Sunday, June 22, 2025
spot_img

SERIKALI ILIVYOIBIWA TANZANITE MKONONI


Na Mwandishi Wetu
MAOFISA wa Serikali waliokuwa katika chumba cha kuchenjulia madini cha mgodi wa TanzaniteOne, uliopo Mererani mkoani Manyara Juni 20, 2017, wanadaiwa kuhadaiwa na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates Limited na kuibiwa ndoo iliyokuwa imejaa madini ya tanzanite.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo anayetajwa kuwahadaa maofisa hao ambao majina na nyadhifa zao tunayahifadhi kwa sasa, ni Faisal Juma Shahbhai.
Kwamba Shahbhai akiwa na wakurugenzi wenzake na maofisa wa Serikali kabla ya kuanza ukaguzi wa ndoo sita za madini katika chumba cha ukaguzi wa madini cha mgodi wa TanzaniteOne, alitoa jiwe kubwa linalodhaniwa kuwa madini na kulionyesha.
Imeelezwa kuwa jiwe hilo liliwaduwaza maofisa wa Serikali ambao walibaki kulikodolea macho na wakiwa katika hali hiyo, ndoo inayodaiwa kujaa tanzanite ilivutwa na mmoja wa washirika wa Shahbhai na kufichwa.

Taarifa za Shahbhai kuwaduwaza maofisa hao ili kuwawezesha washirika wake kukwapua kiasi kikubwa cha madini hayo, zimepatikana ndani ya mgodi wa TanzaniteOne ambao ni mmoja wa wakurugenzi wake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mkakati wa kuibwa kwa ndoo hiyo ya madini uliratibiwa Juni 20, mwaka huu kabla ya kutekelezwa Juni 21. Mbali na Shahbhai, wakugerenzi wengine wa kampuni hiyo ya Sky waliokuwa ndani ya chumba cha ukaguzi ni Hussein Gonga na Rizwan Ullah.
Mmoja wa watoa taarifa kutoka ndani ya mgodi huo, ambaye amefanya mahojiano na Mikito Blog kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa, alisema: “Hiyo story ni ya kweli. Kinachozungumzwa ni kweli.
“Lakini kuna mambo ambayo yanaendelea sasa hivi ya kiserikali na sisi ambao tunalifahamu hilo suala vizuri, tungependa tuiachie Serikali kwanza imalize uchunguzi wake kwa sababu kuna kasoro nyingi zimekwishatokea kuhusu hiyo kampuni kipindi cha nyuma, lakini nyingi zimekuwa zikiishia njiani.
“Kama unavyoona, hii ilivyotokea wakaitwa waandishi wa habari, hatujui walipewa nini wakaenda wakakanusha wao hao hao ambao walisema hiyo kitu ni kweli. 
“Sasa tumeona ili hizi longo longo zisiendelee, tuiachie Serikali ikamilishe uchunguzi wake, baada ya hapo sisi tutaendelea kuongea kilichotokea kwa usalama wetu na kuhahakisha kuwa hili jambo linafika mwisho.
“Kwa sababu hawa jamaa wanafuatilia sana magazeti, kila kinachotoka kwenye magazeti wanakuwa hatua moja mbele, wanajua wafanye nini, wanajua waende wakazuie wapi.”
Alipoulizwa jinsi tukio hilo lilivyotokea, huku akikataa kueleza kinaga ubaga, alisema: “Ninaweza nikakupa ‘hint’, lakini siwezi kukueleza mambo mengi kwenye simu kwa sababu za kiusalama na hii simu inafuatiliwa kwa sababu mimi ninahusika kwa kiasi fulani na hilo tukio.
“Hao jamaa ni kweli walifanya hilo tukio. Ilikuwa ni tarehe 20 na tarehe 21 ndiyo waliweza kutoa huo mzigo. Sasa kuna vipande vya ‘footage’ vimesambaa hapa mjini vikionyesha namna mpango huo ulivyotekelezwa, lakini pia wapo ambao wana ‘footage’ zinazoonyesha tukio zima kuanzia tarehe 20 wakijiandaa kufanya hilo tukio, tarehe 21 mzigo ule ukitolewa ‘ghalani’ na kuingizwa kwenye gari pamoja na yule mhusika aliyebeba lile dumu, mhindi aliyehusika mpaka gari linatoka nje ya kampuni.
“Kwenye ‘footage’ wahusika wote wanaonekana, anaonekana Faisal, anaonekana Gonga na Rizwan, wote walikuwa wamekaa kwenye meza, wanaonekana.
“Wakurugenzi wa kampuni wanaruhusiwa kuingia kwenye chumba cha kuchenjulia madini. Wanaingia wakati mzigo unapokatwa utepe ukitoka mgodini kuangalia kilichopo ndani kabla ya kutoa ruhusa uanze kufanyiwa usafi na taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuupanga.
“Katika tukio hili wafanyakazi pia wanahusika, wakiwemo walinzi kwa sababu wapo ambao wamekuwa wakieleza jinsi mchezo mzima ulivyofanyika.
“Jinsi madini hayo yalivyoibwa ni kwamba wale wakurugenzi walikuwa wamekaa kwenye meza pamoja na wale watu wa Serikali. Sasa kabla ya kuanza kukagua zile ndoo, Shahbhai alitoa jiwe fulani akawaonyesha wale watu wa Serikali ambao walianza kuliangalia kwa mshangao.
“Huku nyuma maofisa wale walipokuwa wakishangaa jiwe lile, mhindi mmoja aliyekuwa mle ndani, alilivuta lile dumu kwa chini chini akampatia mwenzake kwa nyuma akalipeleka chumba kingine wakati wale maofisa wa Serikali wakiendelea kushangaa jiwe walilokuwa wakionyeshwa na Shahbhai.
“Hivyo watu wa Serikali hawakuona jinsi lile dumu lilivyotoroshwa na lilivyotolewa likapelekwa hadi kwenye chumba cha pili na yule mhindi akaenda kulifungia huko, ndiyo wakarudi wakaendelea na shughuli nyingine kama kawaida.
“Haya yote kwenye ‘footage’ yanaonekana na mtu yeyote akiiona hata kama hajui masuala ya wizi, atajua ni namna gani mchezo ulivyochezwa.”
Arafat
Mdogo wake Shahbhai ambaye katika mahojiano na Mikito Blog alijitambulisha kwa jina la Arafat, alipoulizwa kuhusu tukio hilo baada ya jina lake kutajwa, alikana kuhusika kwa kueleza kuwa siku inayodaiwa wizi huo kufanyika yeye alikuwa mgonjwa.
 “Mimi siku ya tukio inayosemwa nilikuwa naumwa, ni kweli nilitoka mgodini, lakini sikuwa eneo la tukio. Hapa kuna maneno mengi sana na fitina nyingi sana.
“Siku ambayo tukio linadaiwa kutokea ilikuwa mwezi wa Ramadhani, mimi nilikuwa nimefunga. Nina matatizo ya kifua na nilikuwa nimefunga. Nilitoka asubuhi nikaenda nikachukua dawa nikarudi nyumbani, lakini usiku tena nikabanwa nikaenda tena kuchukua dawa.
“Nilitoka kwenye saa tatu asubuhi nikaenda nikachukua dawa yangu nikarudi, usiku tena baada ya kufuturu tu nikashindwa tena kupumua nikaenda zangu mjini kuchukua dawa. 
“Sikuwa kwenye chumba cha kuchenjulia kabisa na huyo Yusuf (Mhagama) wanayesema nilikuwa naye mimi sikuwa naye.”
Akiendelea kujitetea, alisema kuwa huenda taarifa hizo zimezushwa kutokana na ukali wake katika kusimamia ulinzi.
“Niko upande wa ulinzi na tunabana watu na ukweli watu hapa hawanipendi kwa sababu tuko wakali.
“Taratibu zinaturuhusu kuingia mgodini, lakini kwenye chumba cha kuchenjulia madini mimi huwa siingii. Kazi yangu ni kuhakikisha usalama kuanzia mgodini hadi kwenye chumba cha kuchenjulia madini.
“Mimi mwenyewe sipendi kuingia kwenye chumba cha kuchenjulia lakini ninaruhusiwa ila sijaenda kwa muda wa miezi kama minne hivi,” alisema Arafat.
Wakati Arafat akieleza hayo, mtoa taarifa mwingine kutoka ndani ya mgodi wa TanzaniteOne ameieleza Mikito Blog kuwa siku ya tukio Arafat alikuwa mgodini akisimamia mitambo ya ulinzi na baada ya gari lililokuwa na ndoo ya tanzanite iliyoibwa kutolewa ndani ya eneo la mgodi, ndipo akaondoka kwenye eneo alilolitaja kuwa ni ‘control room.’
Arafat alipoulizwa kama baada ya tukio hilo alisafiri kwenda Nairobi, Kenya kama tetesi zilivyosambaa katika Jiji la Arusha, Arafat aliruka kimanga kwa kueleza kuwa hajasafiri kwenda nchini huko.
Shahbhai

Tayari Shahbhai anayedaiwa kuwahadaa maofisa wa Serikali amekwishaeleza kuwa ni kweli yeye pamoja na wakurugenzi wanzake, Gonga na Rizwan walikuwa katika chumba cha kuchenjulia madini siku inayodaiwa kutokea kwa wizi huo.

Shahbhai ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo, pamoja na mambo mengine alisema: “Hiyo ndiyo kazi yetu sisi, mimi kuwa maeneo hayo au kuwa na madini ni sawa kabisa, kati ya tarehe 19 au 20 ni kweli nilikuwa kwenye shughuli ya uchenjuaji wa madini. Kuwa katika maeneo yangu ya kazi ya kuchenjua madini si jambo la ajabu kwangu kwa sababu ndiyo shughuli zangu.

“Ni kweli Arafat ni mdogo wangu wa damu, kuna mambo mengi ya msingi yanayoweza kujenga taifa ya kuandika huku Mirerani badala ya haya ya uongo uongo.

“Yaani gari iende ibadilishwe huko iweje sasa, kwa nini mtu hata kama anataka kitu asiende na gari hiyo hiyo? Watanzania hawajui kitu, hawajui kabisa biashara ya tanzanite, wako ‘very blind’ kwenye biashara hiyo.

“Tunapowaambia vitu, tuwaambie ambavyo kesho hata mwenyezi Mungu akisimama tuweze kusimama kujibu kwamba Mola nilichokisema kiko sawa. Yupo mwandishi alikuja Mirerani kufuatilia suala hili na alikaa hapa kwa muda wa siku tatu, lakini nilimshauri aandike vitu ambavyo vitasaidia jamii ya Watanzania.

“Ni jambo jema kama waandishi wa habari watakuwa wanawajuza watu vitu ambavyo vitajenga uchumi wa taifa kwa sababu hizo taarifa hazijakaa vizuri sana. Katika biashara hii tuna tofauti kubwa na wafanyabiashara wenzetu. 

“Baada ya kuingia kwenye uwekezaji wa biashara ya tanzanite, tumekuwa na ugomvi mkubwa na wachimbaji wadogo kwa sababu maeneo mengi wanayochimba walikuwa wanachimba upande wetu. Nakuhakikishia jambo hilo si la kweli, ni fitina tu.”

Vigogo wa Kampuni ya Sky Associates Limited wanadaiwa kuhusika na utoroshaji wa madini ya tanzanite yenye thamani ya mabilioni ya shilingi kutoka katika mgodi wa TanzaniteOne uliopo Mererani mkoani Manyara.

Kwamba Shahbhai na wenzake walitekeleza mpango huo Juni 21 kwa kuyasafirisha madini hayo kwa kutumia gari aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T 710 BWT ambalo ni mali ya Kampuni ya TanzaniteOne, lililokuwa likiendeshwa na Yusuf Mhagama ambaye ni mfanyakazi wa kampuni hiyo.

Taarifa zilinai kuwa Mhagama ambaye alikuwa ameambatana na Arafat katika safari hiyo, waliyashusha madini hayo kabla ya kufika Arusha mjini na kuyapakia kwenye gari jingine aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T 492 BSS.

Mikito Blog inaendelea na uchunguzi wa sakata hili.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya