kwa mashahidi wa upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi na wa kwanza alikuwa Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dominician Dominic ambaye alidai mahakamani hiyo kuwa leo ripoti ya uchunguzi wa mkojo wa Manji ilionyesha kuwa alikutwa na kemikali aina ya benzodiazepines na morphine.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis, Shahidi huyo alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa Februari 9, 2017 saa 5 asubuhi alipokea Askari akiwa na watuhumiwa wawili kwa ajili ya kutoa sampuli ili kupima mkojo.

Mahojiano baina ya wakili na shahidi yalikuwa hivi;
Wakili Vitalis: Je, unawakumbuka watuhumiwa kwa majina yao na Askari aliyewaleta?

Mkemia: Ndiyo, watuhumiwa waliofikishwa ofisini ni Mchungaji Gwajima na Manji ambao waliletwa na Koplo Sospeter mwenye namba E 1135.

Wakili: Jinsi gani ulianza kufanya uchunguzi?


Mkemia: Kuna maliwato maalum ambayo askari anaingia na mtuhumiwa kutoa sampuli na nilimpatia kontena niliyoipa namba ya maabara 367/2017 ambayo sampuli hii ilikuwa ya Manji.

Wakili: Je, kuna chochote kiliwasilishwa kwako na nani aliwasilisha fomu namba 001?

Mkemia: Sampuli iliwasilishwa na fomu maalumu kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya ambayo Koplo Sospeter ndiye aliyeiwasilisha.

Wakili: Je, ukiiona fomu hiyo utaweza kuitambua? Pia uieleze Mahakama baada ya kuchukua sampuli ya mkojo ulifanya nini?

Mkemia: Fomu hiyo naweza kuitambua kwa kuwa ina saini yangu na jina la mtuhumiwa aliyeletwa kwa ajili ya uchunguzi.

“Nilifanya uchunguzi wa awali kwa kutumika kifaa kinachoitwa Diaquicky Multpanel Urine Test na matokeo yalionyesha kuwa mkojo ulikuwa na kemikali inayoitwa benzodiazepines.

“Kuwepo kwa dawa hizi wakati mwingine hutumika kupunguza maumivu na matumizi mengine kulingana na daktari anavyosema.”

 Wakili: Baada ya hatua ya kwanza ulifanya nini katika hatua ya pili kuthibitisha dawa hizo?

Mkemia: Kemikali hizi zipo za aina nyingi lakini ili kupata majibu kama kweli anatumia dawa za kulevya nilichukua kemikali hiyo na kuunganisha na dawa za kulevya. Katika sampuli hii niligundua kwamba mkojo una kemikali aina ya morphine.

Alidai kemikali hiyo ya Morpine ilikuwa ndani yake na chembechembe ya dawa za kulevya aina ya Heroin. Dawa hii pia hutumika hata wakati wa upasuaji mahospitalini.

Naye wakili wa utetezi, alimuuliza shahidi huyo  iwapo mkojo ni wa Manji au Polisi ambapo alijibu hivi;

Mkemia: Sijui kama mkojo ni wa Manji au Polisi kwa sababu sikwenda nao maliwato wakati wa kutoa sampuli ila nililetewa sampuli na Polisi, nilikuwa nje.

 Wakili Ndusyepo; ulitumia sampuli kiasi gani kufanya uchunguzi hatua ya pili?

Mkemia; Sampuli inayohitajika ni ujazo wa milimita 10.

Jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimkuta Manji na kesi ya kujibu dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya Heroin.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, alitoa uamuzi huo kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa awali.

Hakimu Mkeha alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka na mshtakiwa ana haki ya kujitetea kutokana na mkojo wake kukutwa na dawa aina ya Morphine ambayo zao lake ni Heroin.

“Hivyo mshtakiwa anapaswa kujitetea kwa sababu mahakama imemkuta na hatia,” alisema Hakimu Mkeha.

Baada ya kuelezwa hayo, wakili wa utetezi Hudson Ndusyepo alidai kuwa mshtakiwa atajitetea kwa hati ya kiapo ambapo watakuwa na mashaidi 15 katika kesi hiyo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya