Saturday, April 19, 2025
spot_img

EDWARD LOWASSA, ASIPOKUBALI KUFA, AKAZIKWA HATAFUFUKA


<!–[if !mso]>st1\:*{behavior:url(#ieooui) } <![endif]–>

Lowassa
KUNDI dogo la waombolezaji wa kisisasa limetawanyika katika sehemu mbalimbali za nchi yetu, huku kila mwanakikundi huko aliko akiwa anatoa kilio cha nguvu za kukataa kuwa hakuna msiba wa kisiasa wa Edward Lowassa.
Wana kikundi wa kundi hili dogo wametawanyika sehemu mbalimbali za nchi lakini sauti za vilio vyao ni kali na zenye kuudhi kweli kweli masikioni mwa watu. Wana sauti kali kwa sababu wanakula wanashiba. Kazi yao ya uliaji misibani inawalipa vizuri, hivyo wana uhakika wa kula na kusaza.
Jamaa hawa waombelezaji ni maarufu sana hapa nchini kwa sababu  wanafahamika kutokana na umahili wao wa kulia kwa staili ya maombolezo. 
Na wanafahamika zaidi kwa sababu ya sifa yao ya kupenda kuomboleza vifo vya wakubwa tu, hasa wanaokufa kisiasa kutokana na kashfa, ziwe zile walizozifanya au ambazo hawakuzifanya.
Lowassa, baada ya kuanza kuugua ugonjwa wa kashfa ambao ulimsumbua kwa muda mfupi tu kisha ukamuua kisiasa, waomboleza misiba ya wakubwa walianza kupiga mayowe kuwa  hajafa, amelala tu kujipumzisha lakini baada ya muda ataamka na atawashughulikia bila huruma wote waliomuambukiza maradhi ya kashfa.
Wengine walisikika wakipayuka kuwa amekufa nusu na nusu hajafa, hivyo amekataa kuzikwa.
Kwenye misiba kuna mambo mengi. Yapo ya kusikitisha na wakati mwingine ya kufurahisha. Na katika msiba wa kisiasa wa Lowassa, jambo lililofurahisha kwa waliaji misibani ili wale, ni kupiga mayowe kuwa ile sehemu iliyokufa itafufuka kwa sababu inagangwa na matabibu bora mno unaowafahamu wewe kutoka kila pembe ya nchi yetu.
Ili kuhalalisha upuuzi wao huo wakanitaja na mimi mchokonozi kuwa eti, nimegawiwa vijihela ili niungane na jopo la matabibu wenye majina makubwa hapa nchini bila kujali kama ni mazuri au mabaya, kumpatia tiba Lowassa ili sehemu ya mwili wake iliyokufa ifufuke haraka na pia kutoa dawa ya kinga dhidi ya wale wote wanaotaka kumdhuru.
Waliokuwa wakieneza upuuzi huu walijenga hoja kuwa wapambe wa Lowassa wanatambua ubora wa tiba inayotolewa na safu ya mchokonozi hivyo wasingeweza kuiacha pembeni katika jopo la matabibu waliochaguliwa kumtibu. 
Ilikuwaaminisha watu upuuzi wao huo, walitumia kigezo cha baadhi ya watu walio karibu na Lowassa mwenyewe au jamaa zake ambao ni washirika wangu katika kazi na kwenye kugongeana glass baada ya kazi kuwa ndiyo walionishawishi nikubali kuwemo kwenye jopo la matabibu hao. Na wapo waliothubutu hata kutaja dau la vijehela nilivyopewa kwa kufanya kazi hiyo.
Hizi zilikuwa habari za kusikitisha sana kwangu lakini kwa sababu zilikuwa zikisambazwa na waliaji misibani nilizidharau, jambo ambalo baadaye lilikuja kunigharimu baada ya  upuuzi huo kuaminiwa na wengi.
Sasa hapa niseme kidogo kuhusu mimi. Ni kwamba sijawahi kupewa vijihela kufanya hicho ambacho kimekuwa kikivumishwa kwa muda mrefu sasa. Nasisitiza, sijawahi.
Staili yangu ya maisha na utendaji kazi ni tofauti na wengi wa aina yangu. Nina staili ya kutoeleweka. Nimejisomea  mwenyewe  na nikafanya mtihani ambao nilipojisahihisha nilipata maksi za juu mno katika somo la kutoeleweka. Na hii ndiyo sababu kubwa inayowapa shida wengi kunielewa.
Mashahidi wa hili ni waliowahi au walio karibu yangu. Wanajua kuwa kamwe huwa sikatai takrima kwa sababu huu ni utaratibu wa kawaida kabisa wa kugawana rushwa hapa kwetu, na ninapokumbwa na ukata huwa ninawalazimisha wenye nazo wanipe. Nasema kuwalazimisha, sio kuomba.
Wapo waliojaribu kuninunua na kuambuilia maumivi kwa sababu ni kawaida yangu kutotekeleza makubaliano ya kununuana. 
Na wajinga wachache walioniletea vijihela vya unga unga ili uninase, hao wanajua yaliyowakuta kwa sababu vijihela vyao huwa ninawanyang’anya bila kujali ukubwa wa miili yao.
Huwa ninafanya kazi ya kipolisi kuwadhibiti kwa sababu ni wahalifu. Na hii inaruhusiwa kwetu sisi wachache wenye uwezo huo. 
Kwa sababu hiyo, safu ya mchokonozi haijawahi kumpamba au kumchafua Lowassa kwa sababu zozote za kipuuzi bali imekuwa ikijadili kile inachokiamini kwa maslahi ya wachokonozi wote.
Na kwa Lowassa, nikiri wazi kuwa mbali na kuugua ugonjwa wa kashfa uliomuua kisiasa, kwangu mimi katika uchapakazi, ni Waziri Mkuu ninayemkubali mno na ninaamini kuwa mrithi wake ameshindwa kabisa kuvaa viatu vyake. 
Kaka yangu mwana wa mkulima atanisamehe sana kwa sababu hivi ndivyo ninavyoona kulingana na tathmini yangu. 
Hata hivyo, mwana wa mkulima naye ninamuheshimu sana kwa cheo chake lakini si kwa maneno na matendo yake.  
Lakini pamoja na kumkubali Lowassa kiutendaji, ninaamini pia kuwa hafai hata kidogo kuwa kiongozi kwa sasa kwa sababu amekufa kisiasa. Na hata baadaye kama itawezekana kuja kumkubali ni mpaka atakapokubali kuwa amekufa kisiasa, akubali kuzikwa kisiasa, kisha afufuke akiwa mpya.
Waliaji misibani wanaopayuka sasa kuwa yungali hai wanamdanganya. Na ili aamini kuwa wanamdanganya naandika hapa chini mambo machache ambayo yatamsadikisha.    
lowassa
Kwa kiongozi mwenye hadhi ya Waziri Mkuu, kuchafuliwa kwa kashfa hadi kukubali kuachia ngazi ni sawa na kukubali kuwa umekwisha, kwa maana nyingine ni sahihi kusema nyota ya kisiasa ya mwanasiasa husika imekufa.
Uwaziri mkuu ni wadhfa mkubwa, kwa nchi zetu za Afrika hasa Afrika ya Mashariki, Waziri Mkuu ana mamlaka makubwa mno. Anaweza kuzuia jambo lolote baya linalotaka au linalotokea kwake kwa kutumia ama vyombo vya ulinzi na usalama au hata wapambe wake tu.
Unapoona Waziri Mkuu anachunguzwa na anachunguzika. Kisha ripoti ya uchunguzi wake inatolewa hadharani bila yeye kufanikiwa kuizuia pamoja na mamlaka yote aliyonayo, kwa Tanzania yetu hii. Halafu mkubwa wake anamuacha afe kivyake ni lazima tukubali kuwa kashfa husika inakuwa imemuua kisiasa.
Hivyo wanaodhani kuwa Lowassa baada ya kuangamizwa na kashfa ya Richmond anaweza kuibuka tena, katika mazingira haya ya Watanzania kuchukia kashfa za ubadhilifu na ufisadi unaofanywa na viongozi, wanajidanganya wao mwenyewe na wanamdanganya Lowassa pia.
Jambo jingine lililochangia kufa kwake kisiasa ni ushiriki wake kama mwanamtandao uliomuuingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani. Inawezekana wanaomzungumka hawajui kuwa nayo ni sababu kubwa iliyosababisha kifo chake kisiasa, lakini sisi tulio mbali naye tunajua.
Suala la wanamtandao wa Kikwete kuonekana watu hatari wasiopaswa kupewa nafasi ya kufanya waliyoyafanya mwaka 2005 wakati wa kampeni za urais kuanzia ndani ya chama chao hadi kwa vyama vingine sio jambo la siri tena. Wanachukiwa na wengi, sifa yao imeharibika.
Wanamtandao wanafahamika zaidi sasa kama kundi la wala rushwa waliotumia pesa nyingi kuwahonga wana CCM walioshiriki kupitisha jina la Kikwete kuwa Mgombea wa chama chao. 
Wanafahamika kuwa ni wauaji, ambao wanaweza kukupandikizia kashfa yoyote inayoweza kukupa presha au kulazimisha ukamatwe na wanausalama kwa uzushi wao. Ila mradi tu malengo yao yatimie.
Lowassa ni mmoja wa wanamtandao hata kama hivi sasa ametoswa. Yeye na Kikwete walianza harakati za kuusaka urais tangu wakiwa vijana mno, wakapanga mbinu zao, nzuri na mbaya pamoja.
Kundi la wanamtandao lilipokuwa likipanga mipango mizuri na mibaya ya kuwashughulikia washindani wao katika mbio za urais 2005 kwa kuwachafua kwenye magazeti hata baadhi ya wagombea wakafikia hatua ya kulalama hadharani japo kwa mafumbo kuwa kuna wagombea wanaoweza kutawala kwa mtutu wa bunduki kutokana na staili yao ya kampeni, Lowassa alihusika.
Katika mipango hiyo Lowassa alishiriki moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote ile, hivyo dhambi au sifa yoyote mbaya ya wanamtandao Lowassa haiwezi kuikwepa.
Hivi sasa ambapo Lowassa baada ya kuchafuliwa sana pia yuko katika hatari ya kutupwa na chama chake kwa sababu ya kile kile kinachodaiwa kuwa amekufa kisiasa.
Eti hawezi kufufuka hivyo kuendelea kuwa naye ni kukiua pia chama, anapaswa kutumia busara ya hali ya juu kujitizama upya alikotoka, alipo sasa ana anakokusudia kwenda.
Anapaswa kukubali ukweli kuwa kisiasa amekufa, akubali kuzikwa. Iwapo atakubali kufa na kuzikwa atakuwa na uhakika wa kufufuka, na haina shaka kuwa atafufuka akiwa mpya hivyo atakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuendelea na safari yake ndefu ya kisiasa.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya